< Zaburi 90 >

1 Maombi ya Mose, mtu wa Mungu. Bwana, wewe umekuwa makao yetu katika vizazi vyote.
Bwana, wewe umekuwa kimbilio letu vizazi vyote.
2 Kabla ya kuzaliwa milima au hujaumba dunia na ulimwengu, wewe ni Mungu tangu milele hata milele.
Kabla milima haijaumbwa, wala haujaumba nchi na dunia, tangu milele na milele, wewe ni Mungu.
3 Huwarudisha watu mavumbini, ukisema, “Rudini mavumbini, enyi wanadamu.”
Humrudisha mtu mavumbini, na kusema, “Rudi, ewe uzao wa mwanadmu.
4 Kwa maana kwako miaka elfu ni kama siku moja iliyokwisha pita, au kama kesha la usiku.
Kwa maana miaka elfu machoni pako ni kama jana ipitapo, na kama saa wakati wa usiku.
5 Unawatowesha wanadamu katika usingizi wa kifo, nao ni kama majani machanga ya asubuhi:
Huwafagia kama vile kwa mafuliko nao hulala; na wakati wa asubuhi wako kama majani yameayo.
6 ingawa asubuhi yanachipua, ifikapo jioni huwa yamenyauka na kukauka.
Asubuhi yachipuka na kumea; jioni yakatika na kukauka.
7 Tumeangamizwa kwa hasira yako na tumetishwa kwa ghadhabu yako.
Hakika, tumeangamizwa kwa hasira yako, na gadhabu yako inatuogopesha sana.
8 Umeyaweka maovu yetu mbele yako, dhambi zetu za siri katika nuru ya uwepo wako.
Umeudhihirisha uovu wetu mbele zako, na dhambi zetu zilizofichika katika nuru ya uwepo wako.
9 Tumeishi siku zetu zote chini ya ghadhabu yako, tunamaliza miaka yetu kwa kuomboleza.
Uhai wetu unatoweka chini ya gadhabu yako; Miaka yetu inapita haraka kama pumzi.
10 Siku zetu za kuishi ni miaka sabini, au miaka themanini ikiwa tuna nguvu, lakini yote ni ya shida na taabu, nazo zapita haraka, nasi twatoweka.
Miaka yetu ni sabini, au themanini tukiwa na afya; lakini hata hivyo miaka yetu mizuri imetiwa alama ya taabu na huzuni. Ndiyo, inapita haraka, kisha tunatoweka.
11 Ni nani ajuaye nguvu za hasira yako? Kwa maana ghadhabu yako ni kubwa kama hofu tunayopaswa kuwa nayo kwako.
Ni nani ajuaye kiwango cha hasira yako, na ghadhabu yako ambayo iko sawa na hofu yako?
12 Tufundishe kuzihesabu siku zetu vizuri, ili tujipatie moyo wa hekima.
Hivyo utufundishe sisi kuyafikiria maisha yetu ili kwamba tuweze kuishi kwa hekima.
13 Ee Bwana, uwe na huruma! Utakawia hata lini? Wahurumie watumishi wako.
Ugeuke, Ee Yahwe! Mpaka lini itakuwa hivi? Uwahurumie watumishi wako.
14 Tushibishe asubuhi kwa upendo wako usiokoma, ili tuweze kuimba kwa shangwe na kufurahi siku zetu zote.
Ututosheleze sisi wakati wa asubuhi kwa uaminifu wa agano lako ili kwamba tuweze kufurahi na kushangilia siku zote za maisha yetu.
15 Utufurahishe kulingana na siku ulizotuadhibu, kulingana na miaka tuliyotaabika.
Utufurahishe kwa uwiano sawa na zile siku ulizo tutesa na kwa ile miaka tuliyopitia taabu.
16 Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, utukufu wako kwa watoto wao.
Watumishi wako na waione kazi yako, na watoto wetu wauone ukuu enzi yako.
17 Wema wa Bwana Mungu wetu uwe juu yetu; uzithibitishe kazi za mikono yetu: naam, uzithibitishe kazi za mikono yetu.
Na neema ya Bwana Mungu wetu iwe yetu; fanikisha kazi za mikono yetu; hakika, fanikisha kazi ya mikono yetu.

< Zaburi 90 >