< Zaburi 8 >
1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, Bwana wetu, tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Umeuweka utukufu wako juu ya mbingu.
Yahweh Bwana wetu, ni jinsi gani jina lako ni tukufu katika dunia yote, wewe ufunuaye utukufu wako juu mbinguni.
2 Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao umeamuru sifa, kwa sababu ya watesi wako, kumnyamazisha adui na mlipiza kisasi.
Kutoka katika midomo ya watoto na vichanga umeumba sifa kwa sababu ya utukufu wako, ili kuwanyamazisha maadui wote na walipa kisasi wote.
3 Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota, ulizoziratibisha,
Ninapozitazama mbingu, ambazo vidole vyako vimeumba, mwezi na nyota, ambazo umeziweka kila mmoja katika nafasi yake,
4 mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria, binadamu ni nani hata unamjali?
Binadamu ni nani hata umtazame, na watu hata uwajali wao?
5 Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni, ukamvika taji ya utukufu na heshima.
Umewaumba chini kidogo kuliko viumbe vya mbinguni na umewazunguka na utukufu na heshima.
6 Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako; umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.
Umemfanya binadamu kutawala kazi ya mikono yako; umeviweka vitu vyote chini ya miguu yake:
7 Mifugo na makundi yote pia, naam, na wanyama wa kondeni,
kondoo na ng'ombe wote, na hata wanyama wa porini,
8 ndege wa angani na samaki wa baharini, naam, kila kiogeleacho katika njia za bahari.
ndege wa angani, na samaki wa baharini, na vyote vipitavyo katika mikondo ya bahari.
9 Ee Bwana, Bwana wetu, tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
Yahweh Bwana wetu, ni jinsi gani jina lako ni tukufu katika dunia yote!