< Zaburi 85 >

1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Ee Bwana, ulionyesha wema kwa nchi yako. Ulimrejeshea Yakobo baraka zake.
Yahwe, wewe umeonesha fadhilia kwenye nchi yako; umeurejesha ustawi wa Yakobo.
2 Ulisamehe uovu wa watu wako, na kufunika dhambi zao zote.
Umesamehe dhambi ya watu wako; umezisitiri dhambi zao zote. (Selah)
3 Uliweka kando ghadhabu yako yote na umegeuka na kuiacha hasira yako kali.
Umeondoa ghadhabu yako yote; umeiacha hasira yako kali.
4 Ee Mungu Mwokozi wetu, uturejeshe tena, nawe uiondoe chuki yako juu yetu.
Uturejeshe sisi, Ee Mungu wa wokovu wetu, na uikomeshe chuki yako juu yetu.
5 Je, utatukasirikia milele? Utaendeleza hasira yako kwa vizazi vyote?
Je! Utaendelea kuwa na hasira juu yetu milele? utadumisha hasira kizazi chote kijacho?
6 Je, hutatuhuisha tena, ili watu wako wakufurahie?
Je, hautatuhuisha tena? Kisha watu wako watafurahia katika wewe.
7 Utuonyeshe upendo wako usiokoma, Ee Bwana, utupe wokovu wako.
Utuoneshe sisi uaminifu wa agano lako, Yahwe, utupe sisi wokovu wako.
8 Nitasikiliza lile atakalosema Mungu aliye Bwana; anaahidi amani kwa watu wake, watakatifu wake: lakini nao wasirudie upumbavu.
Nitasikiliza yale Yahwe Mungu asemayo, maana yeye atafanya amani pamoja na watu wake, wafuasi wake waminifu. Lakini lazima wasirudi tena katika njia za kipumbavu.
9 Hakika wokovu wake uko karibu na wale wamchao, ili utukufu wake udumu katika nchi yetu.
Hakika wokovu wake u karibu na wale wanao mwabudu yeye; kisha utukufu utabaki katika nchi yetu.
10 Upendo na uaminifu hukutana pamoja, haki na amani hubusiana.
Uaminifu wa agano na uaminifu vimekutana pamoja; haki na amani vimebusiana.
11 Uaminifu huchipua kutoka nchi, haki hutazama chini kutoka mbinguni.
Uaminifu unatoa chemchem kutoka ardhini, na haki hutazama chini kutoka mawinguni.
12 Naam, hakika Bwana atatoa kilicho chema, nayo nchi yetu itazaa mavuno yake.
Ndiyo, Yahwe atatoa baraka zake njema, na nchi itatoa mazao yake.
13 Haki itatangulia mbele yake na kutengeneza njia kwa ajili ya hatua zake.
Haki itaenda mbele zake na kufanya njia kwa ajili ya nyayo zake.

< Zaburi 85 >