< Zekaria 14 >
1 Siku ya Bwana inakuja ambayo nyara zilizotekwa kwenu zitagawanywa miongoni mwenu.
Tazama! Siku ya Yahwe inakuja wakati mateka wenu watakapogawanywa katikati yenu.
2 Nitayakusanya mataifa yote huko Yerusalemu kupigana dhidi yake, mji utatekwa, nyumba zitavamiwa na kuporwa na wanawake watanajisiwa. Nusu ya mji watakwenda uhamishoni, lakini watakaobaki hawataondolewa kutoka mjini.
Kwa maana nitayakusanya mataifa yote kinyume cha Yerusalemu kwa vita na mji utatekwa. Nyumba zitatekwa na wanawake watabakwa. Nusu ya mji itapelekwa matekani, lakini kumbukumbu ya watu haitaondolewa mjini.
3 Kisha Bwana atatoka na kupigana dhidi ya watu wa yale mataifa, kama apiganavyo siku ya vita.
Lakini Yahwe ataondoka na kufanya vita dhidi ya mataifa kama apigavyo vita katika siku ya vita.
4 Siku hiyo miguu yake itasimama juu ya Mlima wa Mizeituni, mashariki mwa Yerusalemu, nao Mlima wa Mizeituni utagawanyika mara mbili kuanzia mashariki hadi magharibi, ukifanya bonde kubwa, nusu ya mlima ukisogea kuelekea kaskazini na nusu kuelekea kusini.
Siku hiyo miguu yake itasimama juu ya Mlima wa Mizeituni, uliopo kando ya Yerusalemu upande wa mashariki. Mlima wa Mizeituni utagawanyika katikati kati ya mashariki na magharibi kwa bonde kubwa sana na nusu ya mlima itarudi nyuma kuelekea kaskazini na nusu kuelekea kusini.
5 Nanyi mtakimbia kupitia katika bonde hilo la mlima wangu kwa kuwa litaenea hadi Aseli. Mtakimbia kama mlivyokimbia tetemeko la ardhi katika siku za Uzia mfalme wa Yuda. Kisha Bwana Mungu wangu atakuja na watakatifu wote pamoja naye.
Ndipo mtakapokimbia katika bonde kati ya milima ya Yahwe, kwa kuwa bonde kati ya hiyo milima litafika hata Azali. Mtakimbia kama siku mliyokimbia tetemeko la nchi siku za Uzia, mfalme wa Yuda. Ndipo Yahwe Mungu wangu atakapokuja na watakatifu wake wote.
6 Siku hiyo hakutakuwepo nuru, baridi wala theluji.
Hakutakuwa na nuru katika siku hiyo, lakini hakuna baridi wala barafu.
7 Itakuwa siku ya kipekee, isiyo na mchana wala usiku, siku ijulikanayo na Bwana. Jioni inapofika nuru itakuwepo.
Siku hiyo, siku aijuaye Yahwe peke yake, hakutakuwa tena na mchana wala usiku, kwani jioni itakuwa wakati wa nuru.
8 Siku hiyo, maji yaliyo hai yatatiririka kutoka Yerusalemu, nusu kwenda kwenye bahari ya mashariki, na nusu kwenda kwenye bahari ya magharibi wakati wa kiangazi na wakati wa masika.
Siku hiyo maji yaliyo hai yatatiririka kutoka Yerusalemu. Nusu yake yatatiririka kuelekea bahari ya mashariki na nusu bahari ya magharibi, wakati wa masika na wakati wa kiangazi.
9 Bwana atakuwa mfalme juu ya dunia yote. Katika siku hiyo atakuwepo Bwana mmoja na jina lake litakuwa jina pekee.
Yahwe atakuwa mfalme juu ya dunia yote. Katika siku hiyo kutakuwa na Yahwe, Mungu mmoja, na jina lake pekee.
10 Nchi yote kuanzia Geba, kaskazini mwa Yuda, hadi Rimoni, kusini mwa Yerusalemu, itakuwa kama Araba. Lakini Yerusalemu utainuliwa juu na kubaki mahali pake, toka Lango la Benyamini hadi mahali pa Lango la Kwanza, mpaka kwenye Lango la Pembeni na kutoka Mnara wa Hananeli hadi kwenye mashinikizo ya divai ya mfalme.
Nchi yote itakuwa kama Araba, kuanzia Geba hadi Rimoni kusini mwa Yerusalemu. Na Yerusalemu itaendelea kuwa juu. Ataishi mahali pake mwenyewe, kutoka lango la Benjamini hata mahali lilipokuwa lango la kwanza, hata Lango la Pembeni, na kutoka Mnara wa Hananeli hata shinikizo la mfalme.
11 Utakaliwa na watu, kamwe hautaharibiwa tena, Yerusalemu utakaa salama.
Watu watakaa Yerusalemu na hakutakuwa na maangamizi kamili tena kutoka kwa Mungu dhidi yao. Yerusalemu itakuwa salama.
12 Hii ndiyo tauni ambayo Bwana atapiga nayo mataifa yote ambayo yalipigana dhidi ya Yerusalemu: Nyama ya miili yao itaoza wangali wamesimama kwa miguu yao, macho yao yataoza kwenye matundu yake na ndimi zao zitaoza vinywani mwao.
Hii itakuwa tauni ambayo kwayo Yahwe atawapiga jamaa zote za watu wapigao vita juu ya Yerusalemu: miili yao itaoza hata wakiwa wamesimama kwa miguu yao. Macho yao yataoza katika matundu yake na ndimi zao zitaoza katika vinywa vyao.
13 Katika siku hiyo Bwana atawatia wanaume hofu kuu. Kila mwanaume atakamata mkono wa mwenzake nao watashambuliana.
Siku hiyo ile hofu kuu kutoka kwa Yahwe itakuwa miongoni mwao. Kila mmoja ataushika mkono wa mwingine, na mkono wa mwingine utainuliwa kinyume cha mkono wa mwenzake.
14 Yuda pia atapigana katika Yerusalemu. Utajiri wa mataifa yote yanayoizunguka Yerusalemu utakusanywa, wingi wa dhahabu, fedha na nguo.
Yuda pia atapigana na Yerusalemu. Watakusanya utajiri wa mataifa yote yanayowazunguka - dhahabu, fedha, na wingi wa nguo safi.
15 Tauni ya aina iyo hiyo itapiga farasi na nyumbu, ngamia na punda, nao wanyama wote walioko kwenye kambi za adui.
Tauni itakuwa pia juu ya farasi na nyumbu, ngamia na punda, na kila mnyama katika kambi hizo atapigwa kwa hilo pigo.
16 Kisha walionusurika katika mataifa yote ambayo yaliushambulia Yerusalemu watakuwa wakipanda Yerusalemu kila mwaka kumwabudu Mfalme, Bwana Mwenye Nguvu Zote na kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda.
Kisha itakuwa wote watakaosalia katika mataifa yaliyo kinyume na Yerusalemu watakwenda mwaka kwa mwaka kumwabudu mfalme, Yahwe wa majeshi, na kutunza Sikukuu ya Vibanda.
17 Ikiwa taifa lolote la dunia hawatakwenda Yerusalemu kumwabudu Mfalme, Bwana Mwenye Nguvu Zote, mvua haitanyesha kwao.
Na itakuwa kwamba ikiwa mtu yeyote kutoka katika mataifa yote ya dunia haendi Yerusalemu kumwabudu mfalme, Yahwe wa majeshi, ndipo Yahwe hataleta mvua juu yao.
18 Ikiwa watu wa Misri nao hawatakwenda kushiriki, hawatapata mvua. Bwana ataleta juu yao tauni ile ambayo itawapiga mataifa yale ambayo hayatakwenda kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda.
Na ikiwa nchi ya Misri hawatakwenda, ndipo hawatapata mvua. Tauni kutoka kwa Yahwe itayashambulia mataifa yote yasiyokwea kutunza Sikukuu ya Vibanda.
19 Hii itakuwa adhabu ya Misri na adhabu ya mataifa yote yale ambayo hayatakwenda Yerusalemu kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda.
Hii itakuwa ni adhabu kwa Misri na adhabu kwa kila taifa lisilopanda kutunza Sikukuu ya Vibanda.
20 Katika siku hiyo, kengele zilizofungwa kwenye farasi zitaandikwa maneno haya: Takatifu kwa Bwana, navyo vyungu vya kupikia katika nyumba ya Bwana vitakuwa kama bakuli takatifu mbele ya madhabahu.
Lakini katika siku hiyo, kengele za farasi zitasema, “Jitengeni kwa ajili ya Yahwe,” na makalai katika nyumba ya Yahwe yatakuwa kama mabakuri mbele ya madhabahu.
21 Kila chungu kilichoko Yerusalemu na Yuda kitakuwa kitakatifu kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote na wote wanaokuja kutoa dhabihu watachukua baadhi ya vyungu hivyo na kupikia. Katika siku hiyo hatakuwepo tena mfanyabiashara katika nyumba ya Bwana Mwenye Nguvu Zote.
Kwa kuwa kila chungu katika Yerusalemu na Yuda kitatengwa kwa ajili ya Yahwe wa majeshi na kila mmoja aletaye sadaka atakula ndani yake na kuyachemshia. Hakutakuwa na wafanyabiashara tena katika nyumba ya Yahwe wa majeshi siku hiyo.