< Tito 1 >
1 Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo kwa ajili ya imani ya wateule wa Mungu na kuijua kweli iletayo utauwa:
Mimi Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo naandika. Mimi nimechaguliwa kuijenga imani ya wateule wa Mungu na kuwaongoza waufahamu ukweli wa dini yetu,
2 imani na ujuzi ulioko katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu, asiyesema uongo, aliahidi hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, (aiōnios )
ambayo msingi wake ni tumaini la kupata uzima wa milele. Mungu ambaye hasemi uongo, alituahidia uzima huo kabla ya mwanzo wa nyakati, (aiōnios )
3 naye kwa wakati wake aliouweka alilidhihirisha neno lake kwa njia ya mahubiri ambayo mimi nimewekewa amana kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu:
na wakati ufaao ulipowadia, akaudhihirisha katika ujumbe wake. Mimi nilikabidhiwa ujumbe huo nuutangaze kufuatana na amri ya Mungu, Mwokozi wetu.
4 Kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tunayoshiriki sote: Neema iwe kwako na amani itokayo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu.
Ninakuandikia wewe Tito, mwanangu wa kweli katika imani tunayoshiriki. Nakutakia neema na amani kutoka kwa Mungu Baba, na kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wetu.
5 Sababu ya mimi kukuacha huko Krete ni ili uweke utaratibu mambo yale yaliyosalia na kuwaweka wazee wa kanisa katika kila mji, kama nilivyokuagiza.
Nilikuacha Krete ili urekebishe yale mambo ambayo hayakuwa yamekamilika bado, na kuwateua wazee wa kanisa katika kila mji. Kumbuka maagizo yangu:
6 Mzee wa kanisa asiwe na lawama, awe mume wa mke mmoja, mtu ambaye watoto wake ni waaminio na wala hawashtakiwi kwa ufisadi.
mzee wa kanisa anapaswa kuwa mtu asiye na hatia; aliye na mke mmoja tu, na watoto wake wanapaswa kuwa waumini, wasiojulikana kuwa wakorofi au wakaidi.
7 Kwa kuwa mwangalizi, kama wakili wa Mungu, imempasa kuwa mtu asiye na lawama, asiwe mwenye majivuno au mwepesi wa hasira, wala mlevi, wala asiwe mtu mwenye tamaa ya mapato yasiyo ya halali.
Maana kwa vile kiongozi wa kanisa ni mkurugenzi wa kazi ya Mungu, anapaswa kuwa mtu asiye na hatia. Asiwe mwenye majivuno, mwepesi wa hasira, mlevi, mkorofi au mchoyo.
8 Bali awe mkarimu, anayependa mema, mwenye kiasi, mwenye haki, mwadilifu, mnyofu, mtakatifu na mwenye kuitawala nafsi yake.
Anapaswa kuwa mkarimu na anayependa mambo mema. Anapaswa kuwa mtu mtaratibu, mwadilifu, mtakatifu na mwenye nidhamu.
9 Inampasa alishike kwa uthabiti lile neno la imani kama lilivyofundishwa, kusudi aweze kuwaonya wengine kwa mafundisho manyofu na kuwakanusha wale wanaopingana nayo.
Ni lazima ashike kikamilifu ujumbe ule wa kuaminika kama unavyofundishwa. Ndivyo atakavyoweza kuwatia wengine moyo kwa mafundisho ya kweli na kuyafichua makosa ya wale wanaoyapinga mafundisho hayo.
10 Kwa maana wako wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, hasa wale wa kikundi cha tohara.
Maana, wako watu wengi, hasa wale walioongoka kutoka dini ya Kiyahudi, ambao ni wakaidi, wanaowapotosha wengine kwa upumbavu wao.
11 Hao ni lazima wanyamazishwe, kwa sababu wanaharibu watu wa nyumba nzima wakifundisha mambo yasiyowapasa kufundisha. Wanafanya hivyo kwa ajili ya kujipatia mapato ya udanganyifu.
Lazima kukomesha maneno yao, kwani wanavuruga jumuiya nzima kwa kufundisha mambo ambayo hawapaswi kufundisha; wanafanya hivyo kwa nia mbaya ya kupata faida ya fedha.
12 Hata mmojawapo wa manabii wao mwenyewe amesema, “Wakrete ni waongo siku zote, wanyama wabaya, walafi, wavivu.”
Hata mmoja wa manabii wao, ambaye naye pia ni Mkrete, alisema: “Wakrete, husema uongo daima; ni kama wanyama wabaya, walafi na wavivu!”
13 Ushuhuda huu ni kweli. Kwa hiyo, uwakemee kwa ukali wapate kuwa wazima katika imani,
Naye alitoboa ukweli kwa sababu hiyo, unapaswa kuwakaripia vikali, ili wawe na imani kamilifu.
14 ili wasiendelee kuangalia hadithi za Kiyahudi au maagizo ya wale watu wanaoikataa kweli.
Wasiendelee kushikilia hadithi tupu za Kiyahudi na maagizo ya kibinadamu yanayozuka kwa watu walioukataa ukweli.
15 Kwa wale walio safi, kila kitu ni safi kwao. Lakini kwa wale waliopotoka na wasioamini, hakuna chochote kilicho safi. Kwa kweli nia zao na dhamiri zao zimepotoka.
Kila kitu ni safi kwa watu walio safi; lakini hakuna chochote kilicho safi kwa wale waliochafuliwa na wasioamini, maana dhamiri na akili zao zimechafuliwa.
16 Wanadai kumjua Mungu, lakini kwa matendo yao wanamkana. Hao watu ni chukizo, wasiotii, wasiofaa kwa jambo lolote jema.
Watu kama hao hujidai kwamba wanamjua Mungu, lakini kwa matendo yao humkana. Ni watu wa kuchukiza mno na wakaidi, hawafai kwa jambo lolote jema.