< Ufunuo 16 >

1 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mle Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni, mkayamwage duniani hayo mabakuli saba ya ghadhabu ya Mungu.”
Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni mkamwage mabakuli hayo saba ya ghadhabu ya Mungu duniani.”
2 Malaika wa kwanza akaenda akalimwaga hilo bakuli lake juu ya nchi. Majipu mabaya yenye maumivu makali yakawapata wale watu wote waliokuwa na chapa ya yule mnyama na walioabudu sanamu yake.
Basi, malaika wa kwanza akaenda akamwaga bakuli lake juu ya nchi. Mara madonda mabaya na ya kuumiza sana yakawapata wote waliokuwa na alama ya yule mnyama, na wale walioiabudu sanamu yake.
3 Malaika wa pili akalimwaga bakuli lake baharini, nayo ikabadilika kuwa damu kama ya mtu aliyekufa na kila kiumbe hai kilichokuwa ndani ya bahari kikafa.
Kisha malaika wa pili akamwaga bakuli lake baharini. Nayo bahari ikawa damu tupu kama damu ya mtu aliyekufa, na viumbe vyote hai baharini vikafa.
4 Malaika wa tatu akalimwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, nazo zikawa damu.
Malaika wa tatu akamwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, navyo vikageuka damu.
5 Ndipo nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema: “Wewe una haki katika hukumu hizi ulizotoa, wewe uliyeko, uliyekuwako, Uliye Mtakatifu, kwa sababu umehukumu hivyo;
Nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema, “Ewe mtakatifu, Uliyeko na uliyekuwako! Wewe ni mwenye haki katika hukumu hii uliyotoa.
6 kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu wako na manabii wako, nawe umewapa damu wanywe kama walivyostahili.”
Maana waliimwaga damu ya watu wako na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; wamestahili hivyo!”
7 Nikasikia madhabahu ikiitikia, “Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, hukumu zako ni kweli na haki.”
Kisha nikasikia sauti madhabahuni ikisema, “Naam, Bwana Mungu Mwenye Uwezo! Hukumu zako ni za kweli na haki!”
8 Malaika wa nne akamimina bakuli lake kwenye jua, nalo likapewa nguvu za kuwaunguza watu kwa moto.
Kisha malaika wa nne akamwaga bakuli lake juu ya jua. Jua likapewa nguvu ya kuwachoma watu kwa moto wake.
9 Watu wakaunguzwa na hilo joto kali, wakalaani Jina la Mungu, aliyekuwa na uwezo juu ya mapigo haya, tena wakakataa kutubu na kumtukuza Mungu.
Basi, watu wakaunguzwa vibaya sana; wakamtukana Mungu aliye na uwezo juu ya mabaa hayo makubwa. Lakini hawakuziacha dhambi zao na kumtukuza Mungu.
10 Malaika wa tano akamimina bakuli lake kwenye kiti cha enzi cha yule mnyama, nao ufalme wake ukagubikwa na giza. Watu wakatafuna ndimi zao kwa ajili ya maumivu,
Kisha malaika wa tano akamwaga bakuli lake juu ya makao makuu ya yule mnyama. Giza likauvamia utawala wake, watu wakauma ndimi zao kwa sababu za maumivu,
11 wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majeraha yao, wala hawakutubu kwa ajili ya matendo yao maovu.
wakamtukana Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu yao na madonda yao. Lakini hawakuyaacha matendo yao mabaya.
12 Malaika wa sita akamimina bakuli lake kwenye mto mkubwa Frati, maji yake yakakauka ili kutayarisha njia kwa ajili ya wafalme watokao Mashariki.
Kisha malaika wa sita akamwaga bakuli lake juu ya mto mkubwa uitwao Eufrate. Maji yake yakakauka, na hivyo njia ilitengenezwa kwa ajili ya wafalme wa mashariki.
13 Kisha nikaona roho wachafu watatu waliofanana na vyura wakitoka katika kinywa cha lile joka na katika kinywa cha yule mnyama na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.
Kisha nikaona pepo wabaya watatu walio kama vyura, wakitoka kinywani mwa yule joka, kinywani mwa yule mnyama, na kinywani mwa yule nabii wa uongo.
14 Hizo ndizo roho za pepo wachafu zitendazo miujiza. Nazo huwaendea wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya tayari kwa ajili ya vita katika siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.
Hawa ndio roho za pepo wafanyao miujiza. Ndio wanaokwenda kwa wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya pamoja kwa ajili ya vita kuu Siku ile ya Mungu Mwenye Uwezo.
15 “Tazama, naja kama mwizi! Amebarikiwa yeye akeshaye na kuziweka tayari nguo zake ili asiende uchi na kuonekana aibu yake.”
“Sikiliza! Mimi naja kama mwizi! Heri mtu akeshaye na kuvaa nguo zake ili asije akaenda uchi huko na huko mbele ya watu.”
16 Ndipo wakawakusanya wafalme pamoja mahali paitwapo Armagedoni kwa Kiebrania.
Basi, roho hao wakawakusanya hao wafalme mahali paitwapo kwa Kiebrania Harmagedoni.
17 Malaika wa saba akamimina bakuli lake angani na sauti kubwa ikatoka mle hekaluni katika kile kiti cha enzi, ikisema, “Imekwisha kuwa!”
Kisha malaika wa saba akamwaga bakuli lake hewani. Sauti kubwa ikasikika kutoka kwenye kiti cha enzi, Hekaluni, ikisema, “Mwisho umefika!”
18 Kukawa na mianga ya umeme wa radi, ngurumo, radi na tetemeko kubwa la ardhi. Hapajawa kamwe na tetemeko la ardhi kama hilo tangu mwanadamu awepo duniani, hivyo lilikuwa tetemeko kubwa ajabu.
Kukatokea umeme, kelele, ngurumo na tetemeko kubwa la ardhi ambalo halijapata kutokea tangu Mungu alipomuumba mtu.
19 Ule mji mkubwa ukagawanyika katika sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikaanguka. Mungu akaukumbuka Babeli Mkuu na kumpa kikombe kilichojaa mvinyo wa ghadhabu ya hasira yake.
Mji ule mkuu ukapasuliwa sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikateketea. Babuloni, mji mkuu, haukusahauliwa na Mungu. Aliunywesha kikombe cha divai ya ghadhabu yake kuu.
20 Kila kisiwa kikatoweka wala milima haikuonekana.
Visiwa vyote vikatoweka, nayo milima haikuonekena tena.
21 Mvua kubwa ya mawe yenye uzito wa talanta moja ikashuka kutoka mbinguni, ikawaangukia wanadamu. Nao wanadamu wakamlaani Mungu kwa ajili ya hayo mapigo ya mvua ya mawe, kwa sababu pigo hilo lilikuwa la kutisha.
Mvua ya mawe makubwa yenye uzito wa kama kilo hamsini kila moja, ikawanyeshea watu. Nao wakamtukana Mungu kwa sababu ya mapigo ya mvua hiyo ya mawe. Naam, pigo la mvua hiyo ya mawe lilikuwa kubwa mno.

< Ufunuo 16 >