< Zekaria 10 >
1 Mwombeni Bwana mvua wakati wa vuli; ndiye Bwana atengenezaye mawingu ya tufani. Huwapa watu manyunyu ya mvua, pia mimea ya shambani kwa ajili ya kila mtu.
Mwombeni Yahwe mvua nyakati za kipupwe - Yahwe afanyaye mvua ya radi - naye hufanya mvua inyeshe kwa kila mmoja na uoto kondeni.
2 Sanamu huzungumza udanganyifu, waaguzi huona maono ya uongo; husimulia ndoto ambazo si za kweli, wanatoa faraja batili. Kwa hiyo watu wanatangatanga kama kondoo walioonewa kwa kukosa mchungaji.
Kwani sanamu za wenye nyumba husema uongo; waganga hunena uongo; wanasema ndoto za udanganyifu na hutoa faraja tupu, hivyo wapotea kama kondoo na wanaumia kwa sababu hakuna mchungaji.
3 “Hasira yangu inawaka dhidi ya wachungaji, nami nitawaadhibu viongozi; kwa kuwa Bwana Mwenye Nguvu Zote atalichunga kundi lake, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi mwenye kiburi akiwa vitani.
Gadhabu yangu inawaka dhidi ya wachungaji; ni mabeberu - viongozi - nitakao waadhibu. Yahwe wa majeshi atalihudumia pia kundi la kondoo wake, nyumba ya Yuda, na kuwafanya kama farasi wake wa vita!
4 Kutoka Yuda litatokea Jiwe la pembeni, kutoka kwake vitatoka vigingi vya hema, kutoka kwake utatoka upinde wa vita, kutoka kwake atatoka kila mtawala.
Kutoka kwao litatoka jiwe kuu la pembeni; kutoka kwao kitatoka kigingi cha hema; kutoka kwao utatoka upinde wa vita; kutoka kwao watakuja viongozi wote kwa pamoja.
5 Kwa pamoja watakuwa kama mashujaa wanaokanyaga barabara za matope wakati wa vita. Kwa sababu Bwana yu pamoja nao, watapigana na kuwashinda wapanda farasi.
Watakuwa kama mashujaa wawakanyagao adui zao katika matope ya mitaani vitani; watafanya vita, kwa maana Yahwe yu pamoja nao, nao watawaabisha wapanda farasi wa vita.
6 “Nitaiimarisha nyumba ya Yuda na kuiokoa nyumba ya Yosefu. Nitawarejesha kwa sababu nina huruma juu yao. Watakuwa kama watu ambao sijawahi kuwakataa kwa sababu mimi ndimi Bwana Mungu wao, nami nitawajibu.
Nitaitia nguvu nyumba ya Yuda na kuiokoa nyumba ya Yusufu; kwani nitawarejesha na kuwahurumia. Watakuwa kama nilikuwa sijawaondoa, kwani mimi ni Yahwe Mungu wao, nami nitawaitikia.
7 Waefraimu watakuwa kama mashujaa, mioyo yao itafurahi kana kwamba ni kwa divai. Watoto wao wataona na kufurahi, mioyo yao itashangilia katika Bwana.
Ndipo Efraimu atakapokuwa kama shujaa, na mioyo yao itafurahi kama kwa mvinyo; wana wao wataona na kufurahi. Mioyo yao itanifurahia!
8 Nitawaashiria na kuwakusanya ndani. Hakika nitawakomboa, nao watakuwa wengi kama walivyokuwa mwanzoni.
Nitawanong'oneza na kuwakusanya, kwani nitawaokoa, nao watakuwa wakuu kama walivyokuwa mwanzo!
9 Ijapokuwa niliwatawanya miongoni mwa mataifa, hata hivyo wakiwa katika nchi za mbali watanikumbuka mimi. Wao na watoto wao watanusurika katika hatari nao watarudi.
Niliwapanda kati ya watu, lakini watanikumbuka katika nchi ya mbali, hivyo wao na wana wao wataishi na kurejea.
10 Nitawarudisha kutoka Misri na kuwakusanya toka Ashuru. Nitawaleta katika nchi ya Gileadi na Lebanoni, na hapo hapatakuwa na nafasi ya kuwatosha.
Kwa maana nitawarejesha kutoka nchi ya Misri na kuwakusanya kutoka Ashuru. Nitawaleta katika nchi ya Gileadi na Lebanoni mpaka kutakapokuwa hakuna nafasi tena kwa ajili yao.
11 Watapita katika bahari ya mateso; bahari iliyochafuka itatulizwa na vilindi vyote vya Mto Naili vitakauka. Kiburi cha Ashuru kitashushwa, nayo fimbo ya utawala ya Misri itatoweka.
Nitapita katika bahari ya mateso yao; nitayapiga mawimbi ya bahari hiyo na nitavikausha vilindi vyote vya Nile. Utukufu wa Ashuru utashushwa chini, na fimbo ya Misri itakwenda mbali kutoka kwa Wamisri.
12 Nitawaimarisha katika Bwana, na katika jina lake watatembea,” asema Bwana.
Nitawatia nguvu katika mimi mwenyewe, nao watatembea katika jina langu - asema Yahwe.