< Zaburi 9 >
1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa muth-labeni. Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, nitakutukuza kwa moyo wangu wote, nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.
2 Nitafurahi na kushangilia ndani yako. Nitaliimbia sifa jina lako, Ewe Uliye Juu Sana.
3 Adui zangu wamerudi nyuma, wamejikwaa na kuangamia mbele zako.
4 Kwa maana umetetea haki yangu na msimamo wangu; umeketi kwenye kiti chako cha enzi, ukihukumu kwa haki.
5 Umekemea mataifa na kuwaangamiza waovu; umeyafuta majina yao milele na milele.
6 Uharibifu usiokoma umempata adui, umeingʼoa miji yao; hata kumbukumbu lao limetoweka.
7 Bwana anatawala milele, ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu.
8 Mungu atahukumu ulimwengu kwa haki, atatawala mataifa kwa haki.
9 Bwana ni kimbilio la watu wanaoonewa, ni ngome imara wakati wa shida.
10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe, kwa maana wewe Bwana, hujawaacha kamwe wakutafutao.
11 Mwimbieni Bwana sifa, amefanywa mtawala Sayuni, tangazeni miongoni mwa mataifa, yale aliyoyatenda.
12 Kwa maana yeye alipizaye kisasi cha damu hukumbuka, hapuuzi kilio cha wanaoonewa.
13 Ee Bwana, tazama jinsi walivyo wengi adui zangu wanaonitesa! Nihurumie, uniinue kutoka malango ya mauti,
14 ili niweze kutangaza sifa zako katika malango ya Binti Sayuni na huko niushangilie wokovu wako.
15 Mataifa wameanguka kwenye shimo walilolichimba, miguu yao imenaswa kwenye wavu waliouficha.
16 Bwana anajulikana kwa haki yake, waovu wamenaswa katika kazi za mikono yao.
17 Waovu wataishia kuzimu, naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu. (Sheol )
18 Lakini mhitaji hatasahaulika siku zote, wala matumaini ya walioonewa hayatapotea.
19 Ee Bwana, inuka, usimwache binadamu ashinde. Mataifa na yahukumiwe mbele zako.
20 Ee Bwana, wapige kwa hofu, mataifa na yajue kuwa wao ni watu tu.