< Zaburi 59 >
1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi. Wakati Sauli alipotuma wapelelezi nyumbani mwa Daudi ili wamuue. Ee Mungu, uniokoe na adui zangu, unilinde kutokana na hao wanaoinuka dhidi yangu.
2 Uniponye na watu watendao mabaya, uniokoe kutokana na wamwagao damu.
3 Tazama wanavyonivizia! Watu wakali wananifanyia hila, ingawa Ee Bwana, mimi sijakosea wala kutenda dhambi.
4 Sijatenda kosa; hata hivyo wako tayari kunishambulia. Inuka unisaidie, uone hali yangu mbaya!
5 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli! Zinduka uyaadhibu mataifa yote, usionyeshe huruma kwa wasaliti.
6 Hurudi wakati wa jioni, wakibweka kama mbwa, wakiuzurura mji.
7 Tazama yale wanayotema kutoka vinywa vyao, hutema upanga kutoka midomo yao, nao husema, “Ni nani atakayetusikia?”
8 Lakini wewe, Bwana, uwacheke; unayadharau mataifa hayo yote.
9 Ee nguvu yangu, ninakutazama wewe, wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,
10 Mungu wangu unipendaye. Mungu atanitangulia, naye atanifanya niwachekelee wale wanaonisingizia.
11 Lakini usiwaue, Ee Bwana, ngao yetu, au sivyo watu wangu watasahau. Katika uwezo wako wafanye watangetange na uwashushe chini.
12 Kwa ajili ya dhambi za vinywa vyao, kwa ajili ya maneno ya midomo yao, waache wanaswe katika kiburi chao. Kwa ajili ya laana na uongo wanaotamka,
13 wateketeze katika ghadhabu, wateketeze hadi wasiwepo tena. Ndipo itakapofahamika katika miisho ya dunia kwamba Mungu anatawala juu ya Yakobo.
14 Hurudi jioni, wakibweka kama mbwa, wakiuzurura mji.
15 Wanatangatanga wakitafuta chakula, wasipotosheka hubweka kama mbwa.
16 Lakini mimi nitaziimba nguvu zako, asubuhi nitaimba juu ya upendo wako; kwa maana wewe ndiwe ngome yangu na kimbilio langu wakati wa shida.
17 Ee uliye Nguvu zangu, ninakuimbia sifa. Wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu, Mungu unipendaye.