< Zaburi 56 >
1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Njiwa mkimya wa mbali.” Utenzi wa Daudi. Baada ya kukamatwa na Wafilisti huko Gathi. Ee Mungu unihurumie, maana watu wananifuatia vikali; mchana kutwa wanazidisha mashambulizi yao.
Uwe na huruma nami, Mungu, kwa maana watu wananishambulia! Muda wote wale wanao pigana nami hunikaribia zaidi ili wanishambulie.
2 Wasingiziaji wangu wananifuatia mchana kutwa, wengi wananishambulia kwa kiburi chao.
Adui zangu hunikanyaga muda wote; maana ni wengi ambao kwa kiburi hupigana dhidi yangu.
3 Wakati ninapoogopa, nitakutumaini wewe.
Wakati nina woga, nitaweka imani yangu katika wewe.
4 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu, katika Mungu ninatumaini; sitaogopa. Mwanadamu apatikanaye na kufa, atanitenda nini?
Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu - nimeweka imani yangu katika Mungu; sitaogopa; mtu wa kawaida atanifanya nini?
5 Mchana kutwa wanayageuza maneno yangu, siku zote wanapanga shauri la kunidhuru.
Muda wote wanayageuza maneno yangu; mawazo yao yote yako kinyume na mimi kwa ajili ya uovu.
6 Wananifanyia hila, wanajificha, wanatazama hatua zangu, wakiwa na shauku ya kuutoa uhai wangu.
Wanajikusanya kwa pamoja, wanajificha wenyewe, na kuzifuatilia hatua zangu, wakisubiri kuniua.
7 Wasiepuke kwa vyovyote, Ee Mungu, katika hasira yako yaangushe mataifa.
Usiwaache waikimbie adhabu yako kwa ajili ya uovu wao. Uwaangushe watu chini katika hasira yako, Mungu.
8 Andika maombolezo yangu, orodhesha machozi yangu katika gombo lako: je, haya hayapo katika kumbukumbu zako?
Wewe unahesabu kutangatanga kwangu na kuweka machozi yangu kwenye chupa yako; je, hayako kitabuni mwako?
9 Ndipo adui zangu watarudi nyuma ninapoita msaada. Kwa hili nitajua kwamba Mungu yuko upande wangu.
Ndipo maadui zangu watakimbia katika siku ile nikuitapo wewe; hili najua, kwamba Mungu yupo kwa ajili yangu.
10 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu, katika Bwana, ambaye neno lake ninalisifu,
Katika Mungu ambaye neno lake ninalisifu, katika Yahwe ambaye neno lake ninalisifu,
11 katika Mungu ninatumaini, sitaogopa. Mwanadamu anaweza kunitenda nini?
katika Mungu ninaamini, sitaogopa. Yeyote atanifanya nini?
12 Ee Mungu, nina nadhiri kwako, nitakutolea wewe sadaka zangu za shukrani.
Wajibu wa kutimiza viapo vyangu kwako uko juu yangu, Mungu; nitatoa sadaka ya shukurani.
13 Kwa kuwa umeniokoa toka kwenye mauti na miguu yangu kwenye kujikwaa, ili niweze kuenenda mbele za Mungu katika nuru ya uzima.
Kwa kuwa umeokoa uhai wangu na mauti; umezuia miguu yangu isianguke, ili kwamba niweze kutembea mbele ya Mungu katika nuru ya uhai.