< Warumi 10 >

1 Ndugu zangu, shauku ya moyo wangu na maombi yangu kwa Mungu ni kwa ajili ya Waisraeli, kwamba waokolewe.
Ndugu, nia ya moyo wangu na ombi langu kwa Mungu ni kwa ajili yao, kwa ajili ya wokovu wao.
2 Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wana juhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa.
Kwa kuwa nawashuhudia kwamba wanajuhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si kwa ajili ya ufahamu.
3 Kwa kuwa hawakuijua haki itokayo kwa Mungu, wakatafuta kuweka haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.
Kwa kuwa hawajui haki ya Mungu, na wanatafuta kujenga haki yao wenyewe. Hawakuwa watiifu kwa haki ya Mungu.
4 Kwa maana Kristo ni ukomo wa sheria ili kuwe na haki kwa kila mtu aaminiye.
Kwa kuwa Kristo ndiye utimilifu wa sheria kwa ajili ya haki ya kila mtu aaminiye.
5 Mose anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.”
Kwa kuwa Musa anaandika kuhusu haki ambayo huja kutokana na sheria: “Mtu ambaye hutenda haki ya sheria ataishi kwa haki hii.”
6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’” (yaani ili kumleta Kristo chini)
Lakini haki ambayo inatokana na imani husema hivi, “Usiseme moyoni mwako, 'Nani atapaa kwenda mbinguni?' (Hii ni kumleta Kristo chini).
7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.) (Abyssos g12)
Na usiseme, 'Nani atashuka katika shimo?”' (Hii ni, kumleta Kristo juu kutoka kwa wafu). (Abyssos g12)
8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri.
Lakini inasema nini? “Neno liko karibu na wewe, katika kinywa chako na katika moyo wako.” Hilo ni neno la imani, ambalo tunatangaza.
9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka.
Kwa kuwa kama kwa kinywa chako unamkiri Yesu ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka.
10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu.
Kwa kuwa kwa moyo mtu huamini na kupata haki, na kwa kinywa hukiri na kupata wokovu.
11 Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.”
Kwa kuwa andiko lasema, “Kila amwaminiye hata aibika.”
12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao.
kwa kuwa hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani. Kwa kuwa Bwana yule yule ni Bwana wa wote, na ni tajiri kwa wote wamwitao.
13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”
Kwa kuwa kila mtu ambaye huliitia jina la Bwana ataokoka.
14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria?
Kwa jinsi gani wanaweza kumwita yeye ambaye hawajamwamini? Na jinsi gani wanaweza kuamini katika yeye ambaye hawajamsikia? Na watasikiaje pasipo muhubiri?
15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!”
Na jinsi gani wanaweza kuhubiri, isipokuwa wametumwa? - Kama ilivyoandikwa, “Jinsi gani ni mizuri miguu ya wale ambao wanatangaza habari za furaha za mambo mema!”
16 Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?”
Lakini wote hawakusikiliza injili. Kwa kuwa Isaya hunena, “Bwana, ni nani aliyesikia ujumbe wetu?”
17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.
Hivyo imani huja kutokana na kusikia, na kusikia kwa neno la Kristo.
18 Lakini nauliza: Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana: “Sauti yao imeenea duniani pote, nayo maneno yao yameenea hadi miisho ya ulimwengu.”
Lakini nasema, “Je hawakusikia?” Ndiyo, kwa hakika sana. “Sauti yao imekwisha toka nje katika nchi yote, na maneno yao kwenda miisho ya dunia.”
19 Nami nauliza tena: Je, Waisraeli hawakuelewa? Kwanza, Mose asema, “Nitawafanya mwe na wivu kwa watu wale ambao si taifa. Nitawakasirisha kwa taifa lile lisilo na ufahamu.”
Zaidi ya yote, Ninasema, “Je Israel hakujua?” Kwanza Musa hunena, “Nitawachokoza kuwatia wivu kwa watu ambao si taifa. Kwa njia ya taifa lisilo na uelewa, nitawachochea hadi mkasirike.”
20 Naye Isaya kwa ujasiri mwingi anasema, “Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta. Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakunitafuta.”
Na Isaya ni jasiri sana na husema, “Nilipatikana na wale ambao hawakunitafuta. Nilionekana kwa wale ambao hawakunihitaji.”
21 Lakini kuhusu Israeli anasema, “Mchana kutwa nimewanyooshea watu wakaidi na wasiotii mikono yangu.”
Lakini kwa Israel husema, “Siku zote nilinyoosha mikono yangu kwa wasiotii na kwa watu wagumu.”

< Warumi 10 >