< Zaburi 99 >

1 Bwana anatawala, mataifa na yatetemeke; anakalia kiti cha enzi katikati ya makerubi, dunia na itikisike.
Yahwe anatawala; mataifa na yatetemeke. Ameketi juu ya makerubi; nchi inatetemeka.
2 Bwana ni mkuu katika Sayuni; ametukuzwa juu ya mataifa yote.
Yahwe ni mkuu katika Sayuni; naye ametukuka juu ya mataifa yote.
3 Wanalisifu jina lako ambalo ni kuu na la kuogopwa: yeye ni mtakatifu!
Nao walisifu jina lako kuu na lenye kutisha; yeye ni mtakatifu.
4 Mfalme ni mwenye nguvu na hupenda haki, wewe umethibitisha adili; katika Yakobo umefanya yaliyo haki na sawa.
Mfalme ana nguvu, naye hupenda haki. Wewe umeimarisha haki; umetenda haki na hukumu katika Yakobo.
5 Mtukuzeni Bwana Mungu wetu, na mkaabudu katika mahali pa kuwekea miguu yake; yeye ni mtakatifu.
Msifuni Yahwe Mungu wetu na sujuduni miguuni pake. Yeye ni mtakatifu.
6 Mose na Aroni walikuwa miongoni mwa makuhani wake, Samweli alikuwa miongoni mwa walioliitia jina lake; walimwita Bwana, naye aliwajibu.
Musa na Haruni walikuwa miongoni mwa makuhani wake, na Samweli alikuwa miongoni mwa wale walio muomba Yeye. Walimuomba Yahwe, naye akawajibu.
7 Alizungumza nao kutoka nguzo ya wingu; walizishika sheria zake na amri alizowapa.
Alizungumza nao toka nguzo ya wingu. Walizishika amri zake takatifu na sheria ambazo aliwapatia.
8 Ee Bwana, wetu, ndiwe uliyewajibu, kwa Israeli ulikuwa Mungu mwenye kusamehe, ingawa uliadhibu matendo yao mabaya.
Wewe uliwajibu, Yahwe Mungu wetu. Ulikuwa kwao Mungu mwenye kusamehe, lakini uliye adhibu matendo yao ya dhambi.
9 Mtukuzeni Bwana Mungu wetu, mwabuduni kwenye mlima wake mtakatifu, kwa maana Bwana Mungu wetu ni mtakatifu.
Msifuni Yahwe Mungu wetu, na mwabuduni kwenye mlima wake mtakatifu, maana Yahwe Mungu wetu ni Mtakatifu.

< Zaburi 99 >