< Warumi 4 >
1 Tuseme nini basi, kuhusu Abrahamu baba yetu kwa jinsi ya mwili: yeye alipataje kujua jambo hili?
Tuseme nini basi, juu ya Abrahamu baba yetu?
2 Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo, basi, anacho kitu cha kujivunia, lakini si mbele za Mungu.
Kama Abrahamu alikubaliwa kuwa mwadilifu kutokana na matendo yake, basi, anacho kitu cha kujivunia mbele ya Mungu.
3 Kwa maana Maandiko yasemaje? “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”
Kwa maana, Maandiko Matakatifu yasema: “Abrahamu alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.”
4 Basi mtu afanyapo kazi, mshahara wake hauhesabiwi kwake kuwa ni zawadi, bali ni haki yake anayostahili.
Mfanyakazi hulipwa mshahara; mshahara wake si zawadi bali ni haki yake.
5 Lakini kwa mtu ambaye hafanyi kazi na anamtumaini Mungu, yeye ambaye huwahesabia waovu haki, imani yake inahesabiwa kuwa haki.
Lakini mtu asiyetegemea matendo yake mwenyewe, bali anamwamini Mungu ambaye huwasamehe waovu, basi, Mungu huijali imani ya mtu huyo, na hivi humkubali kuwa mwadilifu.
6 Daudi pia alisema vivyo hivyo aliponena juu ya baraka za mtu ambaye Mungu humhesabia haki pasipo matendo:
Naye Daudi asema hivi juu ya furaha ya mtu ambaye Mungu amemkubali kuwa mwadilifu bila kuyajali matendo yake:
7 “Wamebarikiwa wale ambao wamesamehewa makosa yao, ambao dhambi zao zimefunikwa.
“Heri wale waliosamehewa makosa yao ambao makosa yao yamefutwa.
8 Heri mtu yule Bwana hamhesabii dhambi zake.”
Heri mtu yule ambaye Bwana hataziweka dhambi zake katika kumbukumbu.”
9 Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tunasema, “Imani ya Abrahamu ilihesabiwa kwake kuwa haki.”
Je, hiyo ni kwa wale waliotahiriwa tu, ama pia kwa wale wasiotahiriwa? Ni kwa wale wasiotahiriwa pia. Kwa maana tumekwisha sema: “Abrahamu aliamini, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.”
10 Je, ni lini basi ilipohesabiwa kwake kuwa haki? Je, ilikuwa kabla au baada ya kutahiriwa kwake? Haikuwa baada, ila kabla hajatahiriwa.
Je, Abrahamu alikubaliwa kabla ya kutahiriwa ama baada ya kutahiriwa? Kabla ya kutahiriwa, na si baada ya kutahiriwa.
11 Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote wale waaminio pasipo kutahiriwa na ambao wamehesabiwa haki.
Abrahamu alitahiriwa baadaye, na kutahiriwa huko kulikuwa alama iliyothibitisha kwamba Mungu alimkubali kuwa mwadilifu kwa sababu ya imani yake aliyokuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa hiyo, Abrahamu amekuwa baba wa wale wote ambao, ingawa hawakutahiriwa, wamemwamini Mungu, wakafanywa waadilifu.
12 Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo Baba yetu Abrahamu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa.
Vilevile yeye ni baba wa wale waliotahiriwa; lakini si kwa kuwa wametahiriwa, bali kwa sababu wanafuata njia ileile ya imani baba yetu Abrahamu aliyofuata kabla ya kutahiriwa.
13 Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Abrahamu au kwa wazao wake kwa njia ya sheria bali kwa njia ya haki ipatikanayo kwa imani.
Mungu alimwahidi Abrahamu na wazawa wake kwamba ulimwengu ungekuwa mali yao. Ahadi hiyo haikufanywa kwa sababu Abrahamu aliitii Sheria, bali kwa kuwa aliamini, akakubaliwa kuwa mwadilifu.
14 Kwa maana ikiwa wale waishio kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu,
Maana kama watakaopewa hayo aliyoahidi Mungu ni wale tu wanaoitii Sheria, basi, imani haina maana yoyote, nayo ahadi ya Mungu si kitu.
15 kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria hakuna makosa.
Sheria husababisha ghadhabu; lakini kama hakuna Sheria, haiwezekani kuivunja.
16 Kwa hiyo, ahadi huja kwa njia ya imani, ili iwe ni kwa neema, na itolewe kwa wazao wa Abrahamu, si kwa wale walio wa sheria peke yao, bali pia kwa wale walio wa imani ya Abrahamu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote.
Kwa sababu hiyo, jambo hili lategemea imani, hivyo kwamba ahadi hiyo yatokana na neema ya Mungu, na kwamba ni hakika kuwa ahadi hiyo ni kwa ajili ya wote: si kwa wale tu wanaoishika Sheria, bali pia kwa wale waishio kwa imani kama Abrahamu. Yeye ni baba yetu sisi sote.
17 Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anaye fufua waliokufa, na kuvitaja vile vitu ambavyo haviko kana kwamba vimekwisha kuwako.
Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.” Ahadi hiyo ni kweli mbele ya Mungu ambaye Abrahamu alimwamini—Mungu ambaye huwapa wafu uzima, na kwa amri yake, vitu ambavyo havikuwapo huwa.
18 Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Abrahamu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Uzao wako utakuwa mwingi mno.”
Abrahamu aliamini na kutumaini ingawa hali yenyewe ilikuwa bila matumaini, na hivyo amekuwa baba wa mataifa mengi kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Wazao wako watakuwa wengi kama nyota!”
19 Abrahamu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri juu ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri juu ya ufu wa tumbo la Sara.
Alikuwa mzee wa karibu miaka mia moja, lakini imani yake haikufifia ingawa alijua kwamba mwili wake ulikuwa kama umekufa, na pia mkewe, Sara, alikuwa tasa.
20 Lakini Abrahamu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu,
Abrahamu hakuionea mashaka ile ahadi ya Mungu; alipata nguvu kutokana na imani, akamtukuza Mungu.
21 akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi.
Alijua kwamba Mungu anaweza kuyatekeleza yale aliyoahidi.
22 Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.”
Ndiyo maana Mungu alimkubali kuwa mwadilifu.
23 Maneno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake,
Inaposemwa, “Alimkubali,” haisemwi kwa ajili yake mwenyewe tu.
24 bali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupa haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu.
Jambo hili linatuhusu sisi pia ambao tunamwamini Mungu aliyemfufua Yesu, Bwana wetu, kutoka wafu.
25 Alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuliwa kutoka mauti ili tuhesabiwe haki.
Yeye alitolewa auawe kwa ajili ya dhambi zetu, akafufuka ili tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na Mungu.