< Zaburi 42 >
1 Kwa mwimbishaji. Utenzi wa wana wa Kora. Kama vile ayala aoneavyo shauku vijito vya maji, ndivyo nafsi yangu ikuoneavyo shauku, Ee Mungu.
Kama ayala ayatamanivyo maji ya mto. ndivyo hivyo ninakiu yako, Mungu.
2 Nafsi yangu inamwonea Mungu kiu, Mungu aliye hai. Ni lini nitaweza kwenda kukutana na Mungu?
Ninakiu yako Mungu, Mungu uliye hai, ni lini nitaonekana mbele zako?
3 Machozi yangu yamekuwa chakula changu usiku na mchana, huku watu wakiniambia mchana kutwa, “Yuko wapi Mungu wako?”
Machozi yangu yamekuwa ni chakula changu mchana na usiku, wakati maadui zangu siku zote wanasema, “Yuko wapi Mungu wako?”
4 Mambo haya nayakumbuka ninapoimimina nafsi yangu: Jinsi nilivyokuwa nikienda na umati wa watu, nikiongoza maandamano kuelekea kwenye nyumba ya Mungu, kwa kelele za shangwe na za shukrani katikati ya umati uliosherehekea.
Mambo haya niayakumbuka ninapoumimina roho yangu: nilipoenda na umati wa watu na kuwaongoza kwenye nyumba ya Mungu kwa sauti ya shangwe na kusifu, ni wengi tulisherekea.
5 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka? Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu? Weka tumaini lako kwa Mungu, kwa sababu bado nitamsifu, Mwokozi wangu na
Roho yangu, kwa nini unainama? Kwa nini unahuzuni ndani yangu? Mtumaini Mungu, Kwa kuwa kwa mara nyingine nitamsifu yeye ambaye ni wokovu wangu.
6 Mungu wangu. Nafsi yangu inasononeka ndani yangu; kwa hiyo nitakukumbuka kutoka nchi ya Yordani, katika vilele vya Hermoni, kutoka Mlima Mizari.
Mungu wangu, roho yangu imeinama ndani yangu, kwa hiyo ninakukumbuka toka nchi ya Yordani, toka kwenye vilele vitatu vya mlima Hermoni, na toka mlima wa Mizari.
7 Kilindi huita kilindi, katika ngurumo za maporomoko ya maji yako; mawimbi yako yote pamoja na viwimbi vimepita juu yangu.
Kina huita kina kwenye kelele za maporomoko ya maji yako; mawimbi na mafuriko yako yote yako juu yangu.
8 Mchana Bwana huelekeza upendo wake, usiku wimbo wake uko nami: maombi kwa Mungu wa uzima wangu.
Wakati wa mchana Yahwe ataamuru uaminifu wa agano lake; na usiku wimbo wake utakuwa nami, ombi kwa Mungu wa uhai wangu.
9 Ninamwambia Mungu Mwamba wangu, “Kwa nini umenisahau? Kwa nini niendelee kuomboleza, nikiwa nimeonewa na adui?”
Nami nitasema kwa Mungu wangu, mwamba wangu, “Kwa nini umenisahau? Kwa nini ninaenenda katika maombolezo kwa sababu ya ukandamizaji wa adui yangu?”
10 Mifupa yangu inateseka kwa maumivu makali adui zangu wanaponidhihaki, wakiniambia mchana kutwa, “Yuko wapi Mungu wako?”
Kama upanga mifupani pangu, maadui zangu wananikemea, siku zote wakiniambia, “Yuko wapi Mungu wako?”
11 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka? Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu? Weka tumaini lako kwa Mungu, kwa sababu bado nitamsifu, Mwokozi wangu na Mungu wangu.
Roho yangu, kwa nini umeinama chini? Kwa nini unahuzuni ndani yangu? Mtumaini Mungu kwa kuwa nitamsifu tena yeye aliye wokovu wangu na Mungu wangu.