< Warumi 12 >
1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana.
Kwa hiyo, ndugu zangu, maadam Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: jitoleeni nafsi zenu kwa Mungu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu.
2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu. (aiōn )
Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu, kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu. (aiōn )
3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa.
Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni ninyi nyote: msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kufuatana na kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja.
4 Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja,
Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake.
5 vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake.
Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake.
6 Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani.
Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kufuatana na neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake.
7 Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe,
Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe.
8 kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.
Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha.
9 Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema.
Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema.
10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine.
Pendaneni kidugu; kila mmoja amfikirie mwenzake kwanza kwa heshima.
11 Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana.
Msilegee katika bidii, muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana.
12 Kuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi.
Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida na kusali daima.
13 Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni.
Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu.
14 Wabarikini wale wanaowatesa, barikini wala msilaani.
Watakieni baraka wote wanaowadhulumu ninyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani.
15 Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao.
Furahini pamoja na wanaofurahi, lieni pamoja na wanaolia.
16 Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu.
Muwe na wema uleule kwa kila mtu. Msijitakie makuu, bali jishugulisheni na watu wadogo. Msijione kuwa wenye hekima sana.
17 Msimlipe mtu yeyote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote.
Msilipe ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote.
18 Kama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote.
Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote.
19 Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana.
Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza asema Bwana.”
20 Badala yake: “Kama adui yako ana njaa, mlishe; kama ana kiu, mpe kinywaji. Kwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”
Tena, Maandiko yasema: “Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake.”
21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.
Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema.