< Warumi 2 >

1 Kwa hiyo huna udhuru wowote, wewe utoaye hukumu kwa mwingine, kwa maana katika jambo lolote unalowahukumu wengine, unajihukumu wewe mwenyewe kwa sababu wewe unayehukumu unafanya mambo hayo hayo.
Basi, rafiki, kama unawahukumu wengine, huwezi kamwe kujitetea haidhuru wewe ni nani. Kwa maana, kwa kuwahukumu wengine, unajilaani wewe mwenyewe kwa vile nawe unayafanya mambo yaleyale unayohukumu.
2 Basi tunajua kwamba hukumu ya Mungu dhidi ya wale wafanyao mambo kama hayo ni ya kweli.
Tunajua kwamba hukumu ya Mungu kwa wale wanaofanya mambo kama hayo ni hukumu ya haki.
3 Hivyo wewe mwanadamu, utoapo hukumu juu yao na bado unafanya mambo yale yale, unadhani utaepuka hukumu ya Mungu?
Lakini wewe, rafiki, unayewahukumu wale wanaofanya mambo kama hayo bali wewe pia unayafanya, je unadhani utaiepa hukumu ya Mungu?
4 Au waudharau wingi wa wema, ustahimili na uvumilivu wake, bila kujua kuwa wema wa Mungu wakuelekeza kwenye toba?
Au labda unaudharau wema wake mkuu, uvumilivu wake na saburi yake, bila kutambua kwamba wema wake huo una shabaha ya kukuongoza upate kutubu?
5 Lakini kwa sababu ya ukaidi wenu na mioyo yenu isiyotaka kutubu, mnajiwekea akiba ya ghadhabu dhidi yenu wenyewe kwa siku ile ya ghadhabu ya Mungu, wakati hukumu yake ya haki itakapodhihirishwa.
Lakini unao ugumu na ukaidi wa moyo, na hivyo unajilundikia adhabu kwa Siku ile ambayo ghadhabu ya Mungu na hukumu zake za haki vitadhihirishwa.
6 Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake.
Siku hiyo Mungu atamlipa kila mmoja kufuatana na matendo yake.
7 Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele. (aiōnios g166)
Wale wanaozingatia kutenda mema, kutafuta utukufu na heshima ya Mungu na kutokufa, watapata uzima wa milele. (aiōnios g166)
8 Lakini kwa wale watafutao mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu.
Lakini wale wengine wenye ubinafsi, wenye kukataa mambo ya haki na kufuata uovu, wataangukiwa na ghadhabu na hasira ya Mungu.
9 Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu wa Mataifa pia,
Mateso na maumivu yatampata binadamu yeyote atendaye uovu. Yatawapata Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia.
10 bali utukufu, heshima na amani kwa ajili ya kila mmoja atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, kisha kwa mtu wa Mataifa.
Lakini Mungu atawapa utukufu, heshima na amani wale wanaotenda mema; Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia.
11 Kwa maana Mungu hana upendeleo.
Maana Mungu hambagui mtu yeyote.
12 Watu wote waliotenda dhambi pasipo sheria wataangamia pasipo sheria, nao wote wale waliotenda dhambi chini ya sheria watahukumiwa kwa sheria.
Wale wanaotenda dhambi bila kuijua Sheria ya Mose wataangamia ingawaje hawajui Sheria. Na wale wanaotenda dhambi wakiwa wanaijua Sheria watahukumiwa kisheria.
13 Kwa maana si wale wanaoisikia sheria ambao ni wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale wanaoitii sheria ndio watakaohesabiwa haki.
Mtu hafanywi kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kuisikia Sheria, bali kwa kuitii Sheria.
14 (Naam, wakati wa watu wa Mataifa, ambao hawana sheria, wanapofanya kwa asili mambo yatakiwayo na sheria, wao ni sheria kwa nafsi zao wenyewe, hata ingawa hawana sheria.
Mathalan: watu wa mataifa mengine hawana Sheria ya Mose; lakini kila wanapotimiza matakwa ya Sheria wakiongozwa na dhamiri zao, wao wenyewe wanakuwa kipimo cha Sheria ingawa hawaijui Sheria.
15 Wao wanaonyesha kwamba lile linalotakiwa na sheria limeandikwa kwenye mioyo yao, ambayo pia dhamiri zao zikiwashuhudia, nayo mawazo yao yenye kupingana yatawashtaki au kuwatetea.)
Mwenendo wao unaonyesha kwamba matakwa ya Sheria yameandikwa mioyoni mwao. Dhamiri zao zinashuhudia pia jambo hilo, maana fikira zao mara nyingine huwashtaki, na mara nyingine huwatetea.
