< Zaburi 39 >
1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi. Nilisema, “Nitaziangalia njia zangu na kuuzuia ulimi wangu usije ukatenda dhambi; nitaweka lijamu kinywani mwangu wakati wote waovu wanapokuwa karibu nami.”
Niliamua, “Nitakuwa mwangalifu kwa kile nisemacho ili kwamba nisitende dhambi kwa ulimi wangu. Nitaufumba mdomo wangu niwapo uweponi mwa mtu mwovu.”
2 Lakini niliponyamaza kimya na kutulia, hata pasipo kusema lolote jema, uchungu wangu uliongezeka.
Nilikaa kimya; Nilizuia maneno yangu hata kuongea lolote zuri, na maumivu yangu yalizidi sana.
3 Moyo wangu ulipata moto ndani yangu, nilipotafakari, moto uliwaka, ndipo nikasema kwa ulimi wangu:
Moyo wangu ukawaka moto; nilipoyatafakari mambo haya, yaliniunguza kama moto. Ndipo mwishowe niliongea.
4 “Ee Bwana, nijulishe mwisho wa maisha yangu na hesabu ya siku zangu; nijalie kujua jinsi maisha yangu yanavyopita upesi.
Yahwe, unijulishe ni lini utakuwa mwisho wa maisha yangu na kiwango cha siku zangu. Unioneshe jinsi maisha yangu yalivyo mafupi.
5 Umefanya maisha yangu mafupi kama pumzi; muda wangu wa kuishi ni kama hauna thamani kwako. Maisha ya kila mwanadamu ni kama pumzi.
Tazama, wewe umezifanya siku zangu kama upana wa kiganja changu tu, sikuzangu za kuishi ni kama si kitu mbele zako. Hakika kila mtu ana pumzi moja. (Selah)
6 Hakika kila binadamu ni kama njozi aendapo huku na huko: hujishughulisha na mengi lakini ni ubatili; anakusanya mali nyingi, wala hajui ni nani atakayeifaidi.
Hakika kila mtu hutembea kama kivuli. Hakika kila mmoja hufanya haraka kuhusu kukusaya utajiri ingawa hawajui ni nani atazipokea.
7 “Lakini sasa Bwana, nitafute nini? Tumaini langu ni kwako.
Sasa, Bwana, ninasubiri kwa ajili ya nini? Wewe ni tumaini langu pekee.
8 Niokoe kutoka kwenye makosa yangu yote, usinifanye kuwa dhihaka ya wapumbavu.
Uniokoe na dhambi zangu; usinifanye laumu ya wabumbavu.
9 Nilinyamaza kimya, sikufumbua kinywa changu, kwa sababu wewe ndiwe uliyetenda hili.
Niko kimya na siwezi kufungua mdomo wangu, kwa sababu ni wewe ndiwe umefanya hivyo.
10 Niondolee mjeledi wako, nimeshindwa kwa mapigo ya mkono wako.
Acha kunijeruhi; nimezidiwa na pigo la mkono wako.
11 Unakemea na kuadhibu wanadamu kwa ajili ya dhambi zao; unaharibu utajiri wao kama nondo aharibuvyo: kila mwanadamu ni kama pumzi tu.
Wewe unapowaadhibu watu kwa ajili ya dhambi, huvila kama nondo vitu vyao wavitamanivyo; hakika watu si kitu bali mvuke. Serah
12 “Ee Bwana, usikie maombi yangu, usikie kilio changu unisaidie, usiwe kiziwi kwa kulia kwangu. Kwani mimi ninaishi na wewe kama mgeni, kama walivyokuwa baba zangu wote,
Sikia maombi yangu, Yahwe, na unisikilize; usikie kilio changu! Usiwe kiziwi kwangu, kwa maana niko kama mgeni pamoja nawe, kimbilio langu la usalama kama mababu zangu walivyokuwa.
13 Tazama mbali nami, ili niweze kufurahi tena kabla sijaondoka na nisiwepo tena.”
Geuzia furaha yako kwangu ili kwamba niweze kutabasamu kabla sijafa.