< Zaburi 66 >

1 Kwa mwimbishaji. Wimbo. Zaburi. Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote!
Mpigieni Mungu kelele za shangwe, nchi yote;
2 Imbeni utukufu wa jina lake; mpeni sifa zake kwa utukufu!
Imbeni utukufu wa jina lake; mzitukuze sifa zake.
3 Mwambieni Mungu, “Jinsi gani yalivyo ya kutisha matendo yako! Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba adui wananyenyekea mbele zako.
Mwambieni Mugu, “Matendo yako yanatisha kama nini! Kwa ukuu wa nguvu zako maadui zako watajisalimisha kwako.
4 Dunia yote yakusujudia, wanakuimbia wewe sifa, wanaliimbia sifa jina lako.”
Nchi yote watakuabudu wewe na watakuimbia wewe; wataliimbia jina lako.” (Selah)
5 Njooni mwone yale Mungu aliyoyatenda, mambo ya kutisha aliyoyatenda miongoni mwa wanadamu!
Njoni na mtazame kazi za Mungu; yeye anatisha katika matendo yake awatendeayo wanadamu.
6 Alifanya bahari kuwa nchi kavu, wakapita kati ya maji kwa miguu, njooni, tumshangilie.
Aligeuza bahari kuwa nchi kavu; wao walitembea kwa mguu juu ya mto; huko tulishangilia katika yeye.
7 Yeye hutawala kwa uwezo wake milele, macho yake huangalia mataifa yote: waasi wasithubutu kujiinua dhidi yake.
Yeye anatawala milele kwa nguvu zake; macho yake yanachunguza mataifa; waasi wasijivune. (Selah)
8 Enyi mataifa, msifuni Mungu wetu, sauti ya sifa yake isikike,
Mtukuzeni Mungu, enyi watu wa mataifa yote, sauti ya sifa zake isikike.
9 ameyahifadhi maisha yetu na kuizuia miguu yetu kuteleza.
Yeye atuwekaye hai, naye hairuhusu miguu yetu iteleze.
10 Ee Mungu, wewe ulitujaribu, ukatusafisha kama fedha.
Kwa maana wewe, Mungu, umetupima sisi, wewe umetupima kama inavyopimwa fedha.
11 Umetuingiza kwenye nyavu na umetubebesha mizigo mizito migongoni mwetu.
Wewe ulituingiza sisi kwenye wavu; uliweka mzigo mzito viunoni mwetu.
12 Uliwaruhusu watu watukalie vichwani, tulipita kwenye moto na kwenye maji, lakini ulituleta kwenye nchi iliyojaa utajiri tele.
Wewe uliwafanya watu wasafiri juu ya vichwa vyetu; tulipita motoni na majini, lakini ukatuleta mahali pa wazi palipo salama.
13 Nitakuja hekaluni mwako na sadaka za kuteketezwa na kukutimizia nadhiri zangu:
Nitaingia nyumbani mwako nikiwa na sadaka ya kuteketezwa; nitakulipa viapo vyangu
14 nadhiri ambazo midomo yangu iliahidi na nilizotamka kwa kinywa changu nilipokuwa katika shida.
ambavyo midomo yangu iliahidi na kinywa changu kiliongea nilipokuwa katika dhiki.
15 Nitakutolea dhabihu za wanyama wanono na sadaka za kondoo dume, nitakutolea mafahali na mbuzi.
Nitakutolea sadaka ya kuteketezwa ya wanyama wanene pamoja na harufu nzuri ya kondoo waume; Nitatoa ng'ombe na mbuzi. (Selah)
16 Njooni msikilize ninyi nyote mnaomcha Mungu, nami niwaambie aliyonitendea.
Njoni, msikie, ninyi nyote mnao mwabudu Mungu, nami nitatangaza yale yeye aliyoitendea roho yangu.
17 Nilimlilia kwa kinywa changu, sifa zake zilikuwa katika ulimi wangu.
Nilimlilia kwa kinywa changu, naye alipendezwa na ulimi wangu.
18 Kama ningekuwa nimeyaficha maovu moyoni mwangu, Bwana asingekuwa amenisikiliza;
Kama ningelikuwa na dhambi ndani ya moyo wangu, Bwana asingenisikiliza.
19 lakini hakika Mungu amenisikiliza na amesikia sauti yangu katika maombi.
Lakini Mungu hakika amesikia; amesikia sautiya kuomba kwangu.
20 Sifa apewe Mungu, ambaye hakulikataa ombi langu wala kunizuilia upendo wake!
Atukuzwe Mungu, ambaye hakuyakataa maombi yangu wala kuweka uaminifu wa agano lake mbali nami.

< Zaburi 66 >