< Wimbo wa Sulemani 3 >
1 Usiku kucha kwenye kitanda changu nilimtafuta yule moyo wangu umpendaye; nilimtafuta, lakini sikumpata.
2 Sasa nitaondoka na kuzunguka mjini, katika barabara zake na viwanja; nitamtafuta yule moyo wangu umpendaye. Kwa hiyo nilimtafuta lakini sikumpata.
3 Walinzi walinikuta walipokuwa wakizunguka mji. Nikawauliza, “Je, mmemwona yule moyo wangu umpendaye?”
4 Kitambo kidogo tu baada ya kuwapita nilimpata yule moyo wangu umpendaye. Nilimshika na sikumwachia aende mpaka nilipomleta katika nyumba ya mama yangu, katika chumba cha yule aliyenichukua mimba.
5 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza kwa paa na kwa ayala wa shambani: Msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe.
6 Ni nani huyu anayekuja kutoka jangwani kama nguzo ya moshi, anayenukia manemane na uvumba iliyotengenezwa kwa vikolezo vyote vya mfanyabiashara?
7 Tazama! Ni gari la Solomoni lisindikizwalo na mashujaa sitini, walio wakuu sana wa Israeli,
8 wote wamevaa panga, wote wazoefu katika vita, kila mmoja na upanga wake pajani, wamejiandaa kwa ajili ya hofu za usiku.
9 Mfalme Solomoni alijitengenezea gari; alilitengeneza kwa mbao kutoka Lebanoni.
10 Nguzo zake alizitengeneza kwa fedha, kitako chake kwa dhahabu. Kiti chake kilipambwa kwa zambarau, gari lake likanakshiwa njumu kwa upendo na binti za Yerusalemu.
11 Tokeni nje, ninyi binti za Sayuni, mkamtazame Mfalme Solomoni akiwa amevaa taji, taji ambalo mama yake alimvika siku ya arusi yake, siku ambayo moyo wake ulishangilia.