< Warumi 15 >

1 Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe.
Sisi tulio imara katika imani tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Tusijipendelee sisi wenyewe tu.
2 Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani.
Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake kwa wema ili huyo apate kujijenga katika imani.
3 Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.”
Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: “Kashfa zote walizokutolea wewe zimenipata mimi.”
4 Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwamba kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini.
Maana yote yalioandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na Maandiko hayo Matakatifu tupate kuwa na matumaini.
5 Mungu atoaye saburi na faraja, awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu,
Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni ninyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu,
6 ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.
ili ninyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.
7 Karibishaneni ninyi kwa ninyi kama Kristo alivyowakaribisha ninyi ili kumletea Mungu utukufu.
Basi, karibishaneni kwa ajili ya utukufu wa Mungu kama naye Kristo alivyowakaribisheni.
8 Kwa maana nawaambia kwamba, Kristo amekuwa mtumishi kwa wale waliotahiriwa ili kuonyesha kweli ya Mungu na kuthibitisha zile ahadi walizopewa baba zetu wa zamani,
Maana, nawaambieni Kristo aliwatumikia Wayahudi apate kuonyesha uaminifu wa Mungu, na zile ahadi Mungu alizowapa babu zetu zipate kutimia;
9 pia ili watu wa Mataifa wamtukuze Mungu kwa rehema zake. Kama ilivyoandikwa: “Kwa hiyo nitakutukuza katikati ya watu wa Mataifa; nitaliimbia sifa jina lako.”
ili nao watu wa mataifa mengine wapate kumtukuza Mungu kwa sababu ya huruma yake. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Kwa sababu hiyo, nitakusifu miongoni mwa watu wa mataifa. Nitaziimba sifa za jina lako.”
10 Tena yasema, “Enyi watu wa Mataifa, furahini pamoja na watu wa Mungu.”
Tena Maandiko yasema: “Furahini, enyi watu wa mataifa; furahini pamoja na watu wake.”
11 Tena, “Msifuni Bwana, ninyi watu wa Mataifa wote, na kumwimbia sifa, enyi watu wote.”
Na tena: “Enyi mataifa yote, msifuni Bwana; enyi watu wote, msifuni.”
12 Tena Isaya anasema, “Shina la Yese litachipuka, yeye atakayeinuka ili kutawala juu ya mataifa. Watu wa Mataifa watamtumaini.”
Tena Isaya asema: “Atatokea mtu katika ukoo wa Yese, naye atawatawala watu wa mataifa; nao watamtumainia.”
13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
14 Ndugu zangu, mimi mwenyewe ninasadiki kwamba mmejaa wema na ufahamu wote, tena mnaweza kufundishana ninyi kwa ninyi.
Ndugu zangu, mimi binafsi nina hakika kwamba ninyi pia mmejaa wema, elimu yote, na mnaweza kushauriana ninyi kwa ninyi.
15 Nimewaandikia kwa ujasiri vipengele kadha wa kadha katika waraka huu kama kuwakumbusha tena kwa habari ya ile neema Mungu aliyonipa,
Lakini nimewaandikia hapa na pale katika barua hii bila woga, nipate kuwakumbusheni juu ya mambo fulani. Nimefanya hivyo kwa sababu ya neema aliyonijalia Mungu
16 ili kuwa mhudumu wa Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa nikiwa na huduma ya kikuhani ya kutangaza Injili ya Mungu, ili watu wa Mataifa wapate kuwa dhabihu inayokubaliwa na Mungu, iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.
ya kuwa mtumishi wa Yesu Kristo kwa watu wa mataifa. Ni jukumu langu la kikuhani kuihubiri Habari Njema ya Mungu ili watu wa mataifa mengine wapate kuwa dhabihu inayokubaliwa na Mungu, dhabihu iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.
17 Kwa hiyo ninajisifu katika Kristo Yesu, kwenye utumishi wangu kwa Mungu.
Kwa hiyo, nikiwa nimeungana na Kristo Yesu, naweza kujivunia huduma yangu kwa ajili ya Mungu.
18 Kwa maana sitathubutu kusema kitu chochote zaidi ya kile ambacho Kristo amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu wa Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya,
Sithubutu kusema kitu kingine chochote isipokuwa tu kile ambacho Kristo Yesu amekifanya kwa kunitumia mimi ili watu wa mataifa wapate kutii. Amefanya hivyo kwa maneno na vitendo,
19 kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake mpaka Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa ukamilifu.
kwa nguvu ya miujiza na maajabu, na kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Basi, kwa kusafiri kila mahali, tangu kule Yerusalemu mpaka Iluriko, nimeihubiri kikamilifu Habari Njema ya Kristo.
20 Hivyo ni nia yangu kuhubiri Habari Njema, si pale ambapo Kristo amekwisha kujulikana, ili nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine.
Nia yangu imekuwa daima kuihubiri Habari Njema popote pale ambapo jina la Kristo halijapata kusikika, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine.
21 Lakini kama ilivyoandikwa: “Wale ambao hawajahubiriwa habari zake wataona, nao wale ambao hawajazisikia watafahamu.”
Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Watu wote ambao hawakuambiwa habari zote wataona; nao wale ambao hawajapata kusikia, wataelewa.”
22 Hii ndiyo sababu nimezuiliwa mara nyingi nisiweze kuja kwenu.
Kwa sababu hiyo nilizuiwa mara nyingi kuja kwenu.
23 Lakini sasa kwa kuwa hakuna nafasi zaidi kwa ajili yangu katika sehemu hii, ninatamani kuja kwenu kama ambavyo nimekuwa na shauku kwa miaka mingi.
Lakini maadam sasa nimemaliza kazi yangu pande hizi, na kwa kuwa kwa miaka mingi nimekuwa na nia kubwa ya kuja kwenu,
24 Nimekusudia kufanya hivyo nitakapokuwa njiani kwenda Hispania. Natarajia kuwaona katika safari yangu na kusafirishwa nanyi mpaka huko, baada ya kufurahia ushirika wenu kwa kitambo kidogo.
natumaini kufanya hivyo sasa. Ningependa kuwaoneni nikiwa safarini kwenda Spania na kupata msaada wenu kwa safari hiyo baada ya kufurahia kuwa kwa muda pamoja nanyi.
25 Sasa, niko njiani kuelekea Yerusalemu kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu huko.
Lakini, kwa sasa nakwenda kuwahudumia watu wa Mungu kule Yerusalem.
26 Kwa kuwa imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya maskini walioko miongoni mwa watakatifu huko Yerusalemu.
Maana makanisa ya Makedonia na Akaya yemeamua kutoka mchango wao kuwasaidia watu wa Mungu walio maskini huko Yerusalem.
27 Imewapendeza kufanya hivyo, naam, kwani ni wadeni wao. Kwa maana ikiwa watu wa Mataifa wameshiriki baraka za rohoni za Wayahudi, wao ni wadeni wa Wayahudi, ili Wayahudi nao washiriki baraka zao za mambo ya mwilini.
Wao wenyewe wameamua kufanya hivyo; lakini, kwa kweli, hilo ni jukumu lao kwa hao. Maana, ikiwa watu wa mataifa mengine wameshiriki baraka za kiroho za Wayahudi, wanapaswa nao pia kuwahudumia Wayahudi katika mahitaji yao ya kidunia.
28 Kwa hiyo baada ya kukamilisha kazi hii na kuhakikisha kuwa wamepokea kila kitu kilichokusanywa, nitapitia kwenu nikiwa njiani kwenda Hispania.
Nitakapokwisha tekeleza kazi hiyo na kuwakabidhi mchango huo uliokusanywa kwa ajili yao, nitawatembeleeni ninyi nikiwa safarini kwenda Spania.
29 Ninajua kwamba nitakapokuja kwenu, nitakuja na wingi wa baraka za Kristo.
Najua ya kuwa nikija kwenu nitawaletea wingi wa baraka za Kristo.
30 Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa upendo wa Roho Mtakatifu, kujiunga nami katika taabu zangu mkiniombea kwa Mungu.
Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa ajili ya upendo uletwao na Roho, mniunge mkono kwa kuniombea kwa Mungu.
31 Ombeni ili nipate kuokolewa mikononi mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, na kwamba utumishi wangu upate kukubaliwa na watakatifu wa huko Yerusalemu,
Ombeni nipate kutoka salama miongoni mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, nayo huduma yangu huko Yerusalem ipate kukubaliwa na watu wa Mungu walioko huko.
32 ili kwa mapenzi ya Mungu niweze kuja kwenu kwa furaha, nami niburudishwe pamoja nanyi.
Hivyo, Mungu akipenda, nitaweza kuja kwenu na moyo wa furaha, nikapumzike pamoja nanyi.
33 Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amen.
Mungu aliye chanzo cha amani na awe nanyi nyote! Amina!

< Warumi 15 >