< Zaburi 68 >
1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Wimbo. Mungu na ainuke, watesi wake watawanyike, adui zake na wakimbie mbele zake.
Mungu ainuke, maadui zake watawanyike; pia wale wamchukiao wakimbie mbele zake.
2 Kama vile moshi upeperushwavyo na upepo, vivyo hivyo uwapeperushe mbali, kama vile nta iyeyukavyo kwenye moto, vivyo hivyo waovu na waangamie mbele za Mungu.
Kama moshi uondoshwavyo, hivyo uwaondoshe wao; kama nta iyeyukavo mbele ya moto, hivyo waovu waangamizwe uweponi mwa Mungu.
3 Bali wenye haki na wafurahi, washangilie mbele za Mungu, wafurahi na kushangilia.
Bali wenye haki wafurahi; washangilie mbele za Mungu; washangilie na kufurahi.
4 Mwimbieni Mungu, liimbieni sifa jina lake, mtukuzeni yeye aendeshwaye juu ya mawingu: jina lake ni Bwana, furahini mbele zake.
Mwimbieni Mungu! Lisifuni jina lake! Msifuni yule aendeshaye farasi kwenye tambarare ya bonde la Mto Yordani! Yahwe ni jina lake! Shangilieni mbele zake!
5 Baba wa yatima, mtetezi wa wajane, ni Mungu katika makao yake matakatifu.
Baba wa yatima, na mwamuzi wa wajane, ni Mungu anayeishi mahali patakatifu.
6 Mungu huwaweka wapweke katika jamaa, huwaongoza wafungwa wakiimba, bali waasi huishi katika nchi kame.
Mungu huwaweka wakiwa katika familia; yeye huwafungua wafungwa kwa kuimba bali waasi huishi katika ardhi kavu.
7 Ee Mungu, ulipowatangulia watu wako, ulipopita nyikani,
Mungu, wewe ulipoenda mbele ya watu wako, ulipotembea kupitia jangwani, (Selah)
8 dunia ilitikisika, mbingu zikanyesha mvua, mbele za Mungu, Yule wa Sinai, mbele za Mungu, Mungu wa Israeli.
nchi ilitetemeka; mbingu pia zilidondosha mvua katika uwepo wa Mungu, uweponi mwa Mungu wakati alipokuja Sinai, uweponi mwa Mungu, Mungu wa Israeli.
9 Ee Mungu, ulinyesha mvua nyingi na kuiburudisha ardhi iliyokuwa imechoka.
Wewe, Mungu, ulituma mvua nyingi; uliuimarisha urithi wako wakati ulipokuwa umechoka.
10 Ee Mungu, watu wako waliishi huko, nawe kwa wingi wa utajiri wako uliwapa maskini mahitaji yao.
Watu wako waliishi humo; Wewe, Mungu, uliutoa kwa wema wako kwa maskini.
11 Bwana alitangaza neno, waliolitangaza neno hilo walikuwa kundi kubwa:
Bwana alitoa amri, na wale walio zitangaza walikuwa ni jeshi kuu.
12 “Wafalme na majeshi walikimbia upesi, watu waliobaki kambini waligawana nyara.
Wafalme wa majeshi wanakimbia, wanakimbia, na wanawake wakisubiri nyumbani kuvigawana wao na familia zao vilivyotekwa nyara.
13 Hata ulalapo katikati ya mioto ya kambini, mabawa ya njiwa wangu yamefunikwa kwa fedha, manyoya yake kwa dhahabu ingʼaayo.”
Njiwa walio vikwa fedha wakiwa na mabawa ya njano ya dhahabu. Wakati baadhi ya watu wakikaa kati ya mifugo ya kondoo, kwa nini umefanya haya?
14 Wakati Mwenyezi alipowatawanya wafalme katika nchi, ilikuwa kama theluji iliyoanguka juu ya Salmoni.
Mwenyezi Mungu aliwatawanya Wafalme huko, ilikuwa kama vile wakati wa theluji juu ya Mlima Salmoni.
15 Milima ya Bashani ni milima iliyotukuka, milima ya Bashani ina vilele vilivyochongoka.
Mlima mkubwa ni milima wa mji wa Bashani; mlima mrefu ni mlima wa mji wa Bashani.
16 Enyi milima yenye vilele vilivyochongoka, kwa nini mnakazia macho kwa wivu, katika mlima Mungu anaochagua kutawala, ambako Bwana mwenyewe ataishi milele?
Ewe mlima mrefu wa nchi, kwa nini unatazama kwa jicho la husuda, kwenye mlima ambao Mungu ameutaka kwa ajili ya mahali ambapo yeye ataishi? Hakika, Yahwe ataishi humo milele.
17 Magari ya Mungu ni makumi ya maelfu, na maelfu ya maelfu; Bwana amekuja kutoka Sinai hadi katika patakatifu pake.
Magari ya Mungu ni ishirini elfu, maelfu juu ya maelfu; Bwana yu kati yao katika mahari patakatifu, kama katika Sinai.
18 Ulipopanda juu, uliteka mateka, ukapokea vipawa kutoka kwa wanadamu, hata kutoka kwa wale walioasi, ili wewe, Ee Bwana Mungu, upate kuishi huko.
