< Ufunuo 5 >

1 Kisha nikaona katika mkono wake wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na upande wa nje, kikiwa kimefungwa kwa lakiri saba.
Kisha katika mkono wa kulia wa huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi, nikaona kitabu; nacho kilikuwa kimeandikwa ndani na nje na kufungwa na mihuri saba.
2 Nami nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kuu, akisema, “Ni nani anayestahili kuzivunja hizo lakiri na kukifungua kitabu?”
Tena nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kubwa: “Nani anayestahili kuvunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu hicho?”
3 Lakini hapakuwa na yeyote mbinguni wala duniani au chini ya dunia aliyeweza kukifungua hicho kitabu wala hata kutazama ndani yake.
Lakini hakupatikana mtu yeyote mbinguni, wala duniani, wala chini Kuzimu, aliyeweza kukifungua hicho kitabu au kukitazama ndani. (questioned)
4 Nikalia sana sana kwa sababu hakuonekana yeyote anayestahili kukifungua hicho kitabu wala kutazama ndani yake.
Basi, mimi nikalia sana kwa sababu hakupatikana mtu aliyestahili kukifungua, au kukitazama ndani.
5 Kisha, mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama, Simba wa kabila la Yuda, wa Uzao wa Daudi, ameshinda. Yeye ndiye anayeweza kukifungua hicho kitabu na kuvunja hizo lakiri zake saba.”
Kisha mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama! Simba wa kabila la Yuda, mjukuu maarufu wa Daudi, ameshinda. Yeye anaweza kuivunja mihuri yake saba na kukifungua hicho kitabu.”
6 Ndipo nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale viumbe wenye uhai wanne na miongoni mwa wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, akiwa kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambazo ndizo zile Roho saba za Mungu zilizotumwa duniani pote.
Kisha nikaona pale katikati ya kiti cha enzi Mwana kondoo amesimama, akizungukwa kila upande na vile viumbe hai vinne, na wale wazee. Huyo Mwanakondoo alionekana kana kwamba amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba ambayo ni roho saba za Mungu zilizokuwa zimepelekwa kila mahali duniani.
7 Huyo Mwana-Kondoo akaja na kukitwaa kile kitabu kutoka kwenye mkono wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi.
Mwanakondoo akaenda, akakitwaa hicho kitabu kutoka mkono wa kulia wa yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi.
8 Alipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu.
Mara tu alipokwisha twaa hicho kitabu, vile viumbe hai vinne pamoja na wale wazee ishirini na wanne walianguka kifudifudi mbele ya Mwanakondoo. Kila mmoja, alikuwa na kinubi na bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni sala za watu wa Mungu.
9 Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema: “Wewe unastahili kukitwaa kitabu na kuzivunja lakiri zake, kwa sababu ulichinjwa na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu kutoka kila kabila, kila lugha, kila jamaa na kila taifa.
Basi, wakaimba wimbo huu mpya: “Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu na kuivunja mihuri yake. Kwa sababu wewe umechinjwa, na kwa damu yako umemnunulia Mungu watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.
10 Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani wa kumtumikia Mungu wetu, nao watatawala duniani.”
Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani wamtumikie Mungu wetu nao watatawala duniani.”
11 Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu.
Kisha nikatazama, nikasikia sauti ya malaika wengi sana, idadi isiyohesabika, maelfu na maelfu. Walikuwa wamekaa kuzunguka kiti cha enzi, vile viumbe hai vinne na wale wazee;
12 Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema: “Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa, kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na sifa!”
wakasema kwa sauti kuu: “Mwanakondoo aliyechinjwa anastahili kupokea uwezo, utajiri, hekima, nguvu, utukufu na sifa.”
13 Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba: “Sifa na heshima na utukufu na uweza ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi na kwa Mwana-Kondoo, milele na milele!” (aiōn g165)
Nikasikia viumbe vyote mbinguni, duniani, chini kuzimuni na baharini—viumbe vyote ulimwenguni—vikisema: “Kwake yeye aketiye katika kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo, iwe sifa na heshima na utukufu na enzi milele na milele.” (aiōn g165, questioned)
14 Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee ishirini na wanne wakaanguka kifudifudi wakaabudu.
Na vile viumbe vinne hai vikasema, “Amina!” Na wale wazee wakaanguka kifudifudi, wakaabudu.

< Ufunuo 5 >