< Zaburi 95 >
1 Njooni, tumwimbie Bwana kwa furaha; tumfanyie kelele za shangwe Mwamba wa wokovu wetu.
Oh njoni, tumwimbie Yahwe; na tumwimbie kwa shangwe mwamba wa wokovu wetu.
2 Tuje mbele zake kwa shukrani, tumtukuze kwa vinanda na nyimbo.
Tuingie uweponi mwake kwa shukrani; tumwimbie yeye kwa zaburi ya sifa.
3 Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu, mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Kwa maana Yahwe ni Mungu mkuu na Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
4 Mkononi mwake mna vilindi vya dunia, na vilele vya milima ni mali yake.
Mkononi mwake zimo bonde za dunia; navyo vilele vya milima ni vyake.
5 Bahari ni yake, kwani ndiye aliifanya, na mikono yake iliumba nchi kavu.
Bahari ni yake, maana aliiumba, na mikono yake ilitengeneza nchi kavu.
6 Njooni, tusujudu, tumwabudu, tupige magoti mbele za Bwana Muumba wetu,
Oh njoni, tumwabudu na tupige magoti; tupige magoti mbele za Yahwe, muumbaji wetu:
7 kwa maana yeye ndiye Mungu wetu, na sisi ni watu wa malisho yake, kondoo chini ya utunzaji wake. Kama mkiisikia sauti yake leo,
Kwa maana yeye ni Mungu wetu, na sisi tu watu wa malisho yake na kondoo wa mkono wake. Ni heri leo mngesikia sauti yake!
8 msiifanye mioyo yenu migumu kama mlivyofanya kule Meriba, kama mlivyofanya siku ile kule Masa jangwani,
Msiifanye migumu mioyo yenu, kama vile huko Meriba, au kama ile siku ya Masa jangwani,
9 ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima, ingawa walikuwa wameyaona matendo yangu.
ambako baba zenu walinijaribu na kunipima, japo walikuwa wameyaona matendo yangu.
10 Kwa miaka arobaini nilikasirikia kizazi kile, nikasema, “Hawa ni taifa ambalo mioyo yao imepotoka, nao hawajazijua njia zangu.”
Kwa miaka arobaini nilikasirishwa na kizazi hicho na kusema, 'Hawa ni watu ambao mioyo yao imepotoka; hawazijui njia zangu.'
11 Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu, “Kamwe hawataingia rahani mwangu.”
Hivyo katika hasira yangu niliapa kwamba wasingeingia kamwe mahali pa pumziko.”