< Zekaria 5 >

1 Nikatazama tena: na hapo mbele yangu kulikuwa na kitabu kilichoruka!
Kisha nikageuka na kuinua macho yangu, nami nikaona, tazama, gombo lirukalo!
2 Akaniuliza, “Unaona nini?” Nikamjibu, “Naona kitabu kinachoruka chenye, urefu wa dhiraa ishirini na upana wa dhiraa kumi.”
Malaika akaniuliza, “Unaona nini?” Nikajibu, “Ninaona gombo lirukalo, urefu wake dhiraa ishirini na upana wake dhiraa kumi.”
3 Akaniambia, “Hii ni laana inayotoka kwenda juu ya nchi yote, kwa kuwa kufuatana na yale yaliyoandikwa katika upande mmoja, kila mwizi atafukuziwa mbali, pia kufuatana na yaliyo upande wa pili, kila aapaye kwa uongo atafukuziwa mbali.
Ndipo aliponiambia, “Hii ni laana iendayo juu ya uso wa nchi yote, kwani tangu sasa kila mwivi ataondolewa kulingana na lisemavyo upande mmoja, wakati kila aapaye kiapo cha uongo ataondolewa kulingana na lisemavyo upande mwingine, kwa kadili ya maneno yake.
4 Bwana Mwenye Nguvu Zote asema, ‘Nitaituma hiyo laana, nayo itaingia katika nyumba ya mwizi na nyumba ya huyo aapaye kwa uongo kwa Jina langu. Itabaki katika nyumba yake na kuiharibu, pamoja na mbao zake na mawe yake.’”
“Nitalituma - asema Yahwe wa majeshi - hivyo litaingia nyumbani mwa mwivi na nyumbani mwa aapaye kwa uongo kwa jina langu. Litasalia nyumbani mwake na kuteketeza mbao na mawe yake.”
5 Kisha yule malaika aliyekuwa akizungumza nami akanijia na kuniambia, “Tazama juu uone ni nini kile kinachojitokeza.”
Ndipo malaika aliyekuwa akisema nami alipoenda nje na kuniambia, “Inua macho yako uone kinachokuja!”
6 Nikamuuliza, “Ni kitu gani?” Akanijibu, “Ni kikapu cha kupimia.” Kisha akaongeza kusema, “Huu ni uovu wa watu katika nchi nzima.”
Nikasema, “Ni nini hiki?” Akasema, “Hiki ni kikapu kilicho na efa ijayo. Huu ni uovu wao katika nchi yote.”
7 Kisha kifuniko kilichotengenezwa kwa madini ya risasi kilichokuwa kimefunika kile kikapu, kiliinuliwa na ndani ya kile kikapu alikuwako mwanamke ameketi!
Kisha mfuniko wa risasi ukainuliwa kutoka ndani ya kikapu na kulikuwa na mwanamke chini yake amekaa ndani yake!
8 Akasema, “Huu ni uovu,” tena akamsukumia ndani ya kikapu na kushindilia kifuniko juu ya mdomo wa kikapu.
Malaika akasema, “Huu ni uovu!” na akamtupa tena kikapuni, na kurusha mfuniko wa risasi mlango pake.
9 Kisha nikatazama juu: na pale mbele yangu, walikuwepo wanawake wawili, wakiwa na upepo katika mabawa yao! Walikuwa na mabawa kama ya korongo, nao wakainua kile kikapu na kuruka nacho kati ya mbingu na nchi.
Nilipoinua macho nikaona wanawake wawili wakija kwangu, na upepo ulikuwa ndani ya mabawa yao - walikuwa na mabawa kama mabawa ya korongo. Wakainua kikapu kati ya mbingu na nchi.
10 Nikamuuliza yule malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Wanakipeleka wapi hicho kikapu?”
Hivyo nikamwuliza malaika aliyesema nami, “Wanapeleka wapi kikapu?”
11 Akanijibu, “Wanakipeleka katika nchi ya Babeli na kujenga nyumba kwa ajili yake. Itakapokuwa tayari, kikapu kitawekwa pale mahali pake.”
Akaniambia, “Wanakwenda kujengea hekalu katika nchi ya Shinari kwa ajili yake, hekalu litakapokuwa tayari, kikapu kitawekwa kwenye msingi ulioandaliwa kwa ajili yake.”

< Zekaria 5 >