< Tito 3 >
1 Wakumbushe watu kuwanyenyekea watawala na kuwatii wenye mamlaka, wawe tayari kutenda kila lililo jema.
Uwakumbushe kuwanyenyekea viongozi na mamlaka, kuwatii na kuwa tayari katika kila kazi njema.
2 Wasimnenee mtu yeyote mabaya, wasiwe wagomvi, bali wawe wapole, wakionyesha unyenyekevu kwa watu wote.
Wakumbushe kutokumtendea mtu yeyote ubaya, waepuke majibizano, wawape nafasi watu wengine katika kufanya maamuzi, na kuonesha unyenyekevu kwa watu wote.
3 Maana sisi wenyewe wakati fulani tulikuwa wajinga, wasiotii, tukiwa watumwa wa tamaa mbaya na anasa za kila aina. Tuliishi katika uovu na wivu, tukichukiwa na kuchukiana sisi kwa sisi.
Kwa kuwa sisi pia tulikuwa na mawazo potofu na wakaidi. Tulikuwa upotevuni na tulifanywa watumwa kwa tamaa nyingi na starehe. Tuliishi katika wivu na uovu. Tulichukiza na kuchukiana.
4 Lakini wema na upendo wa Mungu Mwokozi wetu ulipofunuliwa,
Lakini wakati huruma ya Mungu mwokozi wetu na upendo wake kwa wanadamu ulipoonekana,
5 alituokoa, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda, bali kwa sababu ya rehema zake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kufanywa wapya kwa njia ya Roho Mtakatifu,
haikuwa kwa matendo yetu ya haki tuliyofanya, bali alituokoa kwa neema yake. Alituokoa kwa kutuosha kwa kuzaliwa upya na katika kufanywa upya kwa Roho Mtakatifu.
6 ambaye Mungu alitumiminia kwa wingi kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu,
Mungu alimwaga Roho Mtakatifu kwa wingi juu yetu kupitia Yesu Kristo mwokozi wetu.
7 ili kwamba, tukiisha kuhesabiwa haki kwa neema yake, tupate kuwa warithi tukiwa na tumaini la uzima wa milele. (aiōnios )
Alifanya hivi ili kwamba, tukiwa tumehesabiwa haki kwa neema yake, tuwe washirika katika uhakika wa maisha ya milele. (aiōnios )
8 Hili ni neno la kuaminiwa. Nami nataka uyasisitize mambo haya, ili wale ambao wamemwamini Mungu wapate kuwa waangalifu kujitoa kwa ajili ya kutenda mema wakati wote. Mambo haya ni mazuri tena ya manufaa kwa kila mtu.
Huu ni ujumbe wa kuaminika. Ninawataka myanene kwa ujasiri mambo haya, ili kwamba wale wanaomwamini Mungu wawe na dhamira juu ya kazi nzuri ambayo aliiweka mbele yao. Mambo haya ni mazuri na yanafaida kwa ajili ya watu wote.
9 Lakini jiepushe na maswali ya kipuzi, mambo ya koo, mabishano na ugomvi kuhusu sheria, kwa sababu hayana faida, tena ni ubatili.
Lakini jiepusheni na mijadala ya kipumbavu, nasaba, mashindano, na migongano kuhusu sheria. Mambo hayo hayana maana wala faida.
10 Mtu anayesababisha mafarakano, mwonye mara ya kwanza, kisha mwonye mara ya pili. Baada ya hapo, usihusike naye tena.
Mkataeni yeyote anayesababisha migawanyiko kati yenu. Baada ya onyo moja ama mawili,
11 Kwa kuwa unajua kwamba mtu kama huyo amepotoka na tena ni mwenye dhambi. Yeye amejihukumu mwenyewe.
jueni kwamba mtu wa jinsi hiyo ameiacha njia iliyo sahihi na anatenda dhambi na kujihukumu mwenyewe.
12 Mara nitakapomtuma Artema au Tikiko kwako, jitahidi kuja unione huko Nikopoli, kwa sababu nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi.
Nitakapomtuma kwako Artemi au Tikiko, harakisha uje kwangu huku Nikopoli ambapo nimeamua kukaa kipindi cha baridi.
13 Fanya kila uwezalo uwasafirishe Zena yule mwanasheria na Apolo na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji katika safari yao.
Harakisha na umtume Zena mtaalamu katika sheria, na Apolo, pasipo kupungukiwa na kitu.
14 Watu wetu hawana budi kujifunza kutenda mema, ili waweze kuyakimu mahitaji ya kila siku, wasije wakaishi maisha yasiyokuwa na matunda.
Watu wetu lazima wajifunze kujishughulisha katika kazi nzuri ambazo zinagusa mahitaji muhimu ili kwamba wasije wakawa wasiozaa matunda.
15 Wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu wale wanaotupenda katika imani. Neema iwe nanyi nyote. Amen.
Wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu wale watupendao katika imani. Neema iwe nanyi nyote.