Wewe umepaa juu; uliwaongoza mateka; umepokea zawadi kutoka kati ya watu, hata kutoka kwa wale waliopigana dhidi yako, ili kwamba wewe, Yahwe Mungu, uweze kuishi huko.
19 Sifa apewe Bwana, Mungu Mwokozi wetu, ambaye siku kwa siku hutuchukulia mizigo yetu.
Abarikiwe Bwana, atubebeaye mizigo yetu, Mungu ambaye ni wokovu wetu. (Selah)
20 Mungu wetu ni Mungu aokoaye, Bwana Mwenyezi hutuokoa na kifo.
Mungu wetu ni Mungu aokoaye; Yahwe Bwana ni yule awezaye kutuokoa sisi dhidi ya kifo.
21 Hakika Mungu ataponda vichwa vya adui zake, vichwa vya hao waendao katika njia za dhambi.
Lakini Bwana atapiga vichwa vya adui zake, mpaka kwenye ngozi ya kichwa yenye nywele ya wale watembeao katika makosa dhidi yake.
22 Bwana alisema, “Nitawarudisha kutoka Bashani; nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari,
Bwana alisema, “Nitawarudisha adui zangu kutoka Bashani; nitawarudisha kutoka katika kina cha bahari
23 ili uweze kuchovya miguu yako katika damu ya adui zako, huku ndimi za mbwa wako zikiwa na fungu lake.”
ili kwamba upate kuwaangamiza adui zako, ukichovya mguu wako katika damu, na ili kwamba ndimi za mbwa wako zipate mlo wao kutoka kwa adui zenu.”
24 Ee Mungu, maandamano yako yameonekana, maandamano ya Mungu wangu, Mfalme wangu, yakielekea patakatifu pake.
Mungu, wameona maandamano yako, maandamano ya Mungu wangu, Mfalme wangu, kwenye mahali patakatifu.
25 Mbele wako waimbaji, baada yao wapiga vinanda, pamoja nao wako wanawali wakipiga matari.
Waimbaji walitangulia, walifuatiwa na wapiga muziki, na katikati walikuwa wanawali wakicheza ngoma.
26 Msifuni Mungu katika kusanyiko kubwa, msifuni Bwana katika kusanyiko la Israeli.
Mtukuzeni Mungu katika kusanyiko; msifuni Yahwe, ninyi ukoo wa kweli wa Israeli.
27 Liko kabila dogo la Benyamini likiwaongoza, wakifuatwa na kundi kubwa la watawala wa Yuda, hatimaye watawala wa Zabuloni na Naftali.
Kuna Benjamini kwanza, kabila dogo, kisha viongozi wa Yuda na watu wao, viongozi wa Zabuloni na viongozi wa Naftali.
28 Ee Mungu, amuru uwezo wako, Ee Mungu tuonyeshe nguvu zako, kama ulivyofanya hapo awali.
Mungu wenu, Israeli, ameamuru nguvu zenu; uzifunue kwetu nguvu zako, Mungu, kama ulivyo zifunua wakati uliopita.
29 Kwa sababu ya Hekalu lako Yerusalemu wafalme watakuletea zawadi.
Uzifunue nguvu zako kwetu toka katika hekalu la Yerusalemu, ambako wafalme huleta zawadi kwako.
30 Mkemee mnyama aliyeko kwenye manyasi, kundi la mafahali katikati ya ndama za mataifa. Na walete minara ya madini ya fedha wakinyenyekea. Tawanya mataifa yapendayo vita.
Pigeni kelele katika vita dhidi ya wanyama wa porini katika mianzi, dhidi ya watu, lile kundi la mafahari na ndama. Wafedhehesheni na kuwalazimisha wawaletee zawadi; watawanyeni watu wapendao kupigana vita.
31 Wajumbe watakuja kutoka Misri, Kushi atajisalimisha kwa Mungu.
Wakuu watatoka katika Misri; Ethiopia itafanya haraka kuufikisha mkono wake kwa Mungu.
32 Mwimbieni Mungu, enyi falme za dunia, mwimbieni Bwana sifa,
Mwimbieni Mungu, enyi falme za nchi; (Selah) mwimbieni sifa Yahwe.
33 mwimbieni sifa yeye apandaye mbingu za kale zilizo juu, yeye angurumaye kwa sauti kuu.
Kwake yeye apitaye juu ya mbingu za mbingu, zilizokuwepo tangu zama za kale; tazama, yeye hupiga kelele kwa nguvu
34 Tangazeni uwezo wa Mungu, ambaye fahari yake iko juu ya Israeli, ambaye uwezo wake uko katika anga.
Tangazeni kuwa Mungu ni mwenye nguvu; enzi yake iko juu ya Israeli, na nguvu zake ziko angani.
35 Ee Mungu, wewe unatisha katika mahali patakatifu pako, Mungu wa Israeli huwapa watu wake uwezo na nguvu. Mungu Asifiwe!
Mungu, mahali pako patakatifu panatisha; Mungu wa Israeli, yeye huwapa watu wake nguvu na uweza. Atukuzwe Mungu.