< Ufunuo 15 >

1 Ndipo nikaona ishara nyingine kubwa ya ajabu mbinguni: malaika saba wenye yale mapigo saba ya mwisho, kwa sababu kwa mapigo hayo ghadhabu ya Mungu ilikuwa imekamilika.
Kisha nikaona ishara nyingine mbinguni, kubwa na ya kushangaza. Palikuwa hapo malaika saba wenye mabaa makubwa saba ya mwisho. Kwa mabaa hayo makubwa saba, ghadhabu ya Mungu imekamilishwa.
2 Nikaona kile kilichoonekana kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Kando ya hiyo bahari, walikuwa wamesimama wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake pamoja na tarakimu ya jina lake. Mikononi mwao walikuwa wameshika vinubi walivyopewa na Mungu.
Kisha nikaona kitu kama bahari ya kioo, imechanganywa na moto. Nikawaona pia wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake na ambaye jina lake lilitajwa kwa ile tarakimu. Watu hao walikuwa wamesimama kando ya hiyo bahari ya kioo, wakiwa na vinubi walivyopewa na Mungu.
3 Nao wakaimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema: “Bwana Mungu Mwenyezi, matendo yako ni makuu na ya ajabu. Njia zako wewe ni za haki na za kweli, Mfalme wa nyakati zote!
Walikuwa wakiimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwanakondoo: “Bwana Mungu Mwenye Uwezo, matendo yako ni makuu mno! Ewe Mfalme wa mataifa, njia zako ni za haki na za kweli!
4 Ni nani ambaye hatakuogopa wewe Bwana na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako ndiwe mtakatifu. Mataifa yote yatakuja na kuabudu mbele zako, kwa kuwa matendo yako ya haki yamedhihirishwa.”
Bwana, ni nani asiyekucha wewe? Nani asiyelitukuza jina lako? Wewe peke yako ni Mtakatifu. Mataifa yote yatakujia na kukuabudu maana matendo yako ya haki yameonekana na wote.”
5 Baada ya haya nikatazama, nalo hekalu, la hema la Ushuhuda, lilikuwa limefunguliwa mbinguni.
Baada ya hayo nikaona Hekalu limefunguliwa mbinguni, na ndani yake hema ionyeshayo kuwapo kwa Mungu.
6 Ndani ya lile hekalu wakatoka malaika saba wakiwa na mapigo saba. Walikuwa wamevaa nguo safi za kitani ingʼaayo na kufungwa mikanda ya dhahabu vifuani mwao.
Basi, wale malaika saba wenye mabaa saba wakatoka humo Hekaluni, wakiwa wamevaa nguo za kitani safi zenye kung'aa, na kanda za dhahabu vifuani mwao.
7 Ndipo mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akawapa wale malaika saba mabakuli saba ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, yeye aishiye milele na milele. (aiōn g165)
Kisha, mmojawapo wa vile viumbe vinne akawapa hao malaika saba mabakuli ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele. (aiōn g165)
8 Nalo lile hekalu lilijawa na moshi uliotokana na utukufu wa Mungu na uweza wake, wala hakuna yeyote aliyeweza kuingia mle hekaluni mpaka yale mapigo saba ya wale malaika saba yalipomalizika.
Hekalu likajaa moshi uliosababishwa na utukufu na nguvu ya Mungu, na hakuna mtu aliyeweza kuingia Hekaluni mpaka mwisho wa mabaa makubwa saba ya wale malaika saba.

< Ufunuo 15 >