< Zekaria 1 >

1 Katika mwezi wa nane wa mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario, neno la Bwana lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia, mwana wa Ido, kusema:
Katika mwezi wa nane mwaka wa pili wa kutawala kwake Dario, neno la Yahwe lilimjia nabii Zekaria, mwana wa Berekia mwana wa Ido, kusema,
2 “Bwana aliwakasirikia sana baba zako wa zamani.
“Yawhe alikuwa na hasira sana juu ya baba zenu!
3 Kwa hiyo waambie watu: Hivi ndivyo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemavyo: ‘Nirudieni mimi,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, ‘nami nitawarudia ninyi,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
Wambie, 'Yahwe wa majeshi asema hivi: Nirudieni! - nami nitawarudia ninyi, asema Yahwe wa majeshi.
4 Msiwe kama baba zenu, ambao manabii waliotangulia waliwatangazia: Hivi ndivyo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemavyo: ‘Geukeni, mziache njia zenu mbaya na matendo yenu maovu.’ Lakini hawakunisikiliza wala kufuata maelekezo yangu, asema Bwana.
Msiwe kama baba zenu ambao hapo zamani manabii waliwambia, wakisema, “Yahwe wa majeshi asema hivi: Geukeni kutoka katika njia zenu za mbaya na matendo yenu mabaya!” Lakini hawakuweza kusikia wala kunijari - asema Yahwe.'
5 Wako wapi baba zako sasa? Nao manabii, je, wanaishi milele?
Wako wapi baba zenu? Na manabii, je wapo hapa daima?
6 Je, maneno yangu na amri zangu nilizowaagiza manabii watumishi wangu, hayakuwapata baba zenu?” “Kisha walitubu na kusema, ‘Bwana Mwenye Nguvu Zote ametutenda sawasawa na njia zetu na matendo yetu yalivyostahili, kama alivyokusudia kufanya.’”
Lakini maneno yangu na maagizo niliyowaamru watumishi wangu manabii, je hayakuwapata baba zenu? Hivyo walitubu na kusema, 'Kama vile Yahwe wa majeshi alivyokusudia kututenda kwa kadili zinavyostahili njia na matendo yetu, ndivyo alivyotutenda.”
7 Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario, neno la Bwana lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia mwana wa Ido.
Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, ndiyo mwezi wa Shebati, mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Yahwe lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia mwana wa Ido, akasema,
8 Wakati wa usiku nilipata maono, mbele yangu alikuwepo mtu akiendesha farasi mwekundu! Alikuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi kwenye bonde. Nyuma yake walikuwepo farasi wekundu, wa kikahawia na weupe.
“niliona wakati wa usiku, na tazama! mtu alikuwa amepanda farasi mwekundu, naye alikuwa kati ya miti ya mihadasi iliyoko bondeni; na nyuma yake kulikuwa na farasi mwekundu, farasi wa kijivu, na farasi mweupe.”
9 Nikauliza, “Hivi ni vitu gani bwana wangu?” Malaika aliyekuwa akizungumza na mimi akanijibu, “Nitakuonyesha kuwa ni nini.”
Nikauliza, “Bwana, hivi ni vitu gani?” Malaika aliyesema nami akaniambia, “Nitakueleza vitu hivi ni nini.”
10 Kisha yule mtu aliyesimama katikati ya miti ya mihadasi akaeleza, “Ni wale ambao Bwana amewatuma waende duniani kote.”
Kisha mtu aliyesimama kati ya miti ya mihadasi akajibu na kusema, “Hawa ndiyo Yahwe aliowatuma kuzunguka katika dunia yote.”
11 Nao wakatoa taarifa kwa yule malaika wa Bwana, aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumepita duniani kote na kukuta ulimwengu wote umepumzika kwa amani.”
Wakamjibu malaika wa Yahwe aliyekuwa amesimama kati ya miti ya mihadasi na kumwambia, “Tumekuwa tukizunguka duniani pote; tazama, dunia yote imekaa na kutulia.”
