< Zaburi 52 >

1 Kwa mwimbishaji. Utenzi wa Daudi. Baada ya Doegi, Mwedomu kumwendea Sauli na kumjulisha kuwa: “Daudi amekwenda nyumbani kwa Ahimeleki.” Ewe jitu, mbona unajivunia ubaya? Kwa nini unajivuna mchana kutwa, wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu? 2 Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi. Ni kama wembe mkali, ninyi mfanyao hila. 3 Unapenda mabaya kuliko mema, uongo kuliko kusema kweli. 4 Unapenda kila neno lenye kudhuru, ewe ulimi wenye hila! 5 Hakika Mungu atakushusha chini kwa maangamizi ya milele: atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu kutoka hema yako, atakungʼoa kutoka nchi ya walio hai. 6 Wenye haki wataona na kuogopa, watamcheka, wakisema, 7 “Huyu ni yule mtu ambaye hakumfanya Mungu kuwa ngome yake, bali alitumainia wingi wa utajiri wake, na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!” 8 Lakini mimi ni kama mti wa mzeituni unaostawi katika nyumba ya Mungu, nautegemea upendo wa Mungu usiokoma milele na milele. 9 Nitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda, nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema. Nitakusifu mbele ya watakatifu wako.

< Zaburi 52 >