< Warumi 7 >
1 Ndugu zangu (sasa ninasema na wale wanaoijua sheria), je, hamjui ya kwamba sheria ina mamlaka tu juu ya mtu wakati akiwa hai?
Ndugu zangu, bila shaka mtaelewa yafuatayo, maana ninawazungumzia watu wanaojua Sheria. Sheria humtawala mtu wakati akiwa hai.
2 Kwa mfano, mwanamke aliyeolewa amefungwa kwa mumewe wakati akiwa hai, lakini yule mume akifa, yule mwanamke amefunguliwa kutoka sheria ya ndoa.
Mathalan: mwanamke aliyeolewa anafungwa na sheria muda wote mumewe anapokuw hai; lakini mumewe akifa, hiyo sheria haimtawali tena huyo mwanamke.
3 Hivyo basi, kama huyo mwanamke ataolewa na mwanaume mwingine wakati mumewe akiwa bado yuko hai, ataitwa mzinzi. Lakini kama mumewe akifa, mwanamke huyo hafungwi tena na sheria ya ndoa, naye akiolewa na mtu mwingine haitwi mzinzi.
Hivyo mwanamke huyo akiishi na mwanamume mwingine wakati mumewe yungali hai, ataitwa mzinzi; lakini mumewe akifa, mwanamke huyo yu huru kisheria, na akiolewa na mwanamume mwingine, yeye si mzinzi.
4 Vivyo hivyo, ndugu zangu, ninyi mmeifia sheria kwa njia ya mwili wa Kristo, ili mweze kuwa mali ya mwingine, yeye ambaye alifufuliwa kutoka kwa wafu, ili tupate kuzaa matunda kwa Mungu.
Hali kadhalika ninyi ndugu zangu: ninyi pia mmekufa kuhusu Sheria kwa kuwa ninyi ni sehemu ya mwili wa Kristo; sasa mmekuwa wake yeye aliyefufuliwa kutoka wafu ili tupate kuzaa matunda mema kwa ajili ya Mungu.
5 Kwa maana tulipokuwa tunatawaliwa na asili ya dhambi, tamaa za dhambi zilizochochewa na sheria zilikuwa zikitenda kazi katika miili yetu, hivyo tulizaa matunda ya mauti.
Maana, tulipokuwa tukiishi kimaumbile tu, tamaa mbaya zikichochewa na Sheria, zilifanya kazi katika miili yetu, na kuchuma pato la kifo.
6 Lakini sasa, kwa kufia kile kilichokuwa kimetufunga kwanza, tumewekwa huru kutokana na sheria ili tutumike katika njia mpya ya Roho, wala si katika njia ya zamani ya sheria iliyoandikwa.
Lakini sasa tumekuwa huru kutoka vifungo vya Sheria, kwa sababu tumekufa kuhusu lile jambo lililotufanya sisi watumwa. Sasa tunatumikia kufuatana na maisha mapya ya Roho, na si kufuatana na hali ile ya kale ya Sheria iliyoandikwa.
7 Tuseme nini basi? Kwamba sheria ni dhambi? La, hasha! Lakini, isingekuwa kwa sababu ya sheria, nisingalijua dhambi. Nisingalijua kutamani ni nini kama sheria haikusema, “Usitamani.”
Je, tuseme basi, kwamba Sheria ni dhambi? Hata kidogo! Lakini bila Sheria, mimi nisingalijua dhambi ni kitu gani. Maana, nisingalijua ni nini hasa kutamani mabaya, kama Sheria isingalikuwa imesema: “Usitamani.”
8 Lakini dhambi kwa kupata nafasi katika amri, hii ikazaa ndani yangu kila aina ya tamaa. Kwa maana pasipo sheria, dhambi imekufa.
Kwa kuitumia hiyo amri, dhambi ilipata fursa ya kuamsha kila aina ya tamaa mbaya ndani yangu. Maana, bila Sheria dhambi ni kitu kilichokufa.
9 Wakati fulani nilikuwa hai pasipo sheria, lakini amri ilipokuja, dhambi ikawa hai, nami nikafa.
Wakati mmoja mimi nilikuwa hai mbali na Sheria; lakini amri ilipokuja, dhambi ilifufuka,
10 Nikaona kwamba ile amri iliyokusudiwa kuleta uzima, ilileta mauti.
nami nikafa. Hiyo amri ambayo shabaha yake ilikuwa kuleta uhai, kwangu imeleta kifo.
11 Kwa maana dhambi kwa kupata nafasi katika amri, ilinidanganya, na kupitia katika hiyo amri, ikaniua.
Maana, dhambi ilichukua fursa iliyopatiwa na amri hiyo, ikanidanganya na kuniua.
12 Hivyo basi, sheria yenyewe ni takatifu, na amri ni takatifu na ya haki, tena ni njema.
Basi, Sheria yenyewe ni takatifu, na amri yenyewe ni takatifu, ni ya haki na nzuri.
13 Je, kile kilicho chema basi kilikuwa mauti kwangu? La, hasha! Lakini ili dhambi itambuliwe kuwa ni dhambi, ilileta mauti ndani yangu kupitia kile kilichokuwa chema, ili kwa njia ya amri dhambi izidi kuwa mbaya kupita kiasi.
Je, hii inamaanisha kwamba kile kilicho kizuri kimesababisha kifo changu? Hata kidogo! Iliyo ni kwamba, dhambi, ili ionekane dhahiri kuwa ni dhambi, imekitumia kile kilicho kizuri na kusababisha kifo changu. Hivyo dhambi, kwa njia ya ile amri, ilijionyesha kikamilifu jinsi ilivyo mbaya mno.
14 Kwa maana tunajua kwamba sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kimwili nikiwa nimeuzwa kwenye utumwa wa dhambi.
Tunajua kwamba Sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kidunia, mimi nimeuzwa kuwa mtumwa wa dhambi.
15 Sielewi nitendalo, kwa maana lile ninalotaka kulitenda, silitendi, lakini ninatenda lile ninalolichukia.
Sielewi nifanyacho, maana kile ninachotaka sikifanyi, bali kile ninachochukia ndicho nikifanyacho.
16 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, ni kwamba ninakubali kuwa sheria ni njema.
Ikiwa basi, ninatenda kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba nakubali kuwa ile Sheria ni nzuri.
17 Lakini, kwa kweli si mimi tena nitendaye lile nisilotaka bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.
Basi, si mimi hasa ninayefanya kitu hicho, bali ile dhambi iliyo ndani yangu.
18 Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote likaalo ndani yangu, yaani, katika asili yangu ya dhambi. Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda.
Najua kwamba hamna jema lolote ndani yangu mimi, kadiri ya ubinadamu wangu. Kwa maana, ingawa nataka kufanya jambo jema, siwezi kulitekeleza.
19 Sitendi lile jema nitakalo kutenda, bali lile baya nisilolitaka, ndilo nitendalo.
Yaani, badala ya kufanya lile jambo jema ninalotaka, nafanya lile baya nisilotaka.
20 Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.
Basi, kama ninafanya kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba si mimi ninayefanya hayo, bali ni ile dhambi iliyo ndani yangu.
21 Hivyo naiona sheria ikitenda kazi. Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo.
Basi, nimegundua kanuni hii: ninataka kufanya jema, lakini najikuta kwamba lile lililo baya ndilo ninalochagua.
22 Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia sheria ya Mungu.
Ndani kabisa katika moyo wangu naifurahia sheria ya Mungu.
23 Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu.
Lakini naona kwamba kuna sheria nyingine inayofanya kazi mwilini mwangu, sheria ambayo inapingana na ile inayokubaliwa na akili yangu. Hiyo inanifanya niwe mtumwa wa sheria ya dhambi ifanyayo kazi mwilini mwangu.
24 Ole wangu mimi maskini! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?
Maskini miye! Nani atakayeniokoa kutoka katika mwili huu unaonipeleka kifoni?
25 Ashukuriwe Mungu kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo basi, mimi mwenyewe kwa akili zangu ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika asili ya dhambi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.
Shukrani kwa Mungu afanyaye hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo! Hii basi, ndiyo hali yangu: mimi binafsi, kwa akili yangu, ninaitumikia sheria ya dhambi.