< Zaburi 61 >

1 Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za uimbaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, sikia kilio changu, usikilize maombi yangu.
Sikia kulia kwangu, shughulikia maombi yangu.
2 Kutoka miisho ya dunia ninakuita, ninaita huku moyo wangu unadhoofika; uniongoze kwenye mwamba ule ulio juu kuliko mimi.
Kutokea mwisho wa nchi nitakuita wewe wakati moyo wangu umeelemewa; uniongoze kwenye mwamba ulio juu kuliko mimi.
3 Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu, ngome imara dhidi ya adui.
Maana wewe umekuwa kimbilio langu la usalama, nguzo imara dhidi ya adui.
4 Natamani kukaa hemani mwako milele, na kukimbilia chini ya uvuli wa mbawa zako.
Uniache niishi hemani mwako milele! Nipate kimbilio salama chini ya makazi ya mbawa zako. (Selah)
5 Ee Mungu, kwa kuwa umesikia nadhiri zangu, umenipa urithi wa wale wanaoliogopa jina lako.
Kwa kuwa wewe, Mungu, umesikia viapo vyangu, wewe umenipa mimi urithi wa wale wanao liheshimu jina lako.
6 Mwongezee mfalme siku za maisha yake, miaka yake kwa vizazi vingi.
Wewe utaongeza maisha ya mfalme; miaka yake itakuwa kama vizazi vingi.
7 Yeye na atawazwe kwenye kiti cha enzi mbele za Mungu milele; amuru upendo wako na uaminifu wako vimlinde.
Yeye atabakia mbele ya Mungu milele.
8 Ndipo daima nitaliimbia sifa jina lako na kuzitimiza nadhiri zangu siku baada ya siku.
Nitaliimbia sifa jina lako milele ili kwamba niweze kufanya viapo vyangu kila siku.

< Zaburi 61 >