< Ruth 2 >

1 Basi Naomi alikuwa na jamaa wa upande wa mume wake, kutoka ukoo wa Elimeleki, mtu maarufu ambaye aliitwa Boazi.
Basi Elimeleki mme wa Naomi, alikuwa na jamaa aitwaye Boazi, aliye kuwa tajiri, na mtu maarufu.
2 Ruthu, Mmoabu, akamwambia Naomi, “Nitakwenda mashambani nikaokote mabaki ya nafaka nyuma ya yule nitakayepata kibali machoni pake.” Naomi akamwambia, “Nenda, binti yangu.”
Ruth, Mmoabu, alimwambia Naomi, “Ngoja niende nikakusanye mabaki ya chakula katika shamba. Nitamfuata yeyote ambaye nitapata kibali machoni pake.” Hivyo naomi akamwambia, “Nenda, mwanangu.”
3 Basi akaenda, akaokota mabaki ya nafaka mashambani nyuma ya wavunaji. Ikatokea kwamba alijikuta anafanya kazi kwenye shamba lililokuwa mali ya Boazi, ambaye alitoka kwenye ukoo wa Elimeleki.
Ruth alienda kuvuna kwenye shamba akiwafuata kwa nyuma wavunaji. Na kumbe ile sehemu ya shamba ilikuwa ni mali ya Boazi, aliyekuwa na mahusiano na Elimeleki.
4 Papo hapo Boazi akarudi kutoka Bethlehemu, akawasalimu wavunaji, akasema, “Bwana awe nanyi!” Nao wakamjibu, “Bwana akubariki.”
Tazama, Boazi alikuja kutoka bethelehemu na kuwaambia wavunaji, “Yahweh awe nanyi.” Wakamjibu, “Yahweh akubariki.”
5 Boazi akamuuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, yule mwanamwali ni wa nani?”
Ndipo Boazi akamwambia mtumishi wake aliyekuwa akiwasimamia wavunaji, “Vipi bwana huyu msichana ni wa nani?”
6 Msimamizi akamjibu, “Ni yule Mmoabu aliyerudi kutoka nchi ya Moabu pamoja na Naomi.
Mtumishi msimamizi wa wavunaji alijibu na kusema, “Ni msichana Mmoabu aliyerudi na Naomi kutoka nchi ya Moabu.
7 Yeye aliomba, ‘Tafadhali niruhusu niokote na kukusanya miongoni mwa miganda nyuma ya wavunaji.’ Naye ameshinda shambani tangu asubuhi pasipo kupumzika, isipokuwa kwa muda mfupi kivulini.”
Aliniambia, 'Tafadhali niruhusu kuvuna na kukusanya mabaki ya wavunaji.' Hivyo alikuja na ameendelea kuvuna toka asubuhi mpaka sasa, isipokuwa amepumzika kidogo katika nyumba.”
8 Kisha Boazi akamwambia Ruthu, “Binti yangu, nisikilize. Usiende kuokota mabaki ya mavuno katika shamba lingine, na usiondoke hapa. Kaa hapa na hawa watumishi wangu wa kike.
Kisha Boazi akamwambia Ruth, “Unanisikiliza, mwanangu? Usiende kuvuna kwenye shamba lingine; usiondoke shambani kwangu. Badala yake, baki hapa na wasichana wangu wa kazi.
9 Angalia shamba wanaume wanamovuna, ufuate nyuma yao. Nimewaamuru wanaume hawa wasikuguse. Wakati wowote ukiona kiu, nenda kwenye mitungi ukanywe maji waliyoyateka wanaume hawa.”
Yaelekeze tu macho yako kwenye shamba ambamo wanaume wanavuna na ufuatie nyuma ya wanawake wengine. Je, sikuwaelekeza wanaume wasikuguse? Na upatapo kiu, unaweza kwenda kunywa maji kwenye mtungi ambao wanaume wamejaza.”
10 Kwa ajili ya hili, akasujudu mpaka nchi, akamwambia, “Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanijali mimi mgeni?”
Ndipo akapiga magoti mbele ya Boazi, na kugusisha kichwa chake chini. Akamwambia, “Kwa nini nimepata kibali machoni pako, hata unijali mimi mgeni?”
11 Boazi akamjibu, “Nimeambiwa yote uliyomtendea mama mkwe wako tangu mume wako alipofariki, na jinsi ulivyomwacha baba yako na mama yako na nchi yako ulimozaliwa, ukaja kuishi na watu ambao hukuwafahamu awali.
Boazi akajibu na kumwabia, “Nimekwisha ambiwa, yote uliyo yafanya tangu mme wako afariki. Umewaacha baba yako, mama, na nchi uliyozaliwa kumfuata mama mkwe wako na kuja kwa watu usiowajua.
12 Bwana na akulipe kwa yale uliyoyatenda. Ubarikiwe kwa wingi na Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye umekimbilia mabawani mwake.”
Yahweh akulipe kwa matendo yako. Yahweh akulipe kwa wingi, Mungu wa Israeli, ambaye chini ya mbawa zake umepata kimbilio.”
13 Kisha Ruthu akasema, “Naomba niendelee kupata kibali machoni pako, bwana wangu. Kwa maana umenifariji na umezungumza kwa ukarimu na mjakazi wako, hata ingawa mimi si bora kama mmoja wa watumishi wako wa kike.”
Ruth akasema, “Nipate kibali machoni pako, bwana wangu, kwa kuwa umenifariji, na umeongea wema kwangu, ingawa mimi sio mmoja wa watumishi wako wa kike.”
14 Wakati wa chakula, Boazi akamwambia Ruthu, “Karibia hapa. Kula mkate na uchovye ndani ya siki.” Alipoketi pamoja na wavunaji, akampa nafaka zilizookwa. Akala kiasi alichotaka na kusaza.
Wakati wa chakula Boazi alimwambia Ruth, “Njoo hapa, ule baadhi ya mikate, na uchovye kipande katika divai.” Alikaa kando ya wavunaji, na Boazi akampatia kiasi cha nafaka zilizo kaangwa. Ruth alikula mpaka alipotosheka na kusaza.
15 Alipoinuka ili kuokota mabaki ya nafaka, Boazi akawaagiza watu wake, “Hata kama atakusanya kati ya miganda, msimzuie.
Alipoinuka kwenda kuvuna, Boazi aliamuru vijana wake, akisema, “Mwacheni avune hata katika masuke, na msimwambie lolote baya.
16 Badala yake, toeni masuke katika miganda, mwachieni ayaokote, na msimkemee.”
Na pia muachie baadhi ya masuke katika vifurushi kwa ajili yake, na muaache ili ayavune. Msimkemee.”
17 Basi Ruthu akaokota masazo shambani hata jioni. Akatwanga ile shayiri aliyokusanya, ikajaa efa moja.
Kwa hiyo alivuna mpaka jioni. Kisha akatenganisha nafaka na majani ambayo amevuna, nazo nafaka zilikuwa kama efa moja ya shairi.
18 Akaibeba na kuelekea mjini, naye mama mkwe wake akaona jinsi alivyoweza kuokota nafaka nyingi. Pia Ruthu akachukua kile alichobakiza baada ya kula na kushiba, akampa.
Akazibeba na kwenda katika mji. Ndipo mama mkwe wake aliona kile alichokivuna. Ruth pia alimletea mama mkwe wake nafaka zilizo kaangwa alizobakiza kwenye chakula chake.
19 Basi mkwewe akamuuliza, “Je, umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Abarikiwe mtu yule aliyekujali.” Ndipo Ruthu akamwambia mama mkwe wake juu ya yule ambaye yeye alikuwa amefanyia kazi katika shamba lake. Akasema, “Yule mtu niliyefanyia kazi kwake leo, anaitwa Boazi.”
Mama mkwe wake akamwambia, “Umevunia wapi uliko vunia leo? Ulienda kufanyia wapi kazi? abarikiwe mtu aliye kusaidia.” Ndipo Ruth akamwambia mama mkwe wake kuhusu mtu aliye miliki shamba alilokuwa akifanya kazi. Alimwambia, “Jina la mtu ambaye alimiliki shamba nililokuwa nikifanya kazi ni Boazi.”
20 Naye Naomi akamwambia mkwewe, “Bwana ambariki! Hakuacha kuonyesha fadhili zake kwa walio hai na kwa waliokufa.” Pia akamwambia, “Huyo mtu ni mmoja wa jamaa yetu wa karibu anayestahili kutukomboa.”
Naomi akamwambia Ruth, “Abarikiwe na Yahweh, ambaye hakuondoa uaminifu wake kwa walio hai na wafu.” Naomi akamwambia, “Huyo mtu ni jamaa wa karibu nasi, ni jamaa yetu mkombozi.”
21 Kisha Ruthu, Mmoabu, akasema, “Hata aliniambia, ‘Kaa pamoja na watumishi wangu mpaka watakapomaliza kuvuna nafaka yangu yote.’”
Ruth Mmoabu akamwambia, “Ni kweli, aliniambia, 'Ukae karibu na vijana wangu wa kiume mpaka watakapo maliza mavuno yangu yote.'”
22 Kisha Naomi akamwambia Ruthu mkwewe, “Binti yangu, itakuwa vyema wewe ufuatane na wasichana wake, kwa sababu katika shamba la mtu mwingine wanaweza kukudhuru.”
Naomi akamwambia Ruth mke wa mtoto wake wa kiume, “Ni vizuri, mwanangu, kuwa uende pamoja na wasichana wake wa kazi, ili kwamba usije pata madhara yeyote katika shamba lolote.”
23 Kwa hivyo Ruthu akafuatana na watumishi wa kike wa Boazi, akaokota mpaka mwisho wa mavuno ya shayiri na ya ngano. Naye aliishi na mama mkwe wake.
Kwa hiyo alikaa karibu na wafanyakazi wa kike ili avune mpaka mwisho wa mavuno ya shayiri na mavuno ya ngano. Na alikuwa akiishi pamoja na mama mkwe wake.

< Ruth 2 >