< Warumi 16 >

1 Napenda kumtambulisha kwenu dada yetu Foibe, mtumishi katika kanisa la Kenkrea.
Napenda kumjulisha kwenu dada yetu Foibe ambaye ni mtumishi katika kanisa la Kenkrea.
2 Naomba mpokeeni katika Bwana ipasavyo watakatifu na kumpa msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, kwa maana yeye amekuwa msaada kwa watu wengi, mimi nikiwa miongoni mwao.
Mpokeeni kwa ajili ya Bwana kama iwapasavyo watu wa Mungu. Mpeni msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, maana yeye amekuwa mwema sana kwa watu wengi na kwangu pia.
3 Wasalimuni Prisila na Akila, watumishi wenzangu katika Kristo Yesu.
Salamu zangu ziwafikie Priska na Akula, wafanyakazi wenzangu katika utumishi wa Kristo Yesu.
4 Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu; wala si mimi tu ninayewashukuru bali pia makanisa yote ya watu wa Mataifa.
Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu. Wanastahili shukrani; si tu kutoka kwangu, bali pia kutoka kwa makanisa yote ya watu wa mataifa mengine.
5 Lisalimuni pia kanisa linalokutana nyumbani mwao. Msalimuni rafiki yangu mpendwa Epaineto, aliyekuwa mtu wa kwanza kumwamini Kristo huko Asia.
Salamu zangu pia kwa kanisa linalokutana nyumbani kwao. Salamu zangu zimfikie rafiki yangu Epaineto ambaye ni kwa kwanza katika mkoa wa Asia kumwamini Kristo.
6 Msalimuni Maria, aliyefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu.
Nisalimieni Maria ambaye amefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu.
7 Wasalimuni Androniko na Yunia, jamaa zangu ambao wamekuwa gerezani pamoja nami. Wao ni maarufu miongoni mwa mitume, nao walikuwa katika Kristo kabla yangu.
Salamu zangu kwa Androniko na Yunia, wananchi wenzangu waliofungwa gerezani pamoja nami; wao wanajulikana sana kati ya mitume; tena walikuwa Wakristo kabla yangu mimi.
8 Msalimuni Ampliato, yeye nimpendaye katika Bwana.
Salamu zangu kwa Ampliato, rafiki yangu katika kuungana na Bwana.
9 Msalimuni Urbano, mtendakazi mwenzetu katika Kristo, pamoja na rafiki yangu mpendwa Stakisi.
Salamu zangu zimfikie Urbano, mfanyakazi mwenzangu katika utumishi wa Kristo; salamu zangu pia kwa rafiki yangu Staku.
10 Msalimuni Apele aliyejaribiwa na akaithibitisha imani yake katika Kristo. Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Aristobulo.
Nisalimieni Apele ambaye uaminifu wake kwa Kristo umethibitishwa. Salamu zangu kwa wote walio nyumbani mwa Aristobulo.
11 Msalimuni ndugu yangu Herodioni. Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Narkisi walio katika Bwana.
Salamu zangu kwa Herodiana, mwananchi mwenzangu; na kwa jamaa yote ya Narkisi iliyojiunga na Bwana.
12 Wasalimuni Trifaina na Trifosa, wale wanawake wanaofanya kazi kwa bidii katika Bwana. Msalimuni rafiki yangu mpendwa Persisi, mwanamke mwingine aliyefanya kazi kwa bidii katika Bwana.
Nisalimieni Trufena na Trufosa wanaofanya kazi katika utumishi wa Bwana, na rafiki yangu Persi ambaye amefanya mengi kwa ajili ya Bwana.
13 Msalimuni Rufo, mteule katika Bwana, pamoja na mama yake, ambaye amekuwa mama kwangu pia.
Nisalimieni Rufo, mtu hodari sana katika kazi ya Bwana, na mama yake ambaye ni mama yangu pia.
14 Wasalimuni Asinkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herma na ndugu wote walio pamoja nao.
Nisalimieni Asunkrito, Flegoni, Herme Patroba, Herma na ndugu wote walio pamoja nao.
15 Wasalimuni Filologo, Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa na watakatifu wote walio pamoja nao.
Nisalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, na Olumpa, pamoja na watu wote wa Mungu walio pamoja nao.
16 Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa busu takatifu. Makanisa yote ya Kristo yanawasalimu.
Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa ishara ya upendo. Salamu kwenu kutoka kwa makanisa yote ya Kristo.
17 Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza.
Ndugu zangu, nawasihi muwafichue wote wanaosababisha mafarakano na kuwafanya watu wengine waanguke, kinyume cha mafundisho mliyofundishwa. Jiepusheni na watu hao,
18 Kwa maana watu kama hao hawamtumikii Bwana Kristo, bali wanatumikia tamaa zao wenyewe. Kwa kutumia maneno laini na ya kubembeleza, hupotosha mioyo ya watu wajinga.
maana watu wa namna hiyo hawamtumikii Kristo Bwana wetu, bali wanayatumikia matumbo yao wenyewe. Kwa maneno yao matamu na hotuba za kubembeleza hupotosha mioyo ya watu wanyofu.
19 Kila mtu amesikia juu ya utii wenu, nami nimejawa na furaha tele kwa ajili yenu. Lakini nataka mwe na hekima katika mambo mema na bila hatia katika mambo maovu.
Kila mtu amesikia juu ya utii wenu na hivyo mmekuwa sababu ya furaha yangu. Nawatakeni muwe na hekima katika mambo mema, na bila hatia kuhusu mambo mabaya.
20 Mungu wa amani atamponda Shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya Bwana wetu Yesu iwe nanyi. Amen.
Naye Mungu aliye chanzo cha amani hatakawia kumponda Shetani chini ya miguu yenu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.
21 Timotheo, mtendakazi mwenzangu anawasalimu. Vivyo hivyo Lukio, Yasoni, na Sosipatro, ndugu zangu.
Timotheo, mfanyakazi mwenzangu, anawasalimu. Hali kadhalika Lukio, Yasoni, na Sosipatro, wananchi wenzangu, wanawasalimu.
22 Mimi, Tertio, niliye mwandishi wa waraka huu, nawasalimu katika Bwana.
Nami Tertio, ninayeandika barua hii nawasalimuni katika Bwana.
23 Gayo, ambaye ni mwenyeji wangu na wa kanisa lote, anawasalimu. Erasto, mweka hazina wa mji huu, pamoja na Kwarto ndugu yetu pia wanawasalimu. [
Gayo, mwenyeji wangu, pamoja na kanisa lote linalokutana kwake, anawasalimu. Erasto, mweka hazina wa mji huu, pamoja na Kwarto, wanawasalimu.
24 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi nyote. Amen.]
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amina.
25 Sasa atukuzwe yeye awezaye kuwafanya ninyi imara kwa Injili yangu na kuhubiriwa kwa Yesu Kristo, kutokana na kufunuliwa siri zilizofichika tangu zamani za kale. (aiōnios g166)
Basi, sasa na tumsifu Mungu! Yeye anaweza kuwaimarisheni katika ile Habari Njema niliyohubiri juu ya ujumbe wa Yesu Kristo, na katika ile siri iliyofunuliwa na ambayo ilikuwa imefichika kwa karne nyinyi zilizopita. (aiōnios g166)
26 Lakini sasa siri hiyo imefunuliwa na kujulikana kupitia maandiko ya kinabii kutokana na amri ya Mungu wa milele, ili mataifa yote yaweze kumwamini na kumtii (aiōnios g166)
Lakini, sasa ukweli huo umefunuliwa kwa njia ya maandiko ya manabii; na kwa amri ya Mungu wa milele umedhihirisha kwa mataifa yote ili wote waweze kuamini na kutii. (aiōnios g166)
27 Mungu aliye pekee, mwenye hekima, ambaye kwa njia ya Yesu Kristo utukufu ni wake milele na milele! Amen. (aiōn g165)
Kwake Mungu aliye peke yake mwenye hekima, uwe utukufu kwa njia ya Yesu Kristo, milele na milele! Amina. (aiōn g165)

< Warumi 16 >