12 Kisha malaika wa Bwana akasema, “Bwana Mwenye Nguvu Zote, utazuia mpaka lini rehema kutoka Yerusalemu na miji ya Yuda, ambayo umeikasirikia kwa miaka hii sabini?”
Ndipo malaika wa Yahwe alipojibu na kusema, “Yahwe wa majeshi, hata lini usiuhurumie Yerusalemu na miji ya Yuda ambayo imeteswa na kudhurumiwa miaka hii sabini?”
13 Kwa hiyo Bwana akazungumza maneno ya upole na ya kufariji kwa malaika aliyezungumza nami.
Yahwe akamjibu malaika aliyekuwa amesema nami, kwa maneno mazuri, maneno ya faraja.
14 Kisha malaika yule aliyekuwa akizungumza nami akasema, “Tangaza neno hili: Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: ‘Nina wivu sana kwa ajili ya Yerusalemu na Sayuni,
Hivyo malaika aliyekuwa anaongea nami akaniambia, “Ita kwa sauti na useme 'Yahwe wa majeshi asema: Nina wivu kwa ajili ya Yerusalemu yaani Sayuni kwa uchungu mkubwa!
15 lakini nimeyakasirikia sana mataifa yanayojisikia kuwa yako salama. Nilikuwa nimewakasirikia Israeli kidogo tu, lakini mataifa hayo yaliwazidishia maafa.’
Nami nina hasira juu ya mataifa yaliyo na utulivu. Kwa maana nilikasirika kidogo tu, lakini wao wakasababisha madhara mabaya.
16 “Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Nitairudia Yerusalemu kwa rehema na huko nyumba yangu itajengwa tena. Nayo kamba ya kupimia itanyooshwa Yerusalemu,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
Kwa hiyo Yahwe wa majeshi asema hivi: Nimeirudia Yerusalema kwa huruma. Hivyo nyumba yangu itajengwa ndani yake - asema Yahwe wa majeshi. Kipimo kitanyoshwa juu ya Yerusalemu!
17 “Endelea kutangaza zaidi kwamba: Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Miji yangu itafurika tena ustawi na Bwana atamfariji tena Sayuni na kumchagua Yerusalemu.’”
Ita tena, ukisema, 'Yahwe wa majeshi asema hivi: Miji yangu kwa mara nyingine itajawa na uzuri, na Yahwe ataifariji tena Sayuni, na kuichagua Yerusalemu kwa mara nyingine tena.”
18 Kisha nikatazama juu, na pale mbele yangu nikaona pembe nne!
Kisha nikainua macho na kuona pembe nne!
19 Nikamuuliza yule malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Ni nini hivi?” Akanijibu, “Hizi ni zile pembe zilizowatawanya Yuda, Israeli na Yerusalemu.”
Nikaongea na malaika aliyesema nami, “Hivi ni vitu gani? Akanijibu “hizi ni pembe zilisosababisha kutawanyika kwa Yuda, Israeli, na Yerusalemu.”
20 Kisha Bwana akanionyesha mafundi wanne.
Kisha Yahwe akanionesha mafundi stadi wanne.
21 Nikauliza, “Hawa wanakuja kufanya nini?” Akanijibu, “Hizi ndizo pembe zilizowatawanya Yuda ili asiwepo atakayeweza kuinua kichwa chake, lakini mafundi wamekuja kuzitia hofu na kuzitupa chini hizi pembe za mataifa ambayo yaliinua pembe zao dhidi ya nchi ya Yuda na kuwatawanya watu wake.”
Nikasema, “Watu hawa wanakuja kufanya nini?” Akajibu na kusema, “Hizi ni pembe zililoitawanya Yuda na hakuna mtu angeweza kuinua kichwa chake. Lakini watu hawa wanakuja kuziondoa, kutupa chini pembe za mataifa yaliyoinua nguvu zao kinyume cha nchi ya Yuda na kuisambaza.”

< Zekaria 1 >