< Ruth 4 >
1 Boazi akakwea mpaka kwenye lango la mji, akaketi pale. Yule mtu wa jamaa aliyekuwa wa karibu wa kukomboa, ambaye Boazi alimtaja, akaja. Boazi akasema, “Njoo hapa, rafiki yangu. Karibu uketi.” Naye akakaribia, akaketi.
Ndipo Boazi akaenda kwenye lango la Bethelehemu na kukaa chini. Muda mfupi tu akaja ndugu wa karibu ambaye Boazi alimuongelea. Boazi akamwambia, “Rafiki yangu, njoo hapa na uketi. Kisha mtu huyo akaja na kuketi.
2 Boazi akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, “Ketini hapa.” Nao wakaketi.
Ndipo Boazi akakusanya viongozi kumi wa mji na kusema, “Katini hapa.” Hivyo wakaketi.
3 Kisha akamwambia yule jamaa wa karibu wa kukomboa, “Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi iliyokuwa mali ya ndugu yetu Elimeleki.
Boazi alimwambia yule jamaa wa karibu, “Naomi aliyerudi kutoka mji wa Moabu, anauza sehemu ya aridhi ambayo ilikuwa ni miliki ya kaka yetu Elimeleki.
4 Nami niliwaza nikujulishe wewe na kukuambia uinunue mbele ya hawa waliopo hapa, na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya fanya hivyo. Lakini kama hutaikomboa, uniambie, ili nijue. Kwa kuwa hakuna mtu mwingine mwenye haki ya kuikomboa ila wewe na baada yako ni mimi.” Naye akasema, “Nitaikomboa mimi.”
Nilifikiria kukujulisha na kukwambia, 'Inunue mbele ya hawa waliokaa hapa, na mbele ya viongozi wa watu wangu.' Ikiwa utapenda kuikomboa, ikomboe. Lakini ikiwa hauhitaji kuikomboa, uniambie, ili nijue, kwa kuwa hakuna mwingine wa kuikomboa isipokuwa wewe, na mimi ni mdogo wako.” Ndipo huyo mtu mwingine akasema, “Nitalikomboa.”
5 Ndipo Boazi akasema “Siku utakaponunua hiyo ardhi kutoka kwa Naomi na Ruthu, Mmoabu, itakubidi kumchukua pia huyo mjane, ili kudumisha jina la marehemu pamoja na mali yake.”
Kisha Boazi akasema, “Ile siku utakayonunua shamba kutoka mkononi mwa Naomi, yakupasa pia kumchukua Ruth Mmoabu, mjane wa mtoto wa Elimeleki, ili kuliinua jina la marehemu kama urithi wake.”
6 Aliposikia hili, yule jamaa wa karibu wa kukomboa akasema, “Basi mimi sitaweza kuikomboa, kwa sababu inaonekana nitauhatarisha urithi wangu. Wewe ikomboe mwenyewe. Mimi sitaweza.”
Ndipo yule jamaa wa karibu akasema, “Mimi siwezi kuikomboa ardhi kwa ajili yangu bila kuleta athari kwenye urithi wangu binafsi. Nakupa wewe haki ya kuikomboa kwa ajili yako mwenyewe, kwa kuwa mimi sitoweza.”
7 (Basi katika siku za kale huko Israeli, ili kukamilisha tendo la kukomboa na kukabidhiana mali, mmoja huvua kiatu chake na kumpatia mwingine. Hii ilikuwa ni njia ya kuhalalisha mabadilishano katika Israeli.)
Hii ilikuwa ni desturi ya zamani ya Israeli kuhusu ukombozi na kubadilishana mazuri. Kudhibitisha mambo haya yote, mtu huyu alivua kiatu chake na kumpatia jirani yake; hii ilikuwa ni namna ya kufanya makubaliano ya kisheria katika Israeli.
8 Basi yule jamaa wa karibu wa kukomboa akamwambia Boazi, “Wewe inunue mwenyewe.” Naye huyo jamaa akavua kiatu chake.
Kwa hiyo huyu jamaa wa karibu akamwambia Boazi, “Inunue mwenyewe.” Kisha akavua kiatu chake.
9 Kisha Boazi akawatangazia wazee na watu wote waliokuwepo, “Leo ninyi ni mashahidi kwamba mimi nimenunua kutoka kwa Naomi yote yaliyokuwa mali ya Elimeleki, Kilioni na Maloni.
Ndipo Boazi akawaambia viongozi na watu wote, “Ninyi ni mashaidi kuwa nimenunua kila kilichokuwa cha Elimeleki na kila kilichokuwa na Kileoni na Mahilon kutoka kwenye mikono ya Naomi.
10 Nimemchukua pia Ruthu, Mmoabu, mjane wa Maloni, awe mke wangu, ili kuendeleza jina la marehemu pamoja na mali zake, ili jina lake marehemu lisitoweke miongoni mwa jamaa yake, wala katika kumbukumbu za mji wake. Leo hivi ninyi ni mashahidi!”
Zaidi ya hayo kumhusu Ruth Mmoabu, mke wa Mahlon: nimempa kibali cha kuwa mke wangu, ili kuendeleza jina na urithi wa marehumu, ili kwamba jina lake lisipotee kati ya ndugu zake na lango la watu wake. Ninyi ni mashahidi leo.”
11 Kisha wazee pamoja na watu wote waliokuwa langoni wakasema, “Sisi ni mashahidi. Bwana na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wanawake wawili ambao pamoja waliijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrathi na uwe mashuhuri katika Bethlehemu.
Watu wote na viongozi waliokuwa katika lango, walisema, “Tu mashahidi. Yahweh amfanye mwanamke huyu ambaye amekuja nyumbani kwako kama Raheli na Leya, ambao wawili hawa wameijenga nyumba ya Israeli. Na ubarikiwe katika Efrata na kuwa mashuhuri katika Bethelehem.
12 Kupitia kwa watoto ambao Bwana atakupa kutokana na huyu mwanamwali, jamaa yako na ifanane na ya Peresi, ambaye Tamari alimzalia Yuda.”
Na nyumba yako kama nyumba ya Peres, ambaye Tamari alimzalia yuda, kupitia uzao ambao Yahweh atakupatia pamoja na msichana huyu.”
13 Basi Boazi akamwoa Ruthu, naye akawa mke wake. Alipoingia kwake, Bwana akamjalia Ruthu, naye akapata mimba, akamzaa mtoto wa kiume.
Hivyo Boazi alimchukua Ruth, na akawa mke wake. Boazi alilala naye, na Yahweh alimruhusu kupata mimba, na alizaa mtoto wa kiume.
14 Wanawake wakamwambia Naomi: “Ahimidiwe Bwana, asiyekuacha bila kuwa na jamaa wa karibu wa kukomboa. Na awe mashuhuri katika Israeli yote!
Wanamke huyu akamwambia Naomi, “Yahweh abarikiwe, ambaye hajakuacha bila ndugu wa karibu, yaani mtoto huyu. Jina lake na liwe maarufu katika Israeli.
15 Atakurejeshea uhai wako na kukuangalia katika siku za uzee wako. Kwa maana mkweo ambaye anakupenda, na ambaye kwako ni bora zaidi ya watoto wa kiume saba, ndiye alimzaa.”
Na awe kwako mrutubishaji wa maisha na mwenye ruzuku uzeeni mwako, kwa kuwa mtoto wako mkwe, ambaye anakupenda, ambaye ni bora kwako kuliko watoto wa kiume saba, amemzaa.
16 Basi Naomi akamchukua yule mtoto, akampakata na akawa mlezi wake.
Kisha naomi akamchukua mtoto, akamlaza kifuani pake, na kumhudumia.
17 Wanawake waliokuwa jirani zake wakasema, “Naomi ana mtoto wa kiume.” Wakamwita jina lake Obedi. Yeye ndiye baba yake Yese, aliye baba yake Daudi.
Na majirani wa yule mwanamke, wakampa jina, wakisema, “Mtoto amezaliwa kwa Naomi.” Wakawita Obedi. Ambaye alikuja kuwa baba yake na Jese, ambaye alikuja kuwa baba yake na Daudi.
18 Hivi ndivyo vizazi vya Peresi: Peresi alimzaa Hesroni,
Hiki kilikuwa ni kizazi cha Peresi: Peres alimzaa Hezroni,
19 Hesroni akamzaa Ramu, Ramu akamzaa Aminadabu,
Hezroni akamzaa Ram, Ram akamzaa Aminadabu,
20 Aminadabu akamzaa Nashoni, Nashoni akamzaa Salmoni,
Aminadabu akamzaa Nashon, Nashon akamzaa Salmon,
21 Salmoni akamzaa Boazi, Boazi akamzaa Obedi,
Salmon akamzaa Boazi, Boazi akamzaa Obed,
22 Obedi akamzaa Yese, na Yese akamzaa Daudi.
Obedi akamzaa Jese, na Jese akamzaa Daudi.