< Zaburi 94 >

1 Ee Bwana, ulipizaye kisasi, Ee Mungu ulipizaye kisasi, uangaze sasa.
Yahwe, Ee Mungu ulipaye kisasi, Mungu ulipaye kisasi, utuangazie sisi.
2 Ee Mhukumu wa dunia, inuka, uwalipize wenye kiburi kama wanavyostahili.
Inuka, muhukumu wa nchi, uwape wenye majivuno kile wanachosahili.
3 Hata lini, waovu, Ee Bwana, hata lini waovu watashangilia?
Mpaka lini waovu, Yahwe, mpaka lini waovu watafurahia?
4 Wanamimina maneno ya kiburi, watenda mabaya wote wamejaa majivuno.
Wanamwaga maneno yao ya kiburi; wote watendao uovu wanajivuna.
5 Ee Bwana, wanawaponda watu wako, wanawaonea urithi wako.
Wanawaangamiza watu wako, Yahwe; wanalitesa taifa ambao ni milki yako.
6 Wanamchinja mjane na mgeni, na kuwaua yatima.
Wanamuua mjane na mgeni aishiye nchini mwao, na wanamuua yatima.
7 Nao husema, “Bwana haoni, Mungu wa Yakobo hafahamu.”
Nao husema, “Yahwe hawezi kuona, Mungu wa Yakobo hayagundui haya.”
8 Sikizeni, enyi wajinga miongoni mwa watu; enyi wapumbavu, lini mtakuwa na hekima?
Tambueni, ninyi watu wajinga! Enyi wapumbavu, mtajifunza lini?
9 Je, aliyeweka sikio asisikie? Aliyeumba jicho asione?
Yeye aliye liumba sikio, hasikii? Yeye aliye litengeneza jicho, haoni?
10 Je, anayeadhibisha mataifa asiadhibu? Je, awafundishaye wanadamu asiwe na maarifa?
Yeye awaadhibuye mataifa, hayuko sahihi? Yeye ndiye ampaye maarifa mwanadamu.
11 Bwana anajua mawazo ya mwanadamu; anajua kwamba ni ubatili.
Yahwe anayajua mawazo ya wanadamu, kuwa ni mvuke.
12 Ee Bwana, heri mtu anayeadhibishwa na wewe, mtu unayemfundisha kwa sheria yako,
Amebarikiwa yule ambaye umuongozaye, Yahwe, yule ambaye wewe humfundisha kutoka katika sheria yako.
13 unampa utulivu siku za shida, mpaka shimo litakapokuwa limechimbwa kwa ajili ya mwovu.
Wewe humpa pumziko wakati wa shida mpaka shimo litakapokuwa limechimbwa kwa ajili ya waovu.
14 Kwa kuwa Bwana hatawakataa watu wake, hatauacha urithi wake.
Maana Yahwe hatawaacha watu wake wala kutelekeza warithi wake.
15 Hukumu itasimamishwa tena kwenye haki, wote walio na mioyo minyofu wataifuata.
Kwa kuwa tena hukumu itakuwa ya haki; na wote walio wanyoofu wa moyo wataifuata.
16 Ni nani atakayeinuka dhidi ya mwovu kwa ajili yangu? Ni nani atakayenikinga dhidi ya watenda maovu?
Ni nani atainuka kunitetea dhidi ya watendao uovu? Ni nani atasimama dhidi ya waovu kwa ajili yangu?
17 Kama Bwana asingelinisaidia upesi, ningelikuwa ninaishi katika ukimya wa kifo.
Kama Yahwe asingelikuwa msaada wangu, haraka ningekuwa nimelala mahali pa ukimya.
18 Niliposema, “Mguu wangu unateleza,” Ee Bwana, upendo wako ulinishikilia.
Niliposema, mguu wangu unateleza,” Uaminifu wa agano lako, Yahwe, uliniinua.
19 Wakati wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu, faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu.
Wasiwasi uwapo mwingi ndani yangu, faraja yako hunifurahisha.
20 Je, kiti cha utawala wa udhalimu kitajiunga nawe, ule utawala uletao taabu kutokana na sheria zake?
Kiti cha uharibifu chaweza kushirikiana nawe, kitungacho madhara kwa njia ya sheria?
21 Huungana kuwashambulia wenye haki, kuwahukumu kufa wasio na hatia.
Wao kwa pamoja hupanga njama kuwaua wenye haki na kuwahukumu adhabu ya kifo wenye haki.
22 Lakini Bwana amekuwa ngome yangu, na Mungu wangu amekuwa mwamba ninaoukimbilia.
Lakini Yahwe amekuwa mnara wangu mrefu, na Mungu wangu amekuwa mwamba wa kimbilio langu.
23 Yeye atawalipa kwa ajili ya dhambi zao na atawaangamiza kwa ajili ya maovu yao; Bwana Mungu wetu atawaangamiza.
Yeye atawarudishia uovu wao wenyewe na atawaangamiza katika uovu wao wenyewe. Yahwe Mungu wetu atawaangamiza.

< Zaburi 94 >