< Zaburi 50 >

1 Zaburi ya Asafu. Mwenye Nguvu, Mungu, Bwana, asema na kuiita dunia, tangu mawio ya jua hadi mahali pake liendapo kutua.
Mungu, Mwenye nguvu, Yahwe, amenena naye aliita nchi toka mawio ya jua mpaka machweo yake.
2 Kutoka Sayuni, penye uzuri mkamilifu, Mungu anaangaza.
Tokea Sayuni, Mungu ameangaza, ukamilifu wa uzuri.
3 Mungu wetu anakuja na hatakaa kimya, moto uteketezao unamtangulia, akiwa amezungukwa na tufani kali.
Mungu wetu huja naye hakai kimya; mbele yake moto hula, na kuna dhoruba kubwa karibu naye.
4 Anaziita mbingu zilizo juu, na nchi, ili aweze kuwahukumu watu wake:
Yeye huziita mbingu zilizo juu na nchi ili kwamba aweze kuwahukumu watu wake:
5 “Nikusanyieni watu wangu waliowekwa wakfu, waliofanya agano nami kwa dhabihu.”
Kwa pamoja kusanyikeni waaminifu wangu kwangu, wale waliofanya nami agano kwa sadaka.”
6 Nazo mbingu zinatangaza haki yake, kwa maana Mungu mwenyewe ni hakimu.
Mbingu zitatangaza haki yake, kwa maana Mungu mwenyewe ndiye jaji. Serah
7 “Sikieni, enyi watu wangu, nami nitasema, ee Israeli, nami nitashuhudia dhidi yenu: Mimi ndimi Mungu, Mungu wenu.
Sikilizeni, watu wangu, nami nitazungumza; mimi ni Mungu, Mungu wenu.
8 Sikukemei kwa sababu ya dhabihu zako, au sadaka zako za kuteketezwa, ambazo daima ziko mbele zangu.
Sitawakaripia ninyi kwa ajili ya sadaka zenu; sadaka zenu za kuteketeza ziko nami siku zote.
9 Sina haja ya fahali wa banda lako, au mbuzi wa zizi lako.
Sitachukua ng'ombe katika nyumba yenu, wala beberu katika mazizi yenu.
10 Kwa maana kila mnyama wa msituni ni wangu, na pia makundi ya mifugo juu ya vilima elfu.
Kwa maana kila mnyama wa msituni ni wangu, nao ng'ombe kwenye milima elfu ni wangu.
11 Ninamjua kila ndege mlimani, nao viumbe wa kondeni ni wangu.
Ninawajua ndege wa mlimani, na wanyama pori katika shamba ni wangu.
12 Kama ningekuwa na njaa, nisingewaambia ninyi, kwa maana ulimwengu ni wangu, pamoja na vyote vilivyomo ndani yake.
Kama ningekuwa na njaa, nisingewaambia ninyi; maana ulimwengu ni wangu, na vyote vilivyomo.
13 Je, mimi hula nyama ya mafahali au kunywa damu ya mbuzi?
Je! sitakula nyama ya ngombe na kunywa damu ya mbuzi?
14 Toa sadaka za shukrani kwa Mungu, timiza nadhiri zako kwake Yeye Aliye Juu Sana,
Mtoleeni Mungu sadaka za shukurani, na mlipe viapo vyenu kwa Aliye Juu.
15 na uniite siku ya taabu; nami nitakuokoa, nawe utanitukuza.”
Mniite katika siku ya shida; nami nitawaokoa
16 Lakini kwake mtu mwovu, Mungu asema: “Una haki gani kunena sheria zangu au kuchukua agano langu midomoni mwako?
Lakini kwa waovu Mungu anasema, “Inawahusu nini kuitangaza hali yangu, kwamba ninyi mmeliweka agano langu mdomoni mwenu,
17 Unachukia mafundisho yangu na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.
wakati ninyi mnayachukia maelekezo na mnayatupa maneno yangu?
18 Unapomwona mwizi, unaungana naye, unapiga kura yako pamoja na wazinzi.
Mumuanapo mwizi, ninyi hukubaliana naye; ninyi na mnashirikiana na wale wafanyao uasherati.
19 Unakitumia kinywa chako kwa mabaya na kuuongoza ulimi wako kwa hila.
Mwautoa mdomo wenu kwa mabaya, huelezea udanganyifu.
20 Wanena daima dhidi ya ndugu yako na kumsingizia mwana wa mama yako.
Mnakaa na kuongea dhidi ya ndugu yenu; na kukashfu mwana wa mama yenu.
21 Mambo haya unayafanya, nami nimekaa kimya, ukafikiri Mimi nami ni kama wewe. Lakini nitakukemea na kuweka mashtaka mbele yako.
Mmefanya mambo haya, lakini nimekaa kimya, hivyo mlidhani kuwa ni mtu flani nilliye kama ninyi mlivyo. Lakini nitawakaripia ninyi na kuwafunua, mbele ya macho yenu, mambo yote miliyofanya.
22 “Yatafakarini haya, ninyi mnaomsahau Mungu, ama sivyo nitawararua vipande vipande, wala hapatakuwepo na yeyote wa kuwaokoa:
Mlitilie maanani hili, ninyi mnao msahau Mungu, vinginevyo nitawakata ninyi vipande vipande, na hatakuwepo yeyote wakuja kuwasaidia!
23 Atoaye dhabihu za shukrani ananiheshimu mimi, naye aiandaa njia yake ili nimwonyeshe wokovu wa Mungu.”
Yule atoaye sadaka ya shukurani hunitukuza, na yeyote apangaye njia zake katika namna iliyo sahihi nitamuonesha wokovu wa Mungu.”

< Zaburi 50 >