< Ruth 1 >
1 Wakati Waamuzi walipotawala Israeli, kulikuwa na njaa katika nchi. Mtu mmoja kutoka nchi ya Bethlehemu ya Yuda, pamoja na mke wake na wanawe wawili, akaenda kuishi katika nchi ya Moabu.
2 Mtu huyu aliitwa Elimeleki, mkewe aliitwa Naomi, na hao wanawe wawili waliitwa Maloni na Kilioni. Walikuwa Waefrathi kutoka Bethlehemu ya Yuda. Wakaenda katika nchi ya Moabu, wakaishi huko.
3 Elimeleki mumewe Naomi akafa, hivyo Naomi akabaki na wanawe wawili.
4 Nao wakaoa wanawake Wamoabu, jina la mmoja aliitwa Orpa, na wa pili aliitwa Ruthu. Baada ya kama miaka kumi,
5 Maloni na Kilioni pia wakafa. Basi Naomi akabaki hana mume wala wanawe wawili.
6 Aliposikia akiwa huko Moabu kwamba Bwana amewasaidia watu wake kwa kuwapa chakula, Naomi na wakweze wakajiandaa kurudi nyumbani.
7 Yeye na wakweze wawili wakaondoka pale walipokuwa wakiishi na kushika njia kurudi nchi ya Yuda.
8 Ndipo Naomi akawaambia wale wakwe zake wawili, “Rudini, kila mmoja wenu nyumbani kwa mama yake. Bwana na awatendee fadhili kama mlivyowatendea hao waliofariki, na pia mimi.
9 Bwana na amjalie kila mmoja wenu maisha mema nyumbani kwa mume mwingine.” Kisha akawabusu, nao wakalia kwa sauti kubwa,
10 wakamwambia, “Tutarudi pamoja na wewe nyumbani kwa watu wako.”
11 Lakini Naomi akasema, “Rudini nyumbani, binti zangu. Kwa nini mnifuate? Je, mimi nitaweza tena kuwa na wana wengine ambao wataweza kuwaoa ninyi?
12 Rudini nyumbani, binti zangu; mimi ni mzee kiasi kwamba siwezi kumpata mume mwingine. Hata kama ningefikiria kuwa bado kuna tumaini kwangu, hata kama ningekuwa na mume usiku huu na kuwazaa wana,
13 je, mngesubiri mpaka wakue? Mngebakia bila kuolewa mkiwasubiri? La, hasha, binti zangu. Nimepata uchungu kuliko ninyi, kwa sababu mkono wa Bwana umekuwa kinyume nami!”
14 Kisha wakalia tena kwa sauti. Orpa akambusu mama mkwe wake, akaenda zake, lakini Ruthu akaambatana naye.
15 Naomi akamwambia, “Tazama, mwenzako anarejea kwa watu wake na kwa miungu yake. Rudi pamoja naye.”
16 Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakokwenda nami nitakwenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu.
17 Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. Bwana na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.”
18 Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena.
19 Kwa hiyo hao wanawake wawili wakaondoka, wakafika Bethlehemu. Walipofika Bethlehemu, mji mzima ulitaharuki, wanawake wakashangaa, wakasema, “Huyu aweza kuwa ni Naomi?”
20 Akawaambia, “Msiniite tena Naomi, niiteni Mara, kwa sababu Mwenyezi amenitendea mambo machungu sana.
21 Mimi niliondoka hali nimejaa, lakini Bwana amenirudisha mtupu. Kwa nini kuniita Naomi? Bwana amenitendea mambo machungu; Mwenyezi ameniletea msiba.”
22 Kwa hiyo Naomi alirudi pamoja na Ruthu Mmoabu mkwe wake, nao wakafika Bethlehemu mwanzoni mwa kuvuna shayiri.