16 Hili litatukia siku hiyo Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu kwa njia ya Yesu Kristo, kama isemavyo Injili yangu.
Hivyo, kufuatana na hii Habari Njema ninayohubiri, ndivyo itakavyokuwa wakati Mungu atakapohukumu mambo ya siri ya binadamu kwa njia ya Yesu Kristo.
17 Tazama, wewe ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea sheria na kujisifia uhusiano wako na Mungu,
Na wewe, je? Wewe mwenyewe unajiita Myahudi; unaitumainia Sheria na kujivunia kuwa wa Mungu;
18 kama unajua mapenzi ya Mungu na kukubali lililo bora kwa sababu umefundishwa na hiyo sheria,
kwa njia ya Sheria unajua matakwa ya Mungu na unaweza kuchagua jambo jema;
19 kama unatambua kuwa wewe ni kiongozi wa vipofu, na mwanga kwa wale walio gizani,
wewe unajiona kuwa kiongozi wa vipofu na mwanga kwa wale walio gizani;
20 mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa watoto wachanga, kwa kuwa una maarifa ya kweli katika hiyo sheria,
unajiona kuwa mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa wale wasiokomaa bado. Unayo katika Sheria picha kamili ya elimu na ukweli.
21 basi wewe, uwafundishaye wengine, mbona hujifunzi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, wewe mwenyewe waiba?
Basi, wewe unawafundisha wengine; kwa nini hujifundishi wewe mwenyewe? Unawahubiria wengine wasiibe, lakini kumbe wewe mwenyewe unaiba.
22 Wewe usemaye mtu asizini, wewe mwenyewe wazini? Wewe uchukiaye miungu ya sanamu, wafanya jambo la kumchukiza katika mahekalu?
Unasema: “Msizini,” na huku wewe unazini; unachukia sanamu za miungu hali wewe unajitajirisha kwa kuiba katika nyumba za miungu.
23 Wewe ujivuniaye sheria, wamwaibisha Mungu kwa kuvunja sheria?
Kwa kujigamba ati unayo Sheria ya Mungu, je huoni kwamba kwa kuivunja Sheria unamdharau Mungu?
24 Kama ilivyoandikwa, “Kwa ajili yenu ninyi, Jina la Mungu linatukanwa miongoni mwa watu wa Mataifa.”
Kama vile Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Watu wa mataifa mengine wamelikufuru jina la Mungu kwa sababu yenu ninyi Wayahudi!”
25 Kutahiriwa kuna thamani ikiwa unatii sheria, lakini kama unavunja sheria, kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa.
Kutahiriwa kwako kutakuwa na maana kama ukiitii Sheria. Lakini kama unaivunja Sheria, basi, ni afadhali ungalibaki bila kutahiriwa.
26 Hivyo, ikiwa wale wasiotahiriwa wanatimiza mambo ambayo sheria inataka, je, kutokutahiriwa kwao hakutahesabiwa kuwa sawa na kutahiriwa?
Kama mtu wa mataifa mengine ambaye hakutahiriwa akitimiza matakwa ya Sheria, hakika atafikiriwa kana kwamba ametahiriwa.
27 Ndipo wale ambao hawakutahiriwa kimwili lakini wanaitii sheria watawahukumu ninyi, ambao ingawa mmetahiriwa na kuijua sana sheria ya Mungu iliyoandikwa, lakini mwaivunja.
Watu wa mataifa mengine watakuhukumu wewe Myahudi kama ukiivunja Sheria, ingawaje unayo maandishi ya Sheria na umetahiriwa, hali wao wanaitii Sheria ingawa hawakutahiriwa.
28 Kwa maana mtu si Myahudi kwa vile alivyo kwa nje, wala tohara ya kweli si kitu cha nje au cha kimwili.
Ndiyo kusema, si kila anayeonekana kwa nje kuwa Myahudi ni Myahudi wa kweli, wala mtu hawi Myahudi wa kweli ati kwa kuwa ametahiriwa kimwili.
29 Lakini mtu ni Myahudi alivyo ndani, nayo tohara ya kweli ni jambo la moyoni, ni la Roho, wala si la sheria iliyoandikwa. Mtu wa namna hiyo hapokei sifa kutoka kwa wanadamu bali kwa Mungu.
Myahudi wa kweli ni yule aliye Myahudi kwa ndani, yaani yule ambaye ametahiriwa moyoni. Hili ni jambo la Roho, na si jambo la maandishi ya Sheria. Mtu wa namna hiyo anapata sifa, si kutoka kwa watu, bali kutoka kwa Mungu.

< Warumi 2 >