< Zaburi 63 >
1 Zaburi ya Daudi. Wakati alipokuwa katika Jangwa la Yuda. Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu, nakutafuta kwa moyo wote; nafsi yangu inakuonea kiu, mwili wangu unakuonea wewe shauku, katika nchi kame na iliyochoka mahali ambapo hapana maji.
Mungu, wewe ni Mungu wangu! Ninakutafuta wewe kwa bidii, moyo wangu unakiu yako, mwili wangu unakutamani sana wewe, katika ukame na nchi iliyochoka mahali ambapo hakuna maji.
2 Nimekuona katika mahali patakatifu na kuuona uwezo wako na utukufu wako.
Hivyo nimekutafuta wewe katika watu watakatifu kuona nguvu zako na utukufu wako.
3 Kwa sababu upendo wako ni bora kuliko uhai, midomo yangu itakuadhimisha.
Kwa sababu uaminifu wa agano lako ni bora kuliko uhai, midomo yangu itakusifu wewe.
4 Nitakusifu siku zote za maisha yangu, na kwa jina lako nitainua mikono yangu.
Hivyo nitakutukuza wewe niwapo hai; kwa jina lako nitainua mikono yangu juu.
5 Nafsi yangu itatoshelezwa kama kwa wingi wa vyakula; kwa midomo iimbayo kinywa changu kitakusifu wewe.
Itakuwa kana kwamba nilikula mlo wa mafuta na wenye kunona, kwa midomo ya furaha kinywa changu kitakusifu wewe,
6 Kitandani mwangu ninakukumbuka wewe, ninawaza juu yako makesha yote ya usiku.
nikufikiripo kitandani mwangu na kukutafakari wewe wakati wa saa za usiku.
7 Kwa sababu wewe ndiwe msaada wangu, chini ya uvuli wa mbawa zako naimba.
Kwa maana umekuwa msaada wangu, na katika uvuli wa mbawa zako ninafurahia.
8 Nafsi yangu inaambatana nawe, mkono wako wa kuume hunishika.
Ninashikamana nawe; mkono wako wa kuume unanisaidia.
9 Wale wanaotafuta uhai wangu wataharibiwa, watakwenda chini kwenye vilindi vya dunia.
Lakini wale watafutao kuuharibu uhai wangu wataenda chini kwenye sehemu ya chini kabisa ya nchi;
10 Watatolewa wafe kwa upanga, nao watakuwa chakula cha mbweha.
watakabidhiwa kwa wale ambao mikono yao hutumia upanga, nao watakuwa chakula cha mbweha.
11 Bali mfalme atafurahi katika Mungu, wale wote waapao kwa jina la Mungu watamsifu, bali vinywa vya waongo vitanyamazishwa.
Bali mfalme atashangilia katika Mungu; yeyote anaye apa kupitia yeye atajivunia yeye, lakini vinywa ya wale wasemao uongo watanyamazishwa.