< Zaburi 97 >
1 Bwana anatawala, nchi na ifurahi, visiwa vyote vishangilie.
Yahwe anatawala; nchi ishangilie; visiwa vingi na vifurahi.
2 Mawingu na giza nene vinamzunguka, haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake cha enzi.
Mawingu na giza vyamzunguka. Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.
3 Moto hutangulia mbele zake na huteketeza adui zake pande zote.
Moto huenda mbele zake nao huwateketeza adui zake pande zote.
4 Umeme wake wa radi humulika dunia, nchi huona na kutetemeka.
Taa yake huangaza ulimwengu; nchi huona na kutetemeka.
5 Milima huyeyuka kama nta mbele za Bwana, mbele za Bwana wa dunia yote.
Milima huyeyuka kama nta mbele za Yahwe, Bwana wa dunia yote.
6 Mbingu zinatangaza haki yake, na mataifa yote huona utukufu wake.
Mbingu hutangaza haki yake, na mataifa yote huuona utukufu wake.
7 Wote waabuduo sanamu waaibishwa, wale wajisifiao sanamu: mwabuduni yeye, enyi miungu yote!
Wale wote waabuduo sanamu za kuchonga wataaibishwa, wale wanao jivuna katika sanamu zisizo na maana mpigieni yeye magoti, enyi miungu wote!
8 Sayuni husikia na kushangilia, vijiji vya Yuda vinafurahi kwa sababu ya hukumu zako, Ee Bwana.
Sayuni ilisikia na kufurahi, na miji ya Yuda ilishangilia kwa sababu ya amri zako za haki, Yahwe.
9 Kwa kuwa wewe, Ee Bwana, ndiwe Uliye Juu Sana kuliko dunia yote; umetukuka sana juu ya miungu yote.
Kwa kuwa wewe, Yahwe, ndiye uliye juu sana, juu ya nchi yote. Umetukuka sana juu ya miungu yote.
10 Wale wanaompenda Bwana na wauchukie uovu, kwa maana yeye hulinda maisha ya waaminifu wake na kuwaokoa kutoka mkononi mwa mwovu.
Ninyi ambao mnampenda Yahwe, chukieni uovu! Yeye hulinda uhai wa watakatifu wake, naye huwatoa mikononi mwa waovu.
11 Nuru huangaza wenye haki na furaha kwa watu wanyofu wa moyo.
Nuru imepandwa kwa ajili ya wenye haki na furaha kwa ajili ya wanyoofu wa moyo.
12 Furahini katika Bwana, ninyi mlio wenye haki, lisifuni jina lake takatifu.
Furahini katika Yahwe, enyi wenye haki; na mpeni shukurani mkumbukapo utakatifu wake.