< Ufunuo 12 >

1 Kukaonekana ishara kuu mbinguni: Palikuwa na mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ukiwa chini ya miguu yake, na taji ya nyota kumi na mbili ilikuwa kichwani mwake.
Ishara kuu ilionekana mbinguni: mwanamke aliyefunikwa na jua, na akiwa na mwezi chini ya miguu yake; na taji ya nyota kumi na mbili ilikuwa juu ya kichwa chake.
2 Alikuwa na mimba naye akilia kwa uchungu kwa kuwa alikuwa anakaribia kuzaa.
Alikuwa na mimba na alikuwa analia kwa ajili ya maumivu ya kuzaa—katika uchungu wa kujifungua.
3 Kisha ishara nyingine ikaonekana mbinguni: Likaonekana joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na pembe kumi na taji saba katika vichwa vyake.
Na ishara nyingine ilionekana mbinguni: Tazama! Kulikuwa na joka mwekundu mkubwa ambaye alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na kulikuwa na taji saba kwenye vichwa vyake.
4 Mkia wake ukakokota theluthi ya nyota zote angani na kuziangusha katika nchi. Ndipo lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa ili lipate kumla huyo mtoto mara tu atakapozaliwa.
Mkia wake ulikokota theluthi moja ya nyota mbinguni na kuzitupa chini duniani. Joka alisimama mbele ya mwanamke aliyekuwa anakaribia kuzaa, ili kwamba wakati anazaa, apate kummeza mtoto wake.
5 Yule mwanamke akazaa mtoto mwanaume, atakayeyatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya utawala ya chuma. Lakini huyo mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu kwenye kiti chake cha enzi.
Alimzaa mwana, mtoto wa kiume, ambaye atayatawala mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Mtoto wake alinyakuliwa juu kwa Mungu na kwenye kiti chake cha enzi,
6 Yule mwanamke akakimbilia jangwani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali ili apate kutunzwa huko kwa muda wa siku 1,260.
na mwanamke alikimbilia nyikani, mahali ambapo Mungu alikuwa ameandaa eneo kwa ajili yake, ili aweze kuhudumiwa kwa siku 1, 260.
7 Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao.
Sasa kulikuwa na vita mbinguni. Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka; naye joka mkubwa na malaika zake wakapigana nao.
8 Lakini joka na malaika zake wakashindwa, na hapakuwa tena na nafasi yao huko mbinguni.
Lakini joka hakuwa na nguvu za kutosha kushinda. Kwa hiyo haikuwepo tena nafasi mbinguni kwa ajili yake na malaika zake.
9 Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwengu wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake.
Joka mkubwa—yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani ambaye hudanganya - dunia nzima akatupwa chini katika dunia, na malaika zake wakatupwa chini pamoja naye.
10 Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema: “Sasa wokovu na uweza na Ufalme wa Mungu wetu umekuja na mamlaka ya Kristo wake. Kwa kuwa ametupwa chini mshtaki wa ndugu zetu, anayewashtaki mbele za Mungu usiku na mchana.
Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mbinguni: “Sasa wokovu umekuja, nguvu—na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake. Kwa kuwa mshitaki wa ndugu zetu ametupwa chini—ambaye aliwashitaki mbele za Mungu wetu mchana na usiku.
11 Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo na kwa neno la ushuhuda wao. Wala wao hawakuyapenda maisha yao hata kufa.
Walimshinda kwa damu ya Mwanakondoo na kwa neno la ushuhuda wao, kwa maana hawakupenda sana maisha yao, hata kufa.
12 Kwa hiyo, furahini ninyi mbingu na wote wakaao humo! Lakini ole wenu nchi na bahari, kwa maana huyo ibilisi ameshuka kwenu, akiwa amejaa ghadhabu, kwa sababu anajua ya kuwa muda wake ni mfupi!”
Kwa hiyo, shangilieni, ninyi mbingu, na wote mnaokaa ndani yake. Lakini ole wa nchi na bahari kwa sababu mwovu ameshuka kwenu. Amejawa na hasira kali, kwa sababu anajua kwamba ana muda mchache tu.
13 Lile joka lilipoona kuwa limetupwa chini duniani, lilimfuatilia yule mwanamke aliyekuwa amezaa mtoto mwanaume.
Wakati joka alipotambua kuwa ametupwa chini kwenye nchi, alimfuata mwanamke ambaye alikuwa amezaa mtoto wa kiume.
14 Lakini huyo mwanamke akapewa mabawa mawili ya tai mkubwa, kusudi aweze kuruka mpaka mahali palipotayarishwa kwa ajili yake huko jangwani, ambako atatunzwa kwa wakati na nyakati na nusu, ya wakati ambako yule joka hawezi kufika.
Lakini mwanamke alipewa mabawa mawili ya tai mkubwa, ili kwamba aweze kuruka hadi kwenye eneo lililoandaliwa kwa ajili yake kule jangwani, eneo ambalo angeweza kutunzwa, kwa wakati, nyakati na nusu wakati-mahali asipoweza kupafikia huyo nyoka.
15 Ndipo lile joka likamwaga maji kama mto kutoka kinywani mwake, ili kumfikia huyo mwanamke na kumkumba kama mafuriko.
Nyoka alimwaga maji kutoka mdomoni mwake kama mto, ili afanye gharika ya kumgharikisha.
16 Lakini nchi ikamsaidia huyo mwanamke kwa kufungua kinywa na kuumeza huo mto ambao huyo joka alikuwa ameutoa kinywani mwake.
Lakini ardhi ilimsaidia mwanamke. Ilifunua kinywa chake na kuumeza mto alioutema joka kutoka kinywani mwake.
17 Kisha lile joka likapatwa na hasira kali kwa ajili ya huyo mwanamke na likaondoka ili kupigana vita na watoto waliosalia wa huyo mwanamke, yaani, wale wanaozitii amri za Mungu na kuushika ushuhuda wa Yesu Kristo.
Kisha joka akamkasirikia mwanamke naye aliondoka na kufanya vita na uzao wake wote—wale wanaotii amri za Mungu na kushikilia ushuhuda kuhusu Yesu.

< Ufunuo 12 >