< Zaburi 73 >
1 Zaburi ya Asafu. Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, kwa wale ambao mioyo yao ni safi.
Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, kwa wale walio na moyo safi.
2 Bali kwangu mimi, miguu yangu ilikuwa karibu kuteleza; nilikuwa karibu mguu wangu kuachia uliposimama.
Lakini kwangu mimi, kidogo tu miguu yangu iteleze; miguu yangu karibu iteleze kutoka kwangu
3 Kwa maana niliwaonea wivu wenye kujivuna nilipoona kufanikiwa kwa waovu.
kwa sababu niliwaonea wivu wenye kiburi nilipoona mafanikio ya waovu.
4 Wao hawana taabu, miili yao ina afya na nguvu.
Kwa maana hawana maumivu hadi kufa kwao, lakini wana nguvu na wameshiba.
5 Hawapati shida zinazowataabisha watu wengine, wala hawapati mapigo kama wanadamu wengine.
Wako huru dhidi ya mizigo ya watu wengine; nao hawateswi kama watu wengine.
6 Kwa hiyo kiburi ni mkufu wao, wamejivika jeuri.
Kiburi kinawapamba kama mkufu kwenye shingo zao; jeuri huwavika kama vazi.
7 Uovu hutoka katika mioyo yao iliyokufa ganzi, majivuno maovu kutoka mioyoni mwao hauna kikomo.
Katika upofu wa jinsi hii dhambi huja; mawazo maovu hupita mioyoni mwao.
8 Hudhihaki na kusema kwa ukorofi, katika majivuno yao wanatishia kutesa.
Wao hudhihaki na kuongea kwa namna ya uovu; kwa kiburi chao hutishia mateso.
9 Vinywa vyao huweka madai hata kwa mbingu, nazo ndimi zao humiliki duniani.
Wameweka vinywa vyao dhidi ya mbingu, na ndimi zao hutanga tanga duniani.
10 Kwa hiyo watu wao huwageukia na kunywa maji tele.
Kwa hiyo watu wake huwageukia na maji yaliyojaa hukaushwa.
11 Wanasema, “Mungu awezaje kujua? Je, Yeye Aliye Juu Sana anayo maarifa?”
Nao husema, “Mungu anajuaje? Yako maarifa kwake yeye aliye juu?”
12 Hivi ndivyo walivyo waovu: siku zote hawajali, wanaongezeka katika utajiri.
Fahamu: watu hawa ni waovu; mara zote hawajali, wakifanyika matajiri na matajiri.
13 Hakika nimeuweka moyo wangu safi bure, ni bure nimenawa mikono yangu nisiwe na hatia.
Hakika nimeutunza moyo wangu bure na nimenawa mikono yangu pasipo kukosa.
14 Mchana kutwa nimetaabika, nimeadhibiwa kila asubuhi.
Maana mchana kutwa nimeteswa na kuadhibiwa kila asubuhi.
15 Kama ningesema, “Nitasema hivi,” ningelikuwa nimewasaliti watoto wako.
Kama ningesema, “Ningesema mambo haya,” kumbe nigewasaliti kizazi hiki cha watoto wenu.
16 Nilipojaribu kuelewa haya yote, yalikuwa magumu kwangu kuelewa.
Ingawa nilijaribu kuyaelewa mambo haya, yalikuwa ni magumu sana kwangu.
17 Mpaka nilipoingia patakatifu pa Mungu, ndipo nilipotambua mwisho wao.
Ndipo nilipoingia patakatifu pa Mungu na kuelewa hatma yao.
18 Hakika unawaweka mahali pa utelezi, unawaangusha chini kwa uharibifu.
Hakika wewe huwaweka penye utelezi; huwaangusha mpaka palipoharibika.
19 Tazama jinsi wanavyoangamizwa ghafula, wanatoweshwa kabisa na vitisho!
Jinsi gani wamekuwa ukiwa kwa muda mfupi! Wamefika mwisho nao wamemaliza kwa utisho.
20 Kama ndoto mtu aamkapo, hivyo wakati uinukapo, Ee Bwana, utawatowesha kama ndoto.
Wao ni kama ndoto wakati wa mtu kuamka; Bwana, utakapo inuka, utazidharau ndoto zao.
21 Wakati moyo wangu ulipohuzunishwa, na roho yangu ilipotiwa uchungu,
Maana moyo wangu ulipata uchungu, nami nilijeruhiwa sana.
22 nilikuwa mpumbavu na mjinga, nilikuwa mnyama mkatili mbele yako.
Nilikuwa mjinga na sijui neno; nilikuwa kama mnyama tu mbele yako.
23 Hata hivyo niko pamoja nawe siku zote, umenishika mkono wangu wa kuume.
Lakini mimi nipo pamoja nawe daima; umenishika mkono wa kuume.
24 Unaniongoza kwa shauri lako, hatimaye utaniingiza katika utukufu.
Utaniongoza kwa shauri lako na baadaye utanipokea katika utukufu.
25 Nani niliye naye mbinguni ila wewe? Dunia haina chochote ninachokitamani ila wewe.
Ni nani niliye naye mbinguni isipokuwa wewe? Hakuna nimtamaniye duniani isipokuwa wewe.
26 Mwili na moyo wangu vyaweza kushindwa, bali Mungu ni nguvu ya moyo wangu na fungu langu milele.
Mwili wangu na moyo wangu huwa dhaifu, bali Mungu ndiye nguvu ya moyo wangu daima.
27 Wale walio mbali nawe wataangamia, unawaangamiza wote wasio waaminifu kwako.
Wale walio mbali nawe wataangamia; utawaangamiza wote wasio waaminifu kwako.
28 Lakini kwangu mimi, ni vyema kuwa karibu na Mungu. Nimemfanya Bwana Mwenyezi kimbilio langu; nami nitayasimulia matendo yako yote.
Lakini mimi, linipasalo kufanya ni kumkaribia Mungu. Nimemfanya Bwana Yahwe kimbilio langu. Nami nitayatangaza matendo yako yote.