< Zaburi 40 >

1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Nilimngoja Bwana kwa saburi, naye akaniinamia, akasikia kilio changu.
Nalimungoja Yahwe kwa uvumilivu; alinisikia na kusika kilio changu.
2 Akanipandisha kutoka shimo la uharibifu, kutoka matope na utelezi; akaiweka miguu yangu juu ya mwamba na kunipa mahali imara pa kusimama.
Yeye akanitoa nje ya shimo la kutisha, nje ya matope, naye aliiweka miguu yangu juu ya mwamba na kuzifanya hatua zangu salama.
3 Akaweka wimbo mpya kinywani mwangu, wimbo wa sifa kwa Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa na kuweka tumaini lao kwa Bwana.
Yeye ameweka wimbo mpya mdomoni mwangu, sifa kwa Mungu. Wengi watauona na kumheshimu yeye na kumwamini Yahwe.
4 Heri mtu yule amfanyaye Bwana kuwa tumaini lake, asiyewategemea wenye kiburi, wale wenye kugeukia miungu ya uongo.
Amebarikiwa mtu yule ambaye humfanya Yahwe tumaini lake naye hathamini majivuno wala wale wanaokengeuka kwa uongo.
5 Ee Bwana Mungu wangu, umefanya mambo mengi ya ajabu. Mambo uliyopanga kwa ajili yetu hakuna awezaye kukuhesabia; kama ningesema na kuyaelezea, yangekuwa mengi mno kuyaelezea.
Yahwe Mungu wangu, matendo ya ajabu ambayo wewe umeyafanya, ni mengi, na mawazo yako yatuhusuyo sisi hayahesabiki; Ikiwa ningetangaza na kuyazungumza kwao, ni mengi sana hayahesabiki.
6 Dhabihu na sadaka hukuvitaka, lakini umefungua masikio yangu; sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukuzihitaji.
Wewe haufurahishwi katika sadaka au matoleo, bali wewe umeyafungua masikio yangu; wala haukuhitaji sadaka ya kuteketeza au sadaka ya dhambi.
7 Ndipo niliposema, “Mimi hapa, nimekuja: imeandikwa kunihusu katika kitabu.
Ndipo nilisema mimi, “Tazama, nimekuja; imeandikwa kuhusu mimi katika kitabu cha hati.
8 Ee Mungu wangu, natamani kuyafanya mapenzi yako; sheria yako iko ndani ya moyo wangu.”
Ninafurahia kuyafanya mapenzi yako, Mungu wangu; sheria zako ziko moyoni mwangu.”
9 Nimehubiri haki katika kusanyiko kubwa, sikufunga mdomo wangu, Ee Bwana, kama ujuavyo.
Katika kusanyiko kubwa nimetangaza habari njema ya haki yako; Yahwe, wewe unajua sikuizuia midomo yangu.
10 Sikuficha haki yako moyoni mwangu; ninasema juu ya uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha upendo wako na kweli yako mbele ya kusanyiko kubwa.
Sikuficha haki yako moyoni mwangu; nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako; sijaficha uaminifu wa agano lako au uaminifu wako kwenye kusanyiko kubwa.
11 Ee Bwana, usizuilie huruma zako, upendo wako na kweli yako daima vinilinde.
Usiache kunitendea kwa rehema, Yahwe; Uaminifu wa agano lako na uaminifu wako unihifadhi siku zote.
12 Kwa maana taabu zisizo na hesabu zimenizunguka, dhambi zangu zimenikamata, hata nisiweze kuona. Zimekuwa nyingi kuliko nywele za kichwa changu, nao moyo unazimia ndani yangu.
Mabaya yasiyo hesabika yamenizunguka; Maovu yangu yamenipata nami siwezi kuona chochote; nayo ni mengi kuliko nywele za kichwa changu, na moyo wangu umeniangusha.
13 Ee Bwana, uwe radhi kuniokoa; Ee Bwana, njoo hima unisaidie.
Yahwe, tafadhari uniokoe; njoo haraka unisaidie Yahwe.
14 Wote wanaotafuta kuuondoa uhai wangu, waaibishwe na kufadhaishwa; wote wanaotamani kuangamizwa kwangu, warudishwe nyuma kwa aibu.
Waaibike na wafedheheke kabisa wanaufuatilia uhai wangu wauondoe. Warudishwe nyuma na wadharaulike, wale wanaofurahia kuniumiza.
15 Wale waniambiao, “Aha! Aha!” wafadhaishwe na iwe aibu yao.
Waogopeshwe kwa sababu ya aibu yao, wale waniambiao, “Aha, aha!”
16 Lakini wote wakutafutao washangilie na kukufurahia, wale wapendao wokovu wako siku zote waseme, “Bwana atukuzwe!”
Bali wale wote wakutafutao wafurahi na kushangilia katika wewe; na kila mmoja apendaye wokovu wako aseme daima, “Asifiwe Yahwe.”
17 Lakini bado mimi ni maskini na mhitaji; Bwana na anifikirie. Wewe ndiwe msaada wangu na Mwokozi wangu; Ee Mungu wangu, usikawie.
Mimi ni maskini na muhitaji; lakini Bwana hunifikiria. Wewe ni msaada wangu nawe huja kuniokoa; usichelewe, Mungu wangu.

< Zaburi 40 >