< Warumi 9 >
1 Ninasema kweli katika Kristo, wala sisemi uongo, dhamiri yangu inanishuhudia katika Roho Mtakatifu.
Nasema ukweli katika Kristo. Sisemi uongo, na dhamira yangu hushuhudia pamoja nami katika Roho Mtakatifu,
2 Nina huzuni kuu na uchungu usiokoma moyoni mwangu.
kwamba kuna huzuni kubwa na maumivu yasiyo koma ndani ya moyo wangu.
3 Kwa maana ningetamani hata mimi nilaaniwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu hasa, wale walio wa kabila langu kwa jinsi ya mwili,
Kwamba ningetamani mimi mwenyewe kulaaniwa na kutengwa mbali na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, wale wa jamii yangu katika mwili.
4 yaani, watu wa Israeli, ambao ndio wenye kule kufanywa wana, ule utukufu wa Mungu, yale maagano, kule kupokea sheria, ibada ya kwenye Hekalu na zile ahadi.
Wao ni Waisraeli. Walio na hali ya kufanyika watoto, wa utukufu, wa maagano, na zawadi ya sheria, kumwabudu Mungu, na ahadi.
5 Wao ni wa uzao wa mababa wakuu wa kwanza, ambao kutoka kwao Kristo alikuja kwa jinsi ya mwili kama mwanadamu, yeye ambaye ni Mungu aliye juu ya vyote, mwenye kuhimidiwa milele! Amen. (aiōn )
Wao ni watangulizi ambako Kristo amekuja kwa heshima kuvaa mwili huu - ambaye yeye ni Mungu wa vyote. Naye asifiwe milele. Amina. (aiōn )
6 Si kwamba Neno la Mungu limeshindwa. Kwa maana si kila Mwisraeli ambaye ni wa uzao utokanao na Israeli ni Mwisraeli halisi.
Lakini si kwamba ahadi za Mungu zimeshindwa kutimia. Maana si kila mtu aliye Israeli ni Mwiisraeli halisi.
7 Wala hawakuwi wazao wa Abrahamu kwa sababu wao ni watoto wake, lakini: “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaki.”
Sivyo hata kwa uzao wa Abrahamu kuwa ni watoto wake halisi. Lakini, “ni kupitia Isaka uzao wako utaitwa.”
8 Hii ina maana kwamba, si watoto waliozaliwa kimwili walio watoto wa Mungu, bali ni watoto wa ahadi wanaohesabiwa kuwa uzao wa Abrahamu.
Hii ni kwamba, watoto wa mwili si watoto wa Mungu. Lakini watoto wa ahadi wanatazamwa kuwa kama uzao.
9 Kwa maana ahadi yenyewe ilisema, “Nitakurudia tena wakati kama huu, naye Sara atapata mtoto wa kiume.”
Maana hili ndilo neno la ahadi: “Katika majira haya nitakuja, na Sara atapewa mtoto.”
10 Wala si hivyo tu, bali pia watoto aliowazaa Rebeka walikuwa na baba huyo huyo mmoja, yaani, baba yetu Isaki.
Si hili tu, lakini baada ya Rebeka kupata mimba kwa mtu mmoja, Isaka baba yetu-
11 Lakini, hata kabla hao mapacha hawajazaliwa au kufanya jambo lolote jema au baya, ili kwamba kusudi la Mungu la kuchagua lipate kusimama,
kwamba watoto walikuwa bado hawajazaliwa na alikuwa hajafanya jambo lolote zuri au baya, ili kwamba kusudi la Mungu kulingana na uchaguzi lisimame, wala si kwa matendo, lakini ni kwa sababu ya yule aitae.
12 si kwa matendo, bali kwa yeye mwenye kuita, Rebeka aliambiwa, “Yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.”
Ilinenwa kwake, “Mkubwa atamtumikia mdogo.”
13 Kama vile ilivyoandikwa, “Nimempenda Yakobo, lakini nimemchukia Esau.”
Kama ilivyo kwisha andikwa: “Yakobo nilimpenda, lakini Esau nilimchukia.”
14 Tuseme nini basi? Je, Mungu ni dhalimu? La, hasha!
Basi tena tutasema nini? Je kuna udhalimu kwa Mungu? La hasha.
15 Kwa maana Mungu alimwambia Mose, “Nitamrehemu yeye nimrehemuye, na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”
Kwa kuwa anasema kwa Musa, “nitakuwa na rehema kwa yule nitakayemrehemu, na nitakuwa na huruma kwa yule nitakayemhurumia.”
16 Kwa hiyo haitegemei kutaka kwa mwanadamu au jitihada, bali hutegemea huruma ya Mungu.
Kwa hiyo basi, si kwa sababu ya yeye atakaye, wala si kwa sababu ya yeye ambaye hukimbia, lakini kwa sababu ya Mungu, ambaye huonesha rehema.
17 Kwa maana Maandiko yamwambia Farao, “Nilikuinua kwa kusudi hili hasa, ili nipate kuonyesha uweza wangu juu yako, na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani yote.”
Kwa kuwa maandiko husema kwa Farao, “Kwa kusudi hili maalumu nilikuinua, ili kwamba nioneshe nguvu zangu katika wewe, na ili kwamba jina langu litangazwe katika nchi yote.”
18 Kwa hiyo basi, Mungu humhurumia yeye atakaye kumhurumia na humfanya mgumu yeye atakaye kumfanya mgumu.
Hivyo basi, Mungu huwa na rehema kwa yeyote ampendaye, na kwa ambaye humpenda, humfanya kuwa mkaidi.
19 Basi mtaniambia, “Kama ni hivyo, kwa nini basi bado Mungu anatulaumu? Kwa maana ni nani awezaye kupinga mapenzi yake?”
Kisha utasema kwangu, “Kwa nini bado anaona kosa? Ni yupi ambaye alikwisha kustahimili matakwa yake?”
20 Lakini, ewe mwanadamu, u nani wewe ushindane na Mungu? “Je, kilichoumbwa chaweza kumwambia yeye aliyekiumba, ‘Kwa nini umeniumba hivi?’”
Kinyume chake, mwanadamu, wewe ni nani ujibue kinyume na Mungu? Kuna uwezekano wowote wa kilichofinyangwa kusema kwa mfinyanzi, “Kwanini ulinifanya hivi mimi?”
21 Je, mfinyanzi hana haki ya kufinyanga kutoka bonge moja vyombo vya udongo, vingine kwa matumizi ya heshima na vingine kwa matumizi ya kawaida?
Je mfinyazi huwa hana haki juu ya udongo kutengeneza chombo kwa matumizi maalumu kutokana na bonge lile lile, na chombo kingine kwa matumizi ya kila siku?
22 Iweje basi, kama Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake na kufanya uweza wake ujulikane, amevumilia kwa uvumilivu mwingi vile vyombo vya ghadhabu vilivyoandaliwa kwa uharibifu?
Vipi kama Mungu, ambaye ana utayari wa kuonesha gadhabu yake na kufanya nguvu yake kujulikana, alistahimili kwa uvumilivu wa kutosha vyombo vya gadhabu vilivyoandaliwa kwa kuangamiza?
23 Iweje basi, kama yeye alitenda hivi ili kufanya wingi wa utukufu wake ujulikane kwa vile vyombo vya rehema yake, alivyotangulia kuvitengeneza kwa ajili ya utukufu wake,
Vipi kama alifanya hivi ili kwamba aoneshe wingi wa utukufu wake juu ya vyombo vya rehema, ambavyo alikwisha kuviandaa kwa ajili ya utukufu?
24 yaani pamoja na sisi, ambao pia alituita, si kutoka kwa Wayahudi peke yao, bali pia kutoka kwa watu wa Mataifa?
Vipi kama alifanya hii pia kwetu, ambaye pia alituita, si tu kutoka kwa Wayahudi, lakini pia kutoka kwa watu wa Mataifa?
25 Kama vile Mungu asemavyo katika Hosea: “Nitawaita ‘watu wangu’ wale ambao si watu wangu; nami nitamwita ‘mpenzi wangu’ yeye ambaye si mpenzi wangu,”
Kama asemavyo pia katika Hosea: “Nitawaita watu wangu ambao hawakuwa watu wangu, na mpendwa wake ambaye hakupendwa.
26 tena, “Itakuwa hasa mahali pale walipoambiwa, ‘Ninyi si watu wangu,’ wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai.’”
Na itakuwa kwamba pale iliposemwa kwao, 'Ninyi si watu wangu,' pale wataitwa 'wana wa Mungu aliye hai.”'
27 Isaya anapiga kelele kuhusu Israeli: “Ingawa idadi ya wana wa Israeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki yao tu watakaookolewa.
Isaya analia kuhusiana na Israeli, “Kama hesabu ya wana wa Israeli ingekuwa kama mchanga wa bahari, itakuwa ni masalia ambao wataokolewa.
28 Kwa kuwa Bwana ataitekeleza hukumu yake duniani kwa haraka na kwa ukamilifu.”
Kwa kuwa Bwana atalichukua neno lake juu ya nchi, mapema na kwa utimilifu.
29 Ni kama vile alivyotabiri Isaya akisema: “Kama Bwana Mwenye Nguvu Zote asingelituachia uzao, tungelikuwa kama Sodoma, tungelifanana na Gomora.”
Na kama jinsi Isaya alivyosema awali, “Kama Bwana wa majeshi hakutuachia nyuma uzao kwa ajili yetu, tungekuwa kama Sodoma, na tungefanywa kama Gomora.
30 Kwa hiyo tuseme nini basi? Kwamba watu wa Mataifa ambao hawakutafuta haki, wamepata haki ile iliyo kwa njia ya imani.
Tutasema nini basi? kwamba watu wa Mataifa ambao walikuwa hawatafuti haki, walipata haki, haki kwa imani.
31 Lakini Israeli, ambao walijitahidi kupata haki kwa njia ya sheria, hawakuipata.
Lakini Israeli, ambaye alitafuta sheria ya haki, hakuifikia.
32 Kwa nini? Kwa sababu hawakuitafuta kwa njia ya imani bali kwa njia ya matendo. Wakajikwaa kwenye lile “jiwe la kukwaza.”
Kwanini si hivyo? Kwa sababu hawakuitafuta kwa imani, bali kwa matendo. Walijikwaa juu ya jiwe la kujikwaa,
33 Kama ilivyoandikwa: “Tazama naweka katika Sayuni jiwe la kukwaza watu na mwamba wa kuwaangusha. Yeyote atakayemwamini hataaibika kamwe.”
kama ilivyo kwisha andikwa, “Tazama, nimelaza jiwe la kujikwaa katika Sayuni na mwamba wa kukosa. Yeye ambaye huamini katika hili hataaibika.”