< Zaburi 58 >
1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi. Enyi watawala, je, kweli mwanena kwa haki? Je, mnahukumu kwa unyofu miongoni mwa watu?
2 La, mioyoni mwenu mnatunga udhalimu, na mikono yenu hupima jeuri duniani.
3 Waovu ni wapotovu tangu kuzaliwa kwao, toka tumboni mwa mama zao ni wakaidi na husema uongo.
4 Sumu yao ni kama sumu ya nyoka, kama ile ya fira ambaye ameziba masikio yake,
5 ambaye hatasikia sauti ya kutumbuiza ya mwaguzi, hata kama mganga angecheza kwa ustadi kiasi gani.
6 Ee Mungu, yavunje meno katika vinywa vyao; Ee Bwana, vunja meno makali ya hao simba!
7 Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi, wavutapo pinde zao, mishale yao na iwe butu.
8 Kama konokono ayeyukavyo akitembea, kama mtoto aliyezaliwa akiwa mfu, wasilione jua.
9 Kabla vyungu vyenu havijapata moto wa kuni za miiba, zikiwa mbichi au kavu, waovu watakuwa wamefagiliwa mbali.
10 Wenye haki watafurahi waonapo wakilipizwa kisasi, watakapochovya nyayo zao katika damu ya waovu.
11 Ndipo wanadamu watasema, “Hakika utulivu wa wenye haki bado una thawabu, hakika kuna Mungu ahukumuye dunia.”