< Ruth 4 >
1 Boazi akakwea mpaka kwenye lango la mji, akaketi pale. Yule mtu wa jamaa aliyekuwa wa karibu wa kukomboa, ambaye Boazi alimtaja, akaja. Boazi akasema, “Njoo hapa, rafiki yangu. Karibu uketi.” Naye akakaribia, akaketi.
2 Boazi akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, “Ketini hapa.” Nao wakaketi.
3 Kisha akamwambia yule jamaa wa karibu wa kukomboa, “Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi iliyokuwa mali ya ndugu yetu Elimeleki.
4 Nami niliwaza nikujulishe wewe na kukuambia uinunue mbele ya hawa waliopo hapa, na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya fanya hivyo. Lakini kama hutaikomboa, uniambie, ili nijue. Kwa kuwa hakuna mtu mwingine mwenye haki ya kuikomboa ila wewe na baada yako ni mimi.” Naye akasema, “Nitaikomboa mimi.”
5 Ndipo Boazi akasema “Siku utakaponunua hiyo ardhi kutoka kwa Naomi na Ruthu, Mmoabu, itakubidi kumchukua pia huyo mjane, ili kudumisha jina la marehemu pamoja na mali yake.”
6 Aliposikia hili, yule jamaa wa karibu wa kukomboa akasema, “Basi mimi sitaweza kuikomboa, kwa sababu inaonekana nitauhatarisha urithi wangu. Wewe ikomboe mwenyewe. Mimi sitaweza.”
7 (Basi katika siku za kale huko Israeli, ili kukamilisha tendo la kukomboa na kukabidhiana mali, mmoja huvua kiatu chake na kumpatia mwingine. Hii ilikuwa ni njia ya kuhalalisha mabadilishano katika Israeli.)
8 Basi yule jamaa wa karibu wa kukomboa akamwambia Boazi, “Wewe inunue mwenyewe.” Naye huyo jamaa akavua kiatu chake.
9 Kisha Boazi akawatangazia wazee na watu wote waliokuwepo, “Leo ninyi ni mashahidi kwamba mimi nimenunua kutoka kwa Naomi yote yaliyokuwa mali ya Elimeleki, Kilioni na Maloni.
10 Nimemchukua pia Ruthu, Mmoabu, mjane wa Maloni, awe mke wangu, ili kuendeleza jina la marehemu pamoja na mali zake, ili jina lake marehemu lisitoweke miongoni mwa jamaa yake, wala katika kumbukumbu za mji wake. Leo hivi ninyi ni mashahidi!”
11 Kisha wazee pamoja na watu wote waliokuwa langoni wakasema, “Sisi ni mashahidi. Bwana na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wanawake wawili ambao pamoja waliijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrathi na uwe mashuhuri katika Bethlehemu.
12 Kupitia kwa watoto ambao Bwana atakupa kutokana na huyu mwanamwali, jamaa yako na ifanane na ya Peresi, ambaye Tamari alimzalia Yuda.”
13 Basi Boazi akamwoa Ruthu, naye akawa mke wake. Alipoingia kwake, Bwana akamjalia Ruthu, naye akapata mimba, akamzaa mtoto wa kiume.
14 Wanawake wakamwambia Naomi: “Ahimidiwe Bwana, asiyekuacha bila kuwa na jamaa wa karibu wa kukomboa. Na awe mashuhuri katika Israeli yote!
15 Atakurejeshea uhai wako na kukuangalia katika siku za uzee wako. Kwa maana mkweo ambaye anakupenda, na ambaye kwako ni bora zaidi ya watoto wa kiume saba, ndiye alimzaa.”
16 Basi Naomi akamchukua yule mtoto, akampakata na akawa mlezi wake.
17 Wanawake waliokuwa jirani zake wakasema, “Naomi ana mtoto wa kiume.” Wakamwita jina lake Obedi. Yeye ndiye baba yake Yese, aliye baba yake Daudi.
18 Hivi ndivyo vizazi vya Peresi: Peresi alimzaa Hesroni,
19 Hesroni akamzaa Ramu, Ramu akamzaa Aminadabu,
20 Aminadabu akamzaa Nashoni, Nashoni akamzaa Salmoni,
21 Salmoni akamzaa Boazi, Boazi akamzaa Obedi,
22 Obedi akamzaa Yese, na Yese akamzaa Daudi.