< Ufunuo 8 >

1 Mwana-Kondoo alipoivunja ile lakiri ya saba, pakawa kimya mbinguni kwa muda wa nusu saa.
Wakati Mwanakondoo alipofungua muhuri ya saba, kukawa na ukimya mbinguni takribani nusu saa.
2 Nami nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele za Mungu, nao wakapewa tarumbeta saba.
Kisha nikaona malaika saba wasimamao mbele za Mungu, na wakapewa tarumbeta saba.
3 Malaika mwingine aliyekuwa na chetezo cha dhahabu, akaja na kusimama mbele ya madhabahu. Akapewa uvumba mwingi ili autoe pamoja na maombi ya watakatifu wote, juu ya yale madhabahu ya dhahabu yaliyo mbele ya kile kiti cha enzi.
Malaika mwingine akaja, ameshikilia bakuli ya dhahabu yenye uvumba, amesimama madhabahuni. Akapewa uvumba mwingi ili kwamba autoe pamoja na maombi ya waamini wote katika madhabahu ya dhahabu mbele ya kiti cha enzi.
4 Ule moshi wa uvumba pamoja na yale maombi ya watakatifu, vikapanda juu mbele za Mungu, kutoka mkononi mwa huyo malaika.
Moshi wa ule uvumba, pamoja na maombi ya waamini, ukapanda juu mbele za Mungu kutoka mkononi mwa malaika.
5 Kisha yule malaika akachukua kile chetezo, akakijaza moto kutoka kwa yale madhabahu, akautupa juu ya dunia. Pakatokea sauti za radi, ngurumo, umeme wa radi na tetemeko la ardhi.
Malaika akatwaa bakuli la uvumba na akalijaza moto kutoka kwenye madhabahu. Kisha akalitupa chini juu ya nchi, na kukatokea sauti za radi, miale ya radi na tetemeko la nchi.
6 Basi wale malaika saba waliokuwa na zile tarumbeta saba wakajiandaa kuzipiga.
Wale malaika saba ambao walikuwa na tarumbeta saba wakawa tayari kuzipiga.
7 Malaika wa kwanza akaipiga tarumbeta yake, pakatokea mvua ya mawe na moto uliochanganyika na damu, navyo vikatupwa kwa nguvu juu ya nchi. Na theluthi ya dunia ikateketea, theluthi ya miti ikateketea, na nyasi yote mbichi ikateketea.
Malaika wa kwanza akaipiga tarumbeta yake, na kukatokea mvua ya mawe na moto uliochanganyikana na damu. Vikatupwa chini katika nchi ili kwamba theluthi yake iungue, theluthi ya miti ikaungua na nyasi zote za kijani zikaungua.
8 Malaika wa pili akaipiga tarumbeta yake na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi ya bahari ikawa damu,
Malaika wa pili akaipiga tarumbeta yake, na kitu kama mlima mkubwa uliokuwa unaungua kwa moto ukatupwa baharini. Theluthi ya bahari ikawa damu,
9 theluthi ya viumbe vyenye uhai viishivyo baharini vikafa na theluthi ya meli zikaharibiwa.
theluthi ya viumbe hai katika bahari vikafa, na theluthi ya meli zikaharibiwa.
10 Malaika wa tatu akaipiga tarumbeta yake, na nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa ikaanguka toka angani, ikaangukia theluthi ya mito na chemchemi za maji.
Malaika wa tatu akaipiga tarumbeta yake, na nyota kubwa ikaanguka kutoka mbinguni, ikimulika kama kurunzi, juu ya theluthi ya mito na chemichemi za maji.
11 Nyota hiyo inaitwa Uchungu. Theluthi ya maji yakawa machungu na watu wengi wakafa kutokana na maji hayo kwa maana yalikuwa machungu.
Jina la nyota ni pakanga. Theluthi ya maji ikawa pakanga, na watu wengi wakafa kutokana na maji yaliyokuwa machungu.
12 Kisha malaika wa nne akaipiga tarumbeta yake, na theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota zikapigwa. Kwa hiyo theluthi moja ya mwanga ikawa giza. Theluthi ya mchana ikawa haina mwanga na pia theluthi ya usiku.
Malaika wa nne alipiga tarumbeta yake, na theluthi ya jua ikapigwa, pamoja na theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota. Kwa hiyo theluthi ya vyote ikageuka kuwa giza; theluthi ya mchana na theluthi ya usiku havikuwa na mwanga.
13 Nilipokuwa tena nikitazama, nikamsikia tai mmoja akipiga kelele kwa sauti kuu wakati akiruka katikati ya mbingu, akisema, “Ole! Ole! Ole wa watu waishio duniani, kwa sababu ya tarumbeta ambazo malaika hao wengine watatu wanakaribia kuzipiga!”
Nilitazama, na nikasikia tai aliye kuwa anaruka katikati ya anga, akiita kwa sauti kuu, “Ole, ole, ole, kwa wale wakaao katika nchi, kwa sababu ya mlipuko wa tarumbeta iliyosalia ambayo imekaribia kupigwa na malaika watatu.”

< Ufunuo 8 >