< Warumi 6 >
1 Tuseme nini basi? Je, tuendelee kutenda dhambi ili neema ipate kuongezeka?
Tuseme nini basi? Je, twendelee kubaki katika dhambi ili neema ya Mungu iongezeke?
2 La hasha! Sisi tulioifia dhambi, tutawezaje kuendelea kuishi tena katika dhambi?
Hata kidogo! Kuhusu dhambi sisi tumekufa—tutaendeleaje kuishi tena katika dhambi?
3 Au hamjui ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?
Maana, mnajua kwamba sisi tuliobatizwa tukaungana na Kristo Yesu, tulibatizwa na kuungana na kifo chake.
4 Kwa hiyo tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa utukufu wa Baba, vivyo hivyo sisi nasi pia tupate kuenenda katika upya wa uzima.
Tulipobatizwa tuliungana na kifo chake, tukazikwa pamoja naye, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka wafu kwa kitendo kitukufu cha Baba, sisi pia tuweze kuishi maisha mapya.
5 Kwa maana ikiwa tumeungana naye katika mauti yake, bila shaka tutaungana naye katika ufufuo wake.
Maana, kama sisi tumeungana naye katika kufa kama yeye, vivyo hivyo tutaungana naye kwa kufufuliwa kutoka wafu kama yeye.
6 Kwa maana twajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja naye ili ule mwili wa dhambi upate kuangamizwa, nasi tusiendelee kuwa tena watumwa wa dhambi.
Tunajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja na Kristo, ili hali ya dhambi iharibiwe, tusiwe tena watumwa wa dhambi.
7 Kwa maana mtu yeyote aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.
Kwa maana, mtu aliyekufa, amenasuliwa kutoka katika nguvu ya dhambi.
8 Basi ikiwa tulikufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba pia tutaishi pamoja naye.
Basi, ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba tutaishi pia pamoja naye.
9 Kwa maana tunajua kwamba Kristo, kwa sababu alifufuliwa kutoka kwa wafu, hawezi kufa tena; mauti haina tena mamlaka juu yake.
Maana, tunajua kwamba Kristo amekwisha fufuliwa kutoka wafu na hafi tena; kifo hakimtawali tena.
10 Kifo alichokufa, aliifia dhambi mara moja tu, lakini uzima alio nao anamwishia Mungu.
Hivyo, kwa kuwa alikufa—mara moja tu—dhambi haina nguvu tena juu yake; na sasa anaishi maisha yake katika umoja na Mungu.
11 Vivyo hivyo, jihesabuni wafu katika dhambi lakini mlio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.
Hali kadhalika nanyi lazima mjione kuwa mmekufa kuhusu dhambi, lakini kama mnaoishi katika umoja na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.
12 Kwa hiyo, msiruhusu dhambi itawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na kufa, ili kuwafanya mzitii tamaa mbaya.
Kwa hiyo, dhambi isiitawale tena miili yenu ambayo hufa, na hivyo kuzitii tamaa zake.
13 Wala msivitoe viungo vya miili yenu vitumike kama vyombo vya uovu vya kutenda dhambi, bali jitoeni kwa Mungu, kama watu waliotolewa kutoka mautini kuingia uzimani. Nanyi vitoeni viungo vya miili yenu kwake kama vyombo vya haki.
Wala msitoe hata sehemu moja ya miili yenu iwe chombo cha kutenda uovu na dhambi. Badala yake, jitoleeni ninyi wenyewe kwa Mungu kama watu waliofufuliwa kutoka wafu; toeni nafsi zenu zote kwa Mungu kwa ajili ya uadilifu.
14 Kwa maana dhambi haitakuwa na mamlaka juu yenu, kwa sababu hampo chini ya sheria, bali chini ya neema.
Maana, dhambi haitawatawala ninyi tena, kwani hamko chini ya Sheria, bali chini ya neema.
15 Ni nini basi? Je, tutende dhambi kwa kuwa hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? La, hasha!
Basi, tuseme nini? Je, tutende dhambi ati kwa sababu hatuko chini ya Sheria bali chini ya neema? Hata kidogo!
16 Je, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu yeyote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii, aidha watumwa wa dhambi, ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki?
Mnajua kwamba mkijitolea ninyi wenyewe kama watumwa na kumtii fulani, mnakuwa kweli watumwa wake mtu huyo—au watumwa wa dhambi, na matokeo yake ni kifo, au wa utii, na matokeo yake ni kukubaliwa kuwa waadilifu.
17 Lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa.
Ingawa mlikuwa watumwa wa dhambi zamani, sasa lakini—namshukuru Mungu—mmetii kwa moyo wote yale maazimio na mafundisho mliyopokea.
18 Nanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.
Mlikombolewa kutoka utumwa wa dhambi, mkawa watumwa wa uadilifu.
19 Ninasema kwa namna ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wenu wa hali ya asili. Kama vile mlivyokuwa mkivitoa viungo vya miili yenu kama watumwa wa mambo machafu na uovu uliokuwa ukiongezeka zaidi, hivyo sasa vitoeni viungo vyenu kama watumwa wa haki inayowaelekeza mpate kutakaswa.
(Hapa natumia lugha ya kawaida ya watu kwa sababu ya udhaifu wenu wenyewe.) Kama vile wakati fulani mlivyojitolea ninyi wenyewe kutumikia uchafu na uhalifu kwa ajili ya uovu, vivyo hivyo sasa jitoleeni nafsi zenu wenyewe kutumikia uadilifu kwa ajili ya utakatifu.
20 Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa hamtawaliwi na haki.
Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali na uadilifu.
21 Lakini mlipata faida gani kwa mambo hayo ambayo sasa mnayaonea aibu? Mwisho wa mambo hayo ni mauti.
Sasa, mlipata faida gani siku zile kutokana na mambo yale ambayo mnayaonea aibu sasa? Maana, matokeo ya mambo haya ni kifo!
22 Lakini sasa kwa kuwa mmewekwa huru mbali na dhambi na mmekuwa watumwa wa Mungu, faida mnayopata ni utakatifu, ambao mwisho wake ni uzima wa milele. (aiōnios )
Lakini sasa, mmekwisha kombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mmekuwa watumishi wa Mungu; faida mliyo nayo sasa ni utakatifu, na matokeo yake ni uzima wa milele. (aiōnios )
23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu. (aiōnios )
Kwa maana mshahara wa dhambi ni kifo; lakini zawadi anayotoa Mungu ni uzima wa milele katika kuungana na Kristo Yesu, Bwana wetu. (aiōnios )