< Zekaria 11 >

1 Fungua milango yako, ee Lebanoni, ili moto uteketeze mierezi yako!
Fungua milango yako, ee Lebanoni, ili moto uteketeze mielezi yako!
2 Piga yowe, ee mti wa msunobari, kwa kuwa mwerezi umeanguka; miti ya fahari imeharibiwa! Piga yowe, enyi mialoni ya Bashani, msitu mnene umefyekwa!
Omboleza, enyi miti ya misonobari, kwani mierezi imeanguka! Kilichokuwa cha fahari kimeteketezwa! Ombolezeni, enyi mialoni ya Bashani, kwani msitu wenye nguvu umeshushwa.
3 Sikiliza yowe la wachungaji; malisho yao manono yameangamizwa! Sikia ngurumo za simba; kichaka kilichostawi sana cha Yordani kimeharibiwa!
Wachungaji wanapiga yowe, kwa kuwa utukufu wao umeharibiwa! Sauti ya mungurumo wa wana simba, kwa kuwa kiburi cha Mto Yordani kimeharibiwa!
4 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu wangu: “Lilishe kundi lililokusudiwa kuchinjwa.
Hivi ndivyo asemavyo Yahwe Mungu wangu, “Lichungeni kundi la kondoo lililotiyari kuchinjwa!
5 Wanunuzi wake huwachinja na kuondoka pasipo kuadhibiwa. Wale wanaowauza husema, ‘Bwana asifiwe, mimi ni tajiri!’ Wachungaji wao wenyewe hawawahurumii.
(Wanaowanunua wanawachinja bila kuhadhibiwa, nao wawauzao husema, 'Atukuzwe Yahwe! Nimetajirika! Kwa maana wachungaji wafanyao kazi kwa wenye kondoo hawawahurumii.)
6 Kwa kuwa sitawahurumia tena watu wa nchi,” asema Bwana. “Nitawakabidhi kila mtu mkononi mwa jirani yake na mfalme wake. Wataitenda jeuri nchi, nami sitawaokoa kutoka mikononi mwao.”
Kwa maana hiyo sitawahurumia tena wenyeji wa nchi! - hivi ndivyo asemavyo Yahwe. Tazama! Mimi mwenyewe nipo tiyari kumwelekeza kila mtu katika mkono wa jirani yake na katika mkono wa mfalme wake, nao wataiharibu nchi na hakuna hata mmoja wao nitakayemwokoa kutoka katika mkono wao.”
7 Kwa hiyo nikalilisha kundi lililotiwa alama kwa kuchinjwa, hasa kundi lililoonewa sana. Kisha nikachukua fimbo mbili, moja nikaiita Fadhili na nyingine Umoja, nami nikalilisha kundi.
Hivyo nikawa mchungaji wa kondoo walioamriwa kuchinjwa, kwa wanaowashughulikia kondoo. Nilichukua fimbo mbili; fimbo moja nikaiita “Neema” na nyingine nikaiita “Umoja.” Kwa njia hii niliwachunga kondoo.
8 Katika mwezi mmoja nikawaondoa wachungaji watatu. Kundi la kondoo likanichukia, nami nikachoshwa nao,
Ndani ya mwezi mmoja niliwaangamiza wachungaji watatu, kwa maana sikuwavumilia tena, wao pia walinichukia.
9 nikasema, “Sitakuwa mchungaji wenu. Waache wanaokufa wafe na wanaoangamia waangamie. Wale waliobakia kila mmoja na ale nyama ya mwenzake.”
Ndipo nilipowaambia wamiliki, “Sitafanya kazi kama mchungaji wenu tena. Wakondoo wafao - na wafe; kondoo wanaoangamizwa - na waangamizwe. Na kondoo wasaliao kila mmoja ale nyama ya jirani yake.”
10 Kisha nikachukua fimbo yangu inayoitwa Fadhili nikaivunja, kutangua Agano nililofanya na mataifa yote.
Hivyo nikaichukua fimbo yangu “Neema” na nikaivunja kuvunja agano nililokuwa nimelifanya na kabila zangu zote.
11 Likatanguka siku hiyo, kwa hiyo wale waliodhurika katika kundi, waliokuwa wakiniangalia wakajua kuwa hilo lilikuwa neno la Bwana.
Katika siku hiyo agano lilivunjwa, na wale wanaoshughulika na kondoo na waliokuwa wakiniangalia walifahamu kwamba Yahwe amesema.
12 Nikawaambia, “Mkiona kuwa ni vyema, nipeni ujira wangu, la sivyo, basi msinipe.” Kwa hiyo wakanilipa vipande thelathini vya fedha.
Nikawaambia, “Ikiwa itawapendeza, nilipeni ujira wangu. Kama sivyo, msifanye hivyo.” Hivyo wakapima ujira wangu - vipande thelathini vya fedha.
13 Naye Bwana akaniambia, “Mtupie mfinyanzi,” hiyo bei nzuri waliyonithaminia! Kwa hiyo nikachukua hivyo vipande thelathini vya fedha na kumtupia huyo mfinyanzi katika nyumba ya Bwana.
Kisha Yahwe akaniambia, “Weka fedha katika hazina, thamani nzuri zaidi ambayo walikupa!” Hivyo nikachukua vipande thelathini vya fedha na kuviweka katika hazina ndani ya nyumbani Yahwe.
14 Kisha nikaivunja fimbo yangu ya pili iitwayo Umoja, kuvunja undugu kati ya Yuda na Israeli!
Kisha nikavunja fimbo yangu ya pili, “Umoja,” kuvunja undugu kati ya Yuda na Israeli.
15 Kisha Bwana akaniambia, “Vitwae tena vifaa vya mchungaji mpumbavu.
Yahwe akaniambia, “Tena, chukua chombo cha mchungaji mpumbavu kwa ajili yako mwenyewe,
16 Kwa maana ninakwenda kumwinua mchungaji juu ya nchi ambaye hatamjali aliyepotea, wala kuwatafuta wale wachanga au kuwaponya waliojeruhiwa, wala kuwalisha wenye afya, lakini atakula nyama ya kondoo wanono na kuzirarua kwato zao.
kwa maana tazama, niko tiyari kumweka mahali mchungaji katika nchi. Hataangalia kondoo wanaoangamia. Hatatafuta kondoo wapoteao, wala kuwaponya kondoo wachechemeao. Hatawalisha kondoo wenye afya, lakini atakula nyama ya kondoo walionona naye atapasua kwato zao.
17 “Ole wa mchungaji asiyefaa, anayeliacha kundi! Upanga na uupige mkono wake na jicho lake la kuume! Mkono wake na unyauke kabisa, jicho lake la kuume lipofuke kabisa!”
Ole kwa wachungaji wasiofaa wanaoliacha kundi la kondoo! Upanga na uje dhidi ya mkono wake na jicho lake la kulia! Mkono wake na ukauke na jicho lake la kulia lipofuke!

< Zekaria 11 >