< Zaburi 9 >

1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa muth-labeni. Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, nitakutukuza kwa moyo wangu wote, nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.
Nitamshukuru Yahweh kwa moyo wangu wote; nitayasimulia matendo yako makuu.
2 Nitafurahi na kushangilia ndani yako. Nitaliimbia sifa jina lako, Ewe Uliye Juu Sana.
Nitafurahi na kushangilia katika wewe; nitaliimbia jina lako, Wewe uliye juu.
3 Adui zangu wamerudi nyuma, wamejikwaa na kuangamia mbele zako.
Maadui zangu wanaponirudia, hujikwaa na kuangamia mbele zako.
4 Kwa maana umetetea haki yangu na msimamo wangu; umeketi kwenye kiti chako cha enzi, ukihukumu kwa haki.
Kwa kuwa umenitetea kwa haki; unakaa kwenye kiti chako cha enzi, ukihukumu kwa haki!
5 Umekemea mataifa na kuwaangamiza waovu; umeyafuta majina yao milele na milele.
Uliwakemea mataifa; umewaharibu waovu; na kuwa futilia mbali jina lao milele na milele.
6 Uharibifu usiokoma umempata adui, umeingʼoa miji yao; hata kumbukumbu lao limetoweka.
Maadui wamebomoka kama magofu ulipo pindua miji yao. Kumbukumbu yao yote imepotea.
7 Bwana anatawala milele, ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu.
Bali Yahweh anadumu milele; ameweka kiti chake cha enzi kwa ajili ya haki.
8 Mungu atahukumu ulimwengu kwa haki, atatawala mataifa kwa haki.
Naye atauhukumu ulimwengu kwa haki, na atatekeleza hukumu kwa ajili ya mataifa kwa haki.
9 Bwana ni kimbilio la watu wanaoonewa, ni ngome imara wakati wa shida.
Yahweh pia atakuwa ngome kwake aliye onewa, na ngome wakati wa shida.
10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe, kwa maana wewe Bwana, hujawaacha kamwe wakutafutao.
Wale wakujuao jina lako wanaamini katika Wewe, kwa ajili yako, Yahweh, usiwaache wale wakutafutao.
11 Mwimbieni Bwana sifa, amefanywa mtawala Sayuni, tangazeni miongoni mwa mataifa, yale aliyoyatenda.
Mwibieni sifa Yahweh, anaye tawala katika Sayuni; waambieni mataifa yale aliyo yatenda.
12 Kwa maana yeye alipizaye kisasi cha damu hukumbuka, hapuuzi kilio cha wanaoonewa.
Kwa kuwa Mungu alipizae kisasi cha damu hukumbuka; naye hasahau kilio cha anayeonewa.
13 Ee Bwana, tazama jinsi walivyo wengi adui zangu wanaonitesa! Nihurumie, uniinue kutoka malango ya mauti,
Unihurumie, Yahweh; tazama vile ninavyo onewa na wale wanao nichukia, wewe ambaye unaweza kunikwapua katika lango la kifo.
14 ili niweze kutangaza sifa zako katika malango ya Binti Sayuni na huko niushangilie wokovu wako.
Oh, ili niweze kutangaza sifa zako. Katika lango la binti sayuni nitaufurahia wokovu wako!
15 Mataifa wameanguka kwenye shimo walilolichimba, miguu yao imenaswa kwenye wavu waliouficha.
Mataifa yamedidimia chini katika shimo ambalo walilolitengeneza; miguu yao imenaswa kwenye nyavu walioificha wenyewe.
16 Bwana anajulikana kwa haki yake, waovu wamenaswa katika kazi za mikono yao.
Yahweh amejidhihilisha; na kutekeleza hukumu; waovu wameangamia kwa matendo yao wenyewe. (Selah)
17 Waovu wataishia kuzimu, naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu. (Sheol h7585)
Waovu wamekataliwa na kupelekwa kuzimu, mataifa yote yanayo msahau Mungu. (Sheol h7585)
18 Lakini mhitaji hatasahaulika siku zote, wala matumaini ya walioonewa hayatapotea.
Kwa kuwa mhitaji hata sahauliwa siku zote, wala matumaini ya wanyonge hayatapotea milele.
19 Ee Bwana, inuka, usimwache binadamu ashinde. Mataifa na yahukumiwe mbele zako.
Inuka, Yahweh, usimruhusu mtu kutushinda; mataifa na wahukumiwe mbele zako.
20 Ee Bwana, wapige kwa hofu, mataifa na yajue kuwa wao ni watu tu.
Bwana, waogopeshe; mataifa waweze kutambua kuwa ni wanadamu tu. (Selah)

< Zaburi 9 >