< Zaburi 79 >
1 Zaburi ya Asafu. Ee Mungu, mataifa yameuvamia urithi wako, wamelinajisi Hekalu lako takatifu, wameifanya Yerusalemu kuwa magofu.
Zaburi ya Asafu. Mungu, Mataifa ya kigeni yameingia kwenye urithi wako; wamelinajisi hekalu lako takatifu; wameigeuza Yerusalemu kuwa chungu cha magofu.
2 Wametoa maiti za watumishi kuwa chakula cha ndege wa angani na nyama ya watakatifu wako kwa wanyama wa nchi.
Wamezitoa maiti za watumishi wako ziwe chakula cha ndege wa angani, miili ya watakatifu wako iwe chakula cha wanyama wa nchi.
3 Wamemwaga damu kama maji kuzunguka Yerusalemu yote, wala hakuna yeyote wa kuwazika.
Wamemwaga damu zao kama maji sehemu zote za Yesrusalemu, na hakuwepo wa kuwazika.
4 Tumekuwa kitu cha aibu kwa jirani zetu, cha dharau na mzaha kwa wale wanaotuzunguka.
Sisi tumekuwa aibu kwa majirani zetu, tukidhihakiwa na kuzomewa na wale wanaotuzunguka.
5 Hata lini, Ee Bwana? Je, wewe utakasirika milele? Wivu wako utawaka kama moto hadi lini?
Mpaka lini Yahwe? Utabaki kuwa na hasira milele? Ni kwa muda gani hasira yako ya wivu itawaka kama moto?
6 Mwaga ghadhabu yako kwa mataifa yasiyokukubali, juu ya falme za hao wasioliitia jina lako,
Mwaga hasira yako juu ya mataifa ambayo hayakujui wewe na ufalme ambao hauliiti jina lako.
7 kwa maana wamemrarua Yakobo na kuharibu nchi ya makao yake.
Kwa maana walimvamia Yakobo na waliharibu kijiji chake.
8 Usituhesabie dhambi za baba zetu, huruma yako na itujie hima, kwa maana tu wahitaji mno.
Usiendelee kukumbuka dhambi za baba zetu dhidi yetu; matendo yako ya huruma yaje kwetu, maana tuko chini.
9 Ee Mungu Mwokozi wetu, utusaidie, kwa ajili ya utukufu wa jina lako; tuokoe na kutusamehe dhambi zetu kwa ajili ya jina lako.
Utusaidie, Mungu wa wokovu wetu, kwa ajili ya utukufu wa jina lako; utuokoe na usamehe dhambi zetu kwa ajili ya jina lako.
10 Kwa nini mataifa waseme, “Yuko wapi Mungu wenu?” Mbele ya macho yetu, dhihirisha kati ya mataifa kwamba unalipiza kisasi damu iliyomwagwa ya watumishi wako.
Kwa nini mataifa yalazimike kusema, “Mungu wao yuko wapi?” Damu ya watumishi wako ambayo ilimwagwa na ilipize kisasi juu ya mataifa mbele ya macho yako.
11 Kilio cha huzuni cha wafungwa kifike mbele zako; kwa nguvu za mkono wako hifadhi wale waliohukumiwa kufa.
Kilio cha wafungwa na kije mbele zako; kwa uweza wa nguvu zako uwaweke ai wana wa mauti.
12 Walipize jirani zetu mara saba vifuani mwao aibu walizovurumisha juu yako, Ee Bwana.
Uwalipize majirani zetu vifuani mwao mara saba zaidi ya walivyo kutukana wewe, Bwana.
13 Ndipo sisi watu wako, kondoo wa malisho yako, tutakusifu milele; toka kizazi hadi kizazi tutasimulia sifa zako.
Hivyo sisi watu wako na kondoo wa malisho yako tutakushukuru milele. Tutazisimulia sifa zako kwa vizazi vyote.