< Zaburi 77 >

1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Asafu. Nilimlilia Mungu ili anisaidie, nilimlilia Mungu ili anisikie.
Nitampazia Mungu sauti yangu, nitamuita Mungu kwa sauti yangu, na Mungu wangu atanisikia.
2 Nilipokuwa katika taabu, nilimtafuta Bwana, usiku nilinyoosha mikono bila kuchoka na nafsi yangu ilikataa kufarijika.
Katika siku ya taabu nilimtafuta Bwana; usiku niliinua mikono yangu, nayo haikuchoka. Moyo wangu ulikataa kufarijiwa.
3 Ee Mungu, nilikukumbuka wewe, nikalia kwa huzuni; nikatafakari, roho yangu ikadhoofika.
Ningali nikiugua nilielekeza mawazo yangu kwa Mungu. Nilimfikiria Mungu nilipokuwa dhaifu. (Selah)
4 Ulizuia macho yangu kufumba; nilikuwa nasumbuka, nikashindwa kusema.
Uliyafanya macho yangu yasisinzie; nilisumbuka sana kuongea.
5 Nilitafakari juu ya siku zilizopita, miaka mingi iliyopita,
Nilifikiri kuhusu siku za kale, kuhusu mambo yaliyopita muda mrefu.
6 nilikumbuka nilivyoimba nyimbo usiku. Moyo wangu ulitafakari na roho yangu ikauliza:
Wakati wa usiku niliukumbuka wimbo niliouimba mara moja. Nilifikiria kwa makini na kujaribu kuelewa kile kilichokuwa kimetokea.
7 “Je, Bwana atakataa milele? Je, hatatenda mema tena?
Je, Mungu atanikataa milele? Je, hatanionesha tena huruma?
8 Je, upendo wake usio na mwisho umetoweka milele? Je, ahadi yake imekoma nyakati zote?
Je, uaminifu wa agano lake ulikuwa umetoweka milele? Je, ahadi yake imeshindwa milele?
9 Je, Mungu amesahau kuwa na huruma? Je, katika hasira amezuia huruma yake?”
Je, Mungu amesahau kuwa mwenye neema? Je, hasira yake imeifunga huruma yake? (Selah)
10 Ndipo nikawaza, “Huu ndio udhaifu wangu: lakini nitakumbuka miaka ya mkono wa kuume wa Aliye Juu Sana.”
Nilisema, “Hii ni huzuni yangu: mabadiliko ya mkono wa kuume wa Aliye Juu dhidi yetu.”
11 Nitayakumbuka matendo ya Bwana; naam, nitaikumbuka miujiza yako ya zamani.
Lakini nitayakumbuka matendo yako, Yahwe; nitafikiri kuhusu matendo yako makuu yaliyopita.
12 Nitazitafakari kazi zako zote na kuyawaza matendo yako makuu.
Nitayatafakari matendo yako yote nami nitayaishi.
13 Ee Mungu, njia zako ni takatifu. Ni mungu yupi aliye mkuu kama Mungu wetu?
Njia yako, Mungu, ni takatifu; ni mungu gani wa kulinganishwa na Mungu wetu aliye mkuu?
14 Wewe ndiwe Mungu utendaye miujiza, umeonyesha uwezo wako katikati ya mataifa.
Wewe ni Mungu utendaye maajabu; wewe umeonesha nguvu zako kati ya mataifa.
15 Kwa mkono wako wenye nguvu umewakomboa watu wako, uzao wa Yakobo na Yosefu.
Uliwapa watu wako ushindi kwa uweza wako mkuu - ukoo wa Yakobo na Yusufu. (Selah)
16 Maji yalikuona, Ee Mungu, maji yalikuona yakakimbia, vilindi vilitetemeka.
Maji yalikuona wewe, Mungu; maji yalikuona wewe, nayo yakaogopa; vina vya maji vilitetemeka.
17 Mawingu yalimwaga maji, mbingu zikatoa ngurumo kwa radi, mishale yako ikametameta huku na huko.
Mawingu yalitiririsha maji chini; anga zito lilitoa sauti; mishale yako ilipita kati.
18 Ngurumo yako ilisikika katika upepo wa kisulisuli, umeme wako wa radi ukaangaza dunia, nchi ikatetemeka na kutikisika.
Sauti yako kama ya radi ilisikika katika upepo; radi iliwasha dunia; nchi iliogopa na kutetemeka.
19 Njia yako ilipita baharini, mapito yako kwenye maji makuu, ingawa nyayo zako hazikuonekana.
Njia yako ilipita baharini na mapito yako katika maji mengi, lakini alama za miguu yako hazikuonekana.
20 Uliongoza watu wako kama kundi kwa mkono wa Mose na Aroni.
Uliwaongoza watu wako kama kundi kwa mkono wa Musa na Haruni.

< Zaburi 